RAIS Dk Samia Suluhu Hassan ametoa Sh bilioni nane kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mazoezi vitavyotumika katika michuano ya CHAN 2025 na AFCON 2027, Tanzania ikiwa mwenyeji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesaini mkataba wa ujenzi na Suma JKT kwa ajili ya ujenzi na ukatarabati wa viwanja vitano ambavyo ni Meja Jenerali Isamuhyo, Gymkhana, Shule ya Sheria ‘Law school’ na ujenzi wa viwanja vipya Leaders, Farasi, Tirdo na Gymkhana.
Amesema ujenzi huo utahusisha uwekaji wa taa, majukwaa yatayochukua watu 2000 katika viwanja vipya, njia za kupitisha maji na kupanda nyasi halisi ili kuendana na viwango vya CAF utakamilika kwa muda wa siku 120 sawa na miezi mitatu kwa ajili ya CHAN na AFCON.
“Kwa sasa tunahitaji kufanya ukarabati na kujenga baadhi ya viwanja kwa ajili ya mazoezi ambavyo vitatumika kipindi cha CHAN 2025 na 2027 kwa ajili ya AFCON ambao tutakuwa wenyeji.
Sambamba na michuano hiyo pia tuko kwenye mpango wa kuomba wenyeji wa michuano ya All African Games kulingana na mipango hiyo tunalazimika kujenga viwanja vitano katika mikoa mitatu, Dar es Salaam, Dodoma na Arusha,” amesema.
Naye mkurugenzi wa uendeshaji wa kampuni ya Suma JKT, Morgan Nyonyi, amesema wapo tayari kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
“Tayari kazi imeanza na leo tumetiliana mkataba na tulianza Uwanja Meja Jenerali Isamuhyo na CAF walipita na kutupa baadhi ya maelekezo, na sasa tunaendelea na mchakato mzima wa uboreshaji na ujenzi wa viwanja vitano vya mazoezi,” amesema .
SOMA NA HII MAYELE AZIDI KUJAZWA NG'OMBE MIKOANI...APEWA MWINGINE MNONO...BUMBULI ATAJA NA MADAFU...