Home Habari za michezo FAINALI YA KISASI LEO…YANGA VS AZAM FC

FAINALI YA KISASI LEO…YANGA VS AZAM FC

Habari za Yanga Leo

Leo kuna uhondo mwingine katika mechi hiyo ya kisasi kwa timu hizo mbili zilizomaliza nafasi mbili za juu za Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Yanga na Azam FC zilizofunga kalenda ya mashindano kwa msimu uliopita kwa pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho lililopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja.

Sahau matokeo ya mechi hiyo iliyopita ambapo Azam ilipasuka kwa penalti 6-5 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu, leo kuna mechi ya kisasi.

Hapa chini ni baadhi ya dondoo kuonyesha hii ni mechi ya kisasi na mwenye kuzichanga karata vyema ndiye atakayebeba Ngao ya Jamii kwa msimu huu ambao haina mtu kwa sasa baada ya watetezi Simba kupoteza mechi ya nusu fainali na leo itacheza mechi ya kusaka mshindi wa tatu dhidi ya Coastal Union.

Mechi ya Yanga na Azam itapigwa kuanzia saa 1:00 usiku wakati Simba na Coastal Union zitavaana kuanzia saa 9:00 alasiri kusaka mshindi wa tatu wa michuano hiyo. Endelea nayo…!

MIAKA 8 IMEPITA

Kama hujui pambano la leo ni la tano kwa timu hizo kukutana katika michuano ya Ngao ya Jamii tangu iliposisiwa mwaka 2001.

Katika mechi nne za awali ilizokutana, Yanga imeshinda mara tatu na Azam ilishinda mara moja kwa mikwaju ya penalti miaka minane iliyopita.

Rekodi zinaonyesha kwamba timu hizo zilikutana kwa mara nne mfululizo katika mechi za Ngao, ya kwanza ikiwa ni Agosti 13, 2013 na Yanga kushinda bao 1-0  mechi iliyopigwa Kwa Mkapa (enzi hizo Uwanja wa Taifa).

Mara ya pili ilikuwa Septemba 2014, kwenye uwanja huo huo na Yanga ikashinda mabao 3-0 yaliyowekwa kimiani na Gerson Jaja kutoka Brazili aliyefunga mawili na jingine liliwekwa na Simon Msuva na msimu uliofuata wakavaana kwa mara nyingine Agosti 23, 2025 na Yanga kushinda kwa penalti 8-7 baada ya muda wa kawaida kumalizika kwa suluhu.

AZAM YAJIBU MAPIGO

Katika mechi ya nne kwa timu hizo kukutana katika Ngao ya Jamii ilikuwa Agosti 17, 2016 na dakika za kawaida ziliisha kwa sare ya mabao 2-2. Yanga ilitangulia kupata mabao ya mapema kupitia kwa Donald Ngoma aliyefunga dakika ya 20 na Amissi Tambwe aliyetupia dakika nne baadaye.

Yanga ikiamini inaenda kuizamisha Azam kwa mara ya nne mfululizo, Shomari Kapombe alifunga bao dakika 75 na katika dakika za majeruhi, nahodha John Bocco alikwamisha bao la kusawazisha timu kwenda kwenye dakika za nyongeza ambazo hata hivyo hazikuzaa bao lolote na mwishowe kupigiana penalti.

Katika hatua hiyo ya penalti Azam ilifanya kweli kwa kufunga penalti 4-1 na kulipa kisasi kwa Yanga kwa kuitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza na pekee la michuano hiyo.

KISASI KITALIPWA

Mechi ya leo ni ya kisasi kwa timu zote, Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam kwa mabao 2-1, huku nyota kadhaa wa timu hiyo kushindwa kumaliza mchezo kwa kuchezewa madhambi na wenzao wa Wanalambalamba.

Kuumia kwa wachezaji kama Yao Kouassi na Pacome Zouzoua kunaelezwa ndiko kulikoinyima Yanga nafasi ya kuivaa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa imara zaidi, licha ya kutoka suluhu nje ndani na mwisho kutolewa kwa ‘matuta’.

Ni wazi, Yanga itataka kuendeleza ubabe kwa Wanalambalamba katika mechi ya leo kulipa kisasi hicho, lakini kile cha kupoteza kwa penalti pale zilipokutana mara ya mwisho katika michuano hiyo  ya Ngao.

Kwa Azam itashuka ikiwa na hasira ya kupoteza mechi iliyopita ya Kombe la Shirikisho ikiwa visiwani Zanzibar. Pambano hilo lililopita lilikuwa la tatu kwa Azam katika Kombe la Shirikuisho kupoteza mbele ya Yanga, kwani ilishafungwa msimu wa 2015-16 kwa mabao 3-1, kisha ikalala 1-0 msimu wa 2022-2023 na ndipo msimu uliopita ikakaza dakika za kawaida kwa suluhu lakini ikapasuka kwa penalti 6-5.

SOMA NA HII  MAMADOU DOUMBIA NA YANGA .....MAMBO BADO MAGUMU...ISHU YAKE IMEKAA HIVI...