Home Habari za Simba Leo VITA YA NAMBA YAITESA SIMBA..FADLU DAVIDS APAGAWA

VITA YA NAMBA YAITESA SIMBA..FADLU DAVIDS APAGAWA

Habari za Simba- Ahoua

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema ana kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha kwamba anatengeneza usawa kutokana na vita ya namba iliyopo kikosini kwake huku akikiri kuwa na kikosi bora.

Pia amebainisha kuwa anatengeneza timu ya kushambulia na kuzuia kwa pamoja, hivyo anataka kila mchezaji kuwa na utimamu mzuri wa mwili ili aweze kuendana na kasi yake.

Davids amefunguka hayo muda mfupi baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Canal SC ka tika mji wa Ismailia, Misri katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.

Amesema timu imekuwa ikiimarika siku hadi siku jambo ambalo linampa wakati mzuri wa kuamini kuwa anatengeneza timu bora yenye uwiano mzuri kuanzia mchezaji anayeanza kikosini na anayeingia.

“Mchezo huu wa kwanza nimezingatia zaidi utimamu na ndio maana umechezwa kwa dakika nyingi. Nimebaini wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri eneo hilo na niliwatenga kulingana na namna kila mchezaji alikuwa na mapumziko yake baada ya msimu kwisha,” amesema na kuongeza:

“Wachezaji wangu wamekuwa wakiimarika siku hadi siku. Tangu tumefika Misri nimekuwa na muundo tofauti wa kufundisha na wao hawapo nyuma, naenda nao sawasawa na wamekuwa bora eneo hilo.”

Fadlu Davids amesema atahakikisha anawatumia wachezaji wake kwenye nafasi ambazo watakuwa bora na kuonyesha uwezo.

“Ni kazi yangu kuhakikisha nampanga mchezaji kwenye nafasi ambayo atacheza vizuri na kuisaidia timu kupata matokeo. Sitakubali kuona mchezaji anacheza vile anavyotaka bila ya uchezaji wake kuwa na manufaa kwa timu,” amesisitiza.

“Kila mchezaji anatakiwa kucheza kwa kushambulia na kukaba pamoja. Wasipokuwa na mpira wanatakiwa kuhakikisha wanautafuta pamoja.”

Akizungumzia mechi nyingine za kirafiki, amesema bado anataka mbili wiki ijayo kabla ya kurudi Tanzania kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

“Wiki ijayo mechi mbili nafikiri, baada ya kucheza kwa dakika 120 kwa mechi mbili zijazo nitatoa nafasi kwa wachezaji wote kwa kugawana ili waweze kuwa kwenye wakati mzuri wa kujijenga kabla ya wiki ya utambulisho (Simba Day),” amesema.

Naye beki wa kulia, Shomari Kapombe amesema dakika 120 walizocheza jana zilikuwa bora na walikuwa kwenye hali ya utimamu kwa muda wote.

“Kwa siku chache ambazo tupo naye (kocha) anahitaji utimamu wa mwili kwa kila mchezaji na hilo amelithibitisha kwa kuomba mchezo uchezwe dakika nyingi,” amesema Kapombe.

“Kile anachotaka tumekifanya kwa vitendo. Nafikiri ameona na kama kuna upungufu licha ya kupata ushindi ataendelea kufanyia kazi kwa siku zilizopo za maandalizi.”

Akizungumzia usajili mpya, beki huyo mkongwe amesema ujio wao ni mzuri na uwezo ni mkubwa kwani wameonyesha ubora kwa muda mfupi na namna kocha anavyojenga timu wamekuwa pamoja kama wote walikuwa pamoja msimu uliopita.

“Ujio wao ni mzuri, wameonyesha ubora na tumeweza kutengeneza muunganiko mzuri na kocha kadri siku zinavyokwenda amekuwa akitoa nafasi kwa kila mmoja kuonyesha kile alicho nacho,” amesema Kapombe.

SOMA NA HII  LUIS MIQUISSONE AZUA GUMZO KIKOSINI SIMBA