Tukutane kwa Mkapa ndicho mashabiki wa Simba wanaweza kusema kutokana na hesabu zilivyo kwa timu yao baada ya kupoteza jana, Jumapili kwa mabao 2-1 huko Algeria dhidi ya CS Constantine kwenye mechi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika katika hatua ya makundi.
Katika mchezo huo ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui mjini Constantine, Algeria, Simba ilikuwa na nafasi ya kuibuka na ushindi baada ya kuongoza katika dakika 45 za kipindi cha kwanza kufuatia bao na nahodha wao, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Lakini mwisho wa siku walishindwa kushikilia uongozi wao wa 1-0 na walijikuta wakikubali kipigo cha mabao 2-1 ambayo waliruhusu ndani ya dakika tano. Kipigo hiki kilionyesha mapungufu kadhaa ambayo kocha wa Simba, Fadlu Davids anatakiwa kuyafanyia kazi.
MPANGO WA KULINDA
Kocha Fadlu alionyesha wazi kuwa alitaka kuhakikisha kwamba CS Constantine hawapati nafasi ya kupenya katikati ya uwanja. Katika safu ya kiungo, alianzisha wachezaji watatu wenye uwezo mkubwa wa kulindawa, Abdulrazak Hamza ambaye tunafahamu kuwa ni beki wa kati, Augustine Okejepha, na Fabrice Ngoma. Lengo kuu la mpango huu lilikuwa kuzuia kabisa Constantine wasiweze kupenya kupitia katikati ya uwanja.
Uwepo wa wachezaji hao ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, uliwalazimisha wapinzani wao kushambulia kupitia pembeni. Hii ilikuwa ni mbinu ya kulazimisha mchezo wa Constantine uwe wa krosi kutoka pembeni, jambo ambalo linakuwa rahisi kuzuia kwa mabeki wa pembeni wa Simba kama Shomary Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Hata hivyo, ingawa mpango huu ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha kwanza kwa kudhibiti viungo na mashambulizi ya Constantine, ulionekana kushindwa kufanya kazi kwa urahisi katika kipindi cha pili ambapo waliruhusu mabao mawili ndani ya dakika tano.
ILIVYOKUWA SASA
Kwa upande wa Simba, mpango wao wa kushambulia ulionekana kuwa dhaifu na haukuwa na ufanisi mkubwa, kikosi chao kilijaa idadi kubwa ya wachezaji wenye uwezo mzuri zaidi ya kulinda kuliko kushambulia.
Hali hii ilifanya kuwa vigumu kwa Simba kufunga goli kupitia “Open Play”, yaani shambulizi la moja kwa moja bila kuhitaji makosa ya kiufundi kutoka kwa wapinzani.
Kwa hivyo, njia pekee ya Simba kufunga goli ilikuwa kupitia mpira wa faulo au kosa la mchezaji mmoja wa Constantine. Kosa la kiufundi kutoka kwa kipa, Kheireddine Boussouf wa Constantine ndilo lililowezesha bao la Tshabalala.
Ingawa Simba walikuwa na wachezaji wenye uwezo wa kushambulia, walikosa idadi ya wachezaji wa kutosha mbele ya lango la Constantine, jambo ambalo liliwafanya wacheze kwa tahadhari kubwa.
SIMBA ILIPOZIDIWA
CS Constantine, kwa upande wao, walikuwa na mwelekeo wa kutafuta mabao haraka katika kipindi cha pili. Walijua kuwa iwapo wangeendelea kucheza kwa mtindo wa kuchelewesha mashambulizi, Simba wangeweza kuendelea kulinda uongozi wao. Ili kuepuka hali hiyo, Constantine walikazana kutafuta goli la haraka baada ya Simba kufunga, na hii ilikuwa mbinu yao ya kulazimisha kupata matokeo.
Katika dakika ya 46, bao la kusawazisha la CS Constantine ambalo Simba ilijifunga kupitia kwa Hamza lilionyesha jinsi walivyoweza kutumia nguvu zao za kimwili na miondoko ya haraka.
Walilazimisha Simba kufikiria kuhusu kulinda nafasi zao badala ya kushambulia, na baadaye walipata bao la pili kupitia Brahim Dib, ambaye alitumia makosa madogo katika safu ya ulinzi ya Simba.
Baada ya kupata uongozi, Constantine walikuwa na mtindo wa kucheza kwa umakini mkubwa, kuzuia nafasi za Simba, na kutokubali wapinzani wao kupita katikati. Walijua kuwa Simba ingependa kupenya katikati ya safu yao ya ulinzi, lakini walilazimisha mashambulizi yao yawe ya pembeni ambapo walikuwa tayari na idadi ya wachezaji wa kutosha kuzuia kila krosi na kupinga mashambulizi.
HESABU ZILIVYO
Licha ya matokeo hayo, Simba ambayo ipo kundi A, ina nafasi kubwa bado ya kuvuka hatua ya makundi kutokana na mchezo ujao kuwa nyumbani, Desemba 15 dhidi ya CS Sfaxien ambao wanaburuza mkia bila ya pointi.
Msimamo wa kundi hilo kwa sasa unaongozwa na CS Constantine wakiwa na pointi sita kileleni, Simba inafuata katika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu sawa na Bravos do Maquis ambao juzi walipata ushindi wao wa kwanza baada ya kuwafunga CS Sfaxien mabao 3-2.
Fadlu anatakiwa kuchanga vizuri karata zake ili kuhakikisha pointi tatu za mchezo ujao zinasalia kwa Mkapa ili kuweka hai matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya sita katika michuano hiyo ya CAF kwa miaka ya hivi karibuni, wamefanya hivyo mara nne katika ligi ya mabingwa,2018–19, 2020–21, 2022–23 na 2023–24 na moja upande wa Shirikisho 2021–22.
MSIKIE FADLU
Baada ya mchezo, kocha wa Simba, Fadlu Davids, alizungumza kwamba wachezaji wake walikosa “umakini na utekelezaji wa mikakati” waliyojiwekea kabla ya mechi.
“Ni mchezo mgumu na ni vigumu kuficha ukweli kwamba tumepoteza. Tulikuwa na nafasi ya kupata pointi, lakini hatukufanya vizuri katika hatua muhimu. Kama timu, tunahitaji kujifunza kutokana na makosa yetu. Tumeshindwa kudhibiti mashambulizi ya Constantine baada ya goli letu la mapema, na walitumia nafasi hiyo kwa ustadi mkubwa.”
Kocha Davids aliongeza kuwa kuna mambo mengi ya kuboresha, hasa katika upande wa “uwezo wa kutunza mpira na kufanya maamuzi haraka.”
Vikosi vilivyoanza;
CS CONSTANTINE: Boussouf, Meddahi, Baouche, Bellaouel, Boudrama, Merba, Benchaira, Dib, Benchaa, Tahar na Kaibou
SIMBA: Camara, Kapombe, Tshabalala, Chamou, Che Malone, Hamza, Ngoma, Okejepha, Ateba, Ahoua na Kibu.
SOMA NA HII KUELEKEA MECHI NA AZAM....AUCHO APATA 'PANCHA'...AZUA PRESHA...KAZE ASHINDWA KUJIZUIA...