Home Habari za Yanga Leo YANGA KUSAJILI WAWILI…KISA ROBO FAINALI CAF

YANGA KUSAJILI WAWILI…KISA ROBO FAINALI CAF

Habari za Yanga leo

Rais wa klabu ya Yanga Injinia Hersi Said, amesema wanatarajia kusajili nyota wapya wawili katika dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa baadaye mwaka huu.

Hersi alisema hayo jijini jana na kuongeza kuwa nyota hao watakaosajiliwa watakuwa ni wachezaji wa kigeni.

Alisema licha ya kikosi cha Yanga kuonekana ni ’tishio’, lakini viongozi wanaona hakijakamilika katika kiwango wanachohitaji kifike.

“Kikosi hiki hakijakamilika, bado, nataka niwaambie tu, Yanga hii bado, tena kuna mchezaji tulitakiwa tumlete kwenye hili dirisha kubwa lakini dili halikukamilika.

“Na baada ya hapa, Januari kutakuwa na ongezeko la wachezaji wengine wawili wa kigeni. Kwa hiyo haijakamilika, ikikamilika ndiyo wanahabari tuulizeni kuhusu ubingwa wa Afrika, lakini kwa sasa bado,” alisema Hersi.

Aliongeza lengo ya Yanga kwa sasa ni kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na si vinginevyo.

“Sisi malengo yetu ni kufika robo fainali, tunataka tuingie makundi tuzoee kwanza makundi, halafu twende robo fainali, ila wakati mwingine Mungu huwa ana zawadi, akitupa nusu fainali, fainali au tukichukua ubingwa, sawa tunashukuru, lakini lengo ‘mama’ ni robo fainali,” Hersi alisema.

Wakati huo huo, mchezo wa marudiano kati ya Yanga na Vita’O sasa utachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam badala ya Azam Complex, imeelezwa.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo, imesema mchezo utachezwa Jumamosi kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania kama ilivyopangwa awali.

Yanga itashuka dimbani ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 4-0, walioupata kwenye mechi iliyopita.

SOMA NA HII  GAMONDI AAPA KUWAMALIZA CBE NYUMABNI KWAO