Home Habari za Yanga Leo GAMONDI…HATURIDHIKI NA MATOKEO MADOGO…

GAMONDI…HATURIDHIKI NA MATOKEO MADOGO…

habari za yanga-gamondi

Yanga ilipata ushindi MNONO wa mabao 0-4 kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambao Vital’O iliutumia kama wa nyumbani, ikishuhudiwa Prince Dube, Clatous Chama, Clement Mzize na Stephane Aziz KI kila moja akifunga bao.

Lakini Kocha wa YANGA Miguel Gamondi licha ya kuwapongeza wachezaji, lakini amewageukia na kuwaambia; “Kama tuna uwezo wa kushinda zaidi tushinde, tunatakiwa kutumia nafasi zaidi sio kama tulichofanya leo.”

Akizungumzia zaidi kauli hiyo, Gamondi alisema licha ya timu kushinda 4-0 lakini bado wangeweza kupata ushindi mkubwa zaidi endapo wangetulia na kutumia nafasi walizotengeneza katika mechi hiyo ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Gamondi alisema hataki kuwa kocha wa kuridhika na matokeo madogo kwa kuwa hilo linaweza kushusha viwango vya wachezaji anaoamini wanaweza kufanya vizuri zaidi.

“Hizi ni mechi ambazo wakati mwingine zinaweza kuamuliwa kwa kuangalia ulifungwa ngapi na wewe ulifunga mangapi, kama tunaweza kutengeneza nafasi basi tunatakiwa kuzitumia kwa wingi,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Tunawaheshimu wapinzani wetu (Vital’O), lakini tulikuwa na uwezo wa kushinda kwa idadi kubwa zaidi ya hiki tulichofanya jana (juzi), mimi sio kocha ninayependa kuridhika na matokeo madogo, tukifanya kosa kama hili linaweza kutupunguzia ubora wa wachezaji.”

Kocha huyo ameongeza kuwa bado Yanga haijafuzu raundi ya pili hadi itakapoitoa Vital’O, akisisitiza baada ya mapumziko ya siku moja watarudi mazoezini kujipanga kwa mechi ya marudiano alioutabiri kuwa mgumu.

“Bado hatujafuzu, hizi ni dakika 90 za kwanza nani anajua kipi kitatokea katika mchezo wa marudiano, tutapumzika kwa siku moja au mbili baada ya hapo tutarudi kujipanga kwa mechi hiyo,” alisisitiza Gamondi.

Yanga itarudiana na Vital’O Jumamosi ijayo, huku ikihitaji ushindi au sare tu ili kusonga hatua inayofuata ambapo itakutana na mshindi kati ya SC Villa ya Uganda iliyochapwa nyumbani juzi kwa mabao 2-1 na Commercial Bank ya Ethiopia.

SOMA NA HII  SIMBA YAHAMIA KWA MOUSSA CAMARA...MRITHI WA LAKRED