Home Habari za Yanga Leo GAMONDI AWAJIBU WANAOMSEMA CHAMA…

GAMONDI AWAJIBU WANAOMSEMA CHAMA…

Habari za Yanga- Gamondi

KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi amekiri kusikia kelele nyingi kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa soka hasa wale wa Msimbazi wakiponda usajili uliofanywa na klabu hiyo, wakidai wamesajili wazee na kuamua kuwajibu kwa kusema wasubiri msimu uanze ndio watajua hawajui.

Gamondi amesema anashukuru wataufungua msimu kwa kuvaana na Simba na kwa upande wake haangalii matokeo ya msimu uliopita, walipolala kwa penalti 3-1 katika Ngao ya Jamii bali atakomaa na mbinu kuhakikisha Yanga inarudia taji hilo.

Kocha huyo aliyasema hayo muda mchache kabla Yanga haijapaa kwenda Afrika Kusini itakapoweka kambi kwa ajili ya msimu mpya na kesho ikitarajiwa kushuka uwanjani kuvaana na Augsburg ya Ujerumani mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa michuano ya Mpumalanga Cup mechi za michuano hiyo iliyoandaliwa na TS Galaxy kisha kucheza ya tatu na Kaizer Chiefs katika michuano ya Toyota Cup.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu ratiba ya mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambao ni mabingwa watetezi alisema ni mchezo mwingine tofauti na msimu uliopita.

“Wanaweza kusema tumesajili wazee, lakini ukweli ni nina kikosi bora na ninakiamini wakati tunaenda kujiandaa zaidi nje ya nchi kabla ya kuja kucheza mechi ya Ngao ya Jamii,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Simba ni timu nzuri tutacheza nao Ngao ya Jamii, japo sitaangalia matokeo ya mchezo uliopita, siuchukulii mchezo huo kwa ukubwa, ila natamani tupate matokeo na malengo yetu makubwa ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu. Muhimu ni kusubiri kuona itakuwaje.”

Gamondi ameondoka na karibu jeshi lake lote wakiwamo mashine mpya zilizosajiliwa hivi karibuni kama Prince Dube, Duke Abuya, Clatous Chama, Aziz Andambwile, Jean Baleke, Abubakar Khomeiny na Chadrack Boka sambamba na nyota wa msimu uliopita Stephane Aziz KI, Khalid Aucho, Yao Kouassi, Kennedy Musonda, Djigui Diara, Jonas Mkude, Salum Abubakar ‘Sureboy’, huku Pacome Zouzoua akikosekana bila kuwepo kwa taarifa kwa nini kiungo mshambuliaji huyo hayupo kwenye msafara huo.

SOMA NA HII  DOUMBIA KUMBE HAJAMALIZANA NA YANGA, ISHU IKO HIVI