Home Habari za Yanga Leo YANGA KUTESTI JESHI LAKE LEO…VS FC AUGSBURG

YANGA KUTESTI JESHI LAKE LEO…VS FC AUGSBURG

HABARI ZA YANGA

KIKOSI CHA WANANCHI jioni ya leo kitashuka Uwanja wa Mbombela, uliopo Mpumangala Afrika Kusini kuvaana na FC Augsburg inayoshiriki Bundesliga ya Ujerumani, huku ikiwa imefikia na kujichimbia katika hoteli moja ya kishua itakayotumika kwa kambi ya siku 16 nchini huo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2024-25.

Yanga imefikia hoteli ya Mercure Nelspruit iliyopo katikati ya jiji la Mpumalanga, yenye vyumba 104 vya kulala wageni ikiwa kilometa 25 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kruger wa jiji hilo.

Yanga mbali na kujiandaa kwa mazoezi yao itacheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa ikiwamo ya leo saa 10:00 jioni dhidi Wajurumani, FC Augsburg kisha Julai 24 itavaana na wenyeji wao TS Galaxy ya Afrika Kusini ambao ndio waandaaji wa mashindano hayo mafupi yaliyopewa jina la Mpumalanga Cup.

Mchezo dhidi ya FC Augsburg ndio ambao utawafanya mashabiki wengi wa timu hiyo kuufuatilia kwanza ni kutokana na kutarajiwa kuonyeshwa mubashara na Azam TV, lakini ni mchezo unaotumika kutestia mitambo mipya iliyotua klabu hiyo kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano ikiwamo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho (FA) na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ilitua Afrika Kusini sambamba na Wajerumani hao wanaonolewa na kocha Jess Thorup ziote zikifikia Johanesburg, kisha zote mbili mbili zilianza safari ya kwenda Mpumalanga kwa maandalizi ya mwisho wa mechi hizo maalumu zinazopenda sambamba na burudani ya muziki itakayoanza mapema kabla ya mchezo.

Burudani itakayosindikiza pambano hilo la aina yake litahusisha wakali kama Mthandazo, DJ Bongz, Ndumiso, Zaba na Wonder V

Mbali na mechi hizo timu zote zitapata nafasi ya kutembelea Mbuga ya Kitaifa ya Kruger inayoongoza kwa ukubwa duniani ikiwa na hekta 2.2 milioni ambapo mashindanio hayo ni ya kwanza kufanyika jijini hapo.

“Itakuwa uzoefu wa thamani na wenye manufaa kwa timu nzima,” alisema Mkurugenzi mkuu wa Augsburg Michael Stroll. “Tungependa pia kuchangia kuwakilisha Bundesliga nje ya nchi na kuinua hadhi yake ya kimataifa kwa kukaa kwetu Afrika Kusini.”

FC Augsburg itajipima ubavu dhidi ya Yanga bila ya kuwa na nyota wao ghali zaidi mwenye thamani ya Sh. 26.2 bilioni, Rubén Vargas aliyefanya vizuri katika michuano ya mataifa ya Ulaya ‘Euro 2024’ iliyofanyika Ujerumani akiwa na timu ya taifa la Uswisi kwa sasa fundi huyo anamalizika likizo yake.

Wachezaji hatari ambao Yanga itakabiliwa nao ni pamoja na kiungo, Arne Engels na mshambuliaji, Phillip Tietz ambaye msimu uliopita kwenye ligi ya Ujerumani alifunga mabao manane, alishika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa klabu hiyo nyuma ya Ermedin Demirovic aliyetimkia VfB Stuttgart baada ya msimu kumalizika.

Wachezaji hao nao wanathamani sawa na Vargas. Kocha wa FC Augsburg,Jess Thorup katika msafara wake ameambatana pia na wachezaji wa timu za vijana na wale ambao walikuwa kwa mkopo msimu uliopita ili kuwapa nafasi ya kumshawishi wakati wa maandalizi hayo.

Yanga nao itawaonyesha mastaa wake wapya kwa mara ya kwanza wakiwa uwanjani wakiwemo kipa Abubakar Khomeiny, kiungo Clatous Chama, beki Chadrack Boka na mshambuliaji Prince Dube ambao wameongozana na timu hiyo wakataojumuika na mashine nyingine mpya zilizokuwapo msimu uliopita.

Hata hivyo, mashabiki wa Yanga hawatamuona staa mmoja tu, kiungo mshambuliaji, Pacome Zouzoua aliyerejea kwao kwa ruhusa maalum ya kutengeneza pasi yake ya kusafiria inayokaribia kujaa.

Mashabiki wanataka kuiona Yanga mpya itakavyocheza katika pambano hilo dhidi wa Wajerumani, huku kiu kubwa ni kumuona Chama na Dube ambao usajili wao ulitikisa dirisha hili, ikielezwa pia kocha Miguel Gamondi kwa sasa anakuna kichwa kupata kikosi cha kwanza kwa mastaa alionao, japo alishakaririwa akisema hana presha kiviiile kwani anajua namna ya kuwatumia kila mmoja kwa nafsi na umuhimu wake.

SOMA NA HII  MOHAMMED HUSSEIN "TSHABALALA"...NALIAMINIA JESHI LANGU...MECHI NA UGANDA TUTASHINDA