Home Habari za Yanga KIUNDANI:-MFAHAMU KOCHA MPYA YANGA .., MBINU, STAILI NA KAULI YAKE KWA SIMBA…..

KIUNDANI:-MFAHAMU KOCHA MPYA YANGA .., MBINU, STAILI NA KAULI YAKE KWA SIMBA…..

Habari za Yanga leo

BAADA ya sintofahamu katika kambi ya Yanga, wamechukua hatua kwa kumtangaza Sead Ramovic, kocha wa zamani wa TS Galaxy ya Afrika Kusini, kuwa nahodha mpya wa benchi la ufundi.

Ujio wake ni juzi baada ya klabu hiyo kuachana na Miguel Gamondi.

Ramovic, mwenye umri wa miaka 45, anaingia Yanga akiwa na sifa za kipekee na historia ndefu katika soka, si tu kama kocha, bali pia kama mchezaji wa kiwango cha juu aliyewahi kucheza katika klabu kubwa barani Ulaya.

Amezaliwa Stuttgart, Ujerumani, Ramovic alianza kucheza soka katika klabu ya FC Feuerbach kabla ya kuendelea na safari yake kwa kuzichezea Stuttgarter Kickers, VfL Wolfsburg, Borussia Monchengladbach, na Kickers Offenbach nchini Ujerumani. 2006, alihamia Tromsø IL ya Norway kabla ya kucheza Sivasspor ya Uturuki na FK Novi Pazar ya Serbia. Alistaafu mwaka 2014 baada ya muda mfupi akiwa na Stromsgodset ya Norway.

Licha ya kuwa kipa mwenye kipaji, Ramovc hakuwahi kucheza mechi rasmi katika timu ya taifa ya Bosnia na Herzegovina ingawa alijumuishwa kwenye kikosi mara kadhaa.

Baada ya kustaafu alielekeza nguvu zake kwenye ukocha akifanya kazi kubwa TS Galaxy ya Afrika Kusini kuanzia 2021. Katika kipindi cha miaka mitatu aliwapa Galaxy utulivu na ushindani dhidi ya vigogo kama Kaizer Chiefs, Orlando Pirates, na Mamelodi Sundowns.

DHIDI YA VIGOGO

Licha ya kuondoka Afrika Kusini wakati timu yake msimu huu ikiburuza mkia baada ya kupoteza mechi nne na kushinda mbili tu kati ya sita, Ramovic alionyesha uwezo wake wa kupanga mikakati mizuri, akishinda mechi kadhaa muhimu dhidi ya timu kubwa.

CHANGAMOTO ZINAZOMSUBIRI

Ramovic anakabidhiwa timu iliyoshinda mataji matatu ya ligi mfululizo lakini ambayo sasa iko nafasi ya pili, pointi moja nyuma ya watani wao Simba SC.

Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kukumbwa na presha kubwa ya ushindani katika miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Azam FC (1-0) na Tabora United (3-1). Mbali na presha ya kurudisha utawala wao kwenye ligi, Ramovic anakutana na changamoto ya kuhakikisha Yanga wanafanya vizuri katika ma-shindano ya kimataifa, hususan Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga imepangwa kwenye kundi gumu dhidi ya TP Mazembe, Al-Hilal, na MC Alger. Hii inamaanisha mbali na kurejesha hali ya ushindi katika ligi, Ramovic atalazimika kuimarisha safu ya ulinzi na ushambuliaji kwa viwango vya juu zaidi.

MBINU NA FALSAFA

Ramović ni kocha anayejulikana kwa falsafa yake ya soka ya kushambulia huku akizingatia nidhamu ya ulinzi. Hii inajidhihirisha kwenye rekodi yake akiwa na TS Galaxy, ambapo timu yake ilikuwa na safu imara ya ulinzi huku ikitoa changamoto kwa timu zenye mashambulizi makali kama Mamelodi Sundowns.

Katika mahojiano ya awali, Ramović alisisitiza umuhimu wa nidhamu na kujituma kwa wachezaji, akisema: Soka ni zaidi ya vipaji; ni kuhusu juhudi, nidhamu, na ari ya kushinda.

Kwa Yanga, falsafa hii inalingana na matarajio ya klabu ambayo inajivunia wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Clatous Chama, na Clement Mzize, ambao ni nguzo muhimu kwenye kikosi. Ramovic ataangazia zaidi kuhakikisha kwamba kikosi chake kina mwelekeo mzuri wa kucheza mpira wa pamoja huku akitumia ubunifu wa wachezaji wake muhimu kubadilisha matokeo uwanjani.

KAULI YAKE

Baada ya kusaini mkataba na Yanga, Ramovic ni kama aliwatangazia vita watani zao Simba, akisema: “Najua ukubwa wa klabu hii na matarajio yake. Yanga ni moja ya klabu kubwa Afrika, na nina furaha kuwa sehemu ya familia hii.

“Ni jukumu langu kuhakikisha tunarudi kileleni (nafasi mabayo Simba inaishika) mwa ligi na kuwa washindani wakubwa katika michuano ya kimataifa. Wachezaji ninaowaona hapa wana vipaji vikubwa, na naamini kwa pamoja tunaweza kufanikisha ndoto za klabu na mashabiki.”

Kocha huyo aliongeza, “nimeona jinsi wanavyoishi kwa ajili ya timu hii. Nitahakikisha tunacheza soka la ushindani wa hali ya juu ambalo linawapa fahari.”

SOMA NA HII  KISA KUMDHIHAKI MGUNDA...ALLY KAMWE KUKUMBANA NA RUNGU LA TFF...KUFUNGIWA MIEZI 3...