Home Habari za Yanga Leo KITAKACHOIPELEKA YANGA MAKUNDI CAF NI HIKI HAPA

KITAKACHOIPELEKA YANGA MAKUNDI CAF NI HIKI HAPA

HABARI ZA YANGA

Wakati Simba wakifanikiwa kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF mara tano katika misimu sita iliyopita, wenzao Yanga ndani ya muda huo wametinga makundi mara mbili pekee.

Yanga katika mara mbili walizowahi kucheza makundi, zote wamekuvuka hapo na angalau kucheza robo fainali kama ilivyotokea msimu uliopita Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mafanikio yao makubwa zaidi katika kipindi hicho ni msimu wa 2022-2023, walicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuteleza Ligi ya Mabingwa na mechi za mtoano walipigwa na Al Hilal ya Sudan jumla ya mabao 2-1. Walivyoangukia Shirikisho hawakushikika hadi fainali.

Katika msimu wa 2018-19, Yanga haikushiriki kimataifa lakini 2019-20 ilicheza Ligi ya Mabingwa Afrika ikaishia hatua ya pili baada ya kuondolewa na Zesco ya Zambia kwa jumla ya mabao 3-2. Mechi ya kwanza nyumbani matokeo 1-1, ugenini Zesco ikashinda 2-1.

Kabla ya hapo, hatua ya awali Yanga iliwatoa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1. Nyumbani ilikuwa 1-1, ugenini Yanga ikashinda 1-0.

Msimu wa 2021-22, Yanga iliishia hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 2-0 na Rivers United ya Nigeria baada ya kichapo cha bao 1-0 nyumbani na ugenini.

Katika msimu ambao ulikuwa wa kihistoria zaidi kwa Yanga ni 2022-23 na licha ya kutofanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa, walipoangukia Shirikisho walifika hadi fainali.

Yanga msimu huo ilianzia Ligi ya Mabingwa kwa kuifunga Zalan ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 9-0, kisha hatua ya kwanza ikafungwa na Al Ahilal ya Sudan jumla ya mabao 2-1. Nyumbani Yanga ililazimishwa sare ya 1-1, ilipoenda ugenini ikafungwa 1-0.

Kwa bahati, zamani mfumo uliowekwa na CAF ni kwamba timu zikiondolewa hatua ya pili katika Ligi ya Mabingwa, zinakwenda kucheza mtoano Shirikisho kupambania nafasi ya kuingia makundi katika michuano hiyo ya pili ngazi ya klabu barani Afrika.

Mtoano Yanga ilipangwa dhidi ya Waarabu Club Africain kutoka Tunisia, hapa nyumbani matokeo yalikuwa 0-0, ugenini ndipo Yanga wakaenda kufanya maajabu kwa kushinda bao 1-0 lililofungwa na Stephane Aziz Ki dakika ya 79. Wakafuzu makundi ambapo walikwenda kucheza hadi fainali ya michuano hiyo.

Yanga walikaribia kulibeba kombe hilo, lakini sheria ya bao la ugenini ikawahukumu kwani matokeo ya jumla yalikuwa 2-2 dhidi ya USM Alger ya Algeria. Nyumbani walifungwa 2-1, ugenini wakashinda 1-0.

Msimu uliopita 2023-24, wakarejea tena Ligi ya Mabingwa wakianzia hatua ya awali wakiiondosha Djibouti Telecom kwa jumla ya mabao 7-1. Hatua ya pili wakaichapa Al Merrikh ya Sudan jumla ya mabao 3-0.

Ugenini walishinda 2-0 na nyumbani 1-0. Wakafuzu makundi na safari yao ikaishia robo fainali walipoondolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa penalti 3-1 baada ya kushindwa kufungana mechi zote mbili nyumbani na ugenini.

Ukiachana na rekodi hizo, kitendo cha Yanga kucheza nyumbani mechi ya maamuzi dhidi ya timu kutoka Ethiopia nacho kinawapa matumaini makubwa. Rekodi zinaonyesha kwamba, Yanga imecheza mara nne nyumbani dhidi ya Wahabeshi na haijapoteza hata moja. Imeshinda tatu na sare moja.

Katika mechi hizo, imezifunga St. George (5-0), Coffee (6-1), Welaita Dicha (2-0) na sare ya 4-4 dhidi ya Dedebit.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi dhidi ya CBE, amesema wamefanyia marekebisho makosa yaliyotokea ugenini waliposhinda bao 1-0 huku wakikosa nafasi zaidi ya saba za wazi kufunga mabao.

“Sote hatukufurahia kile kilichotokea Ethiopia, ilitakiwa kushinda kwa kiwango kikubwa lakini mambo haya yanatokea kwenye soka, ninachofurahia kila mchezaji anajutia lile.

“Tumefanya mazoezi ya kutosha ya kufunga mabao, naweza kusema kila kilichofanywa na washambuliaji na wachezaji wa nafasi nyingine kimenivutia sana naamini tutakwenda kuwa na dakika 90 nzuri nyumbani mbele ya mashabiki wetu,” alisema Gamondi.

SOMA NA HII  BAADA YA KUONA YANGA WANAZIDI KUSHINDA...AHMED ALLY ASHINDWA KUJIZUIA...AWATOLEA POVU HILI...