KOCHA wa Simba, Fadlu Davids amesema licha ya ushindi walioupata kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Maquiz, bado safu yake ya ushambuliaji imekuwa na tatizo la kukosa umakini kwenye umaliziaji.
Hata hivyo kocha huyo amesema wachezaji wake wanastahili pongezi kwa namna walivyopambana kwenye mchezo huo na kupata ushindi wa bao 1-0.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo wa juzi, Kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema anaenda kufanyia kazi mapungufu hayo ili mchezo ujao waweze kutumia nafasi wanazozitengeneza.
Alisema baada ya kukosa mabao mengi, wachezaji wake walionekana kucheza kwa wasiwasi ili wasikosee hivyo mechi ikaonekana ngumu.
“Nimefurahi kupata pointi tatu kwenye mchezo wetu wa kwanza, ila tungeongeza umakini kidogo tungetoka uwanjani na ushindi wa zaidi ya mabao mawili hasa kipindi cha kwanza, nawaamini wachezaji wangu wote kuanzia wa kwanza hadi wa 26, kila mmoja anaweza kucheza muda wowote, haya ni mashindano ambayo unatakiwa kuwa na wachezaji mbadala,”alisema Fadlu.
Alisema anaamini mchezo ujao watakuwa bora zaidi na kuwataka mashabiki kuendelea kuwaunga mkono wachezaji wao na kuwapa hamasa zaidi.
Pamoja na kupata ushindi wa bao 1-0, baadhi ya mashabiki na wachambuzi wameonekana kutoridhishwa na uwezo wa wachezaji wengi katika mchezo huo, huku pia wengine wakikosoa mabadiliko makubwa ya kikosi aliyoyafanya kwa kuwaacha baadhi ya nyota wake nje.
Shujaa wa mchezo huo, golikipa Moussa Camara, aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kushangilia ushindi huo akisema haukuja kirahisi kwani wamepambana na kiasi kikubwa kuupata, badala ya kusikiliza watu wakilalamikia kiwango.
“Mechi ilikuwa ngumu, lakini tulikuwa nyumbani na tumeweza kupata ushindi, hiki ni kitu kizuri sana kwetu, kipindi cha kwanza tulikosa nafasi nyingi, kipindi cha pili wapinzani wetu walibadilika na mimi kama golikipa ilikuwa ni jukumu langu kuhakikisha naisaidia timu yangu,” alisema Camara.
Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya CS Constantine ya Algeria, alisema utakuwa mchezo mgumu, lakini watajipanga kwa ajili ya kwenda kusaka ushindi au sare.
“Tunaangalia sasa mchezo ujao, utakuwa mgumu kuliko huu, lakini tunakwenda kucheza kwa ajili ya kushinda mechi au sare, kikubwa ni kwenda kupambana,” alisema Camara.
Simba imesafiri hadi Algeria kucheza mchezo wa raundi ya pili, Kundi A, hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine Desemba 8 mwaka huu, Uwanja wa Mohamed Hamlaoui.