ALIYEKUWA kipa namba moja wa Simba, Ayoub Lakred ameanza kupaki mizigo kujiandaa kuondoka klabu hapo dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa Jumapili hii ili kumpisha winga teleza, Elie Mpanzu.
Simba ilishamalizana na Mpanzu siku chache baada ya dirisha kubwa la usajili kufungwa Agosti 31 na kwa sasa anajiandaa kuanza kuitumikia timu hiyo, akiongeza idadi ya nyota wa kigeni kwa klabu hiyo.
Kanuni ya usajili wa nyota wa kigeni inaelekeza klabu kusajili wachezaji wasiozidi 12, lakini hadi sasa Simba ina idadi zaidi ya hiyo na hivyo, mabosi wa klabu hiyo walikuwa wanakuna vichwa kujua yupi wa kumkata.
Kabla ya Mpanzu kuingia Simba tayari ilikuwa na nyota 12 wa kigeni ambao ni makipa Moussa Camara, Ayoub Lakren, Valentin Nouma, Chamou Karaboue, Fondoh Che Malone, Fabrice Ngoma, Augustine Okejepha, Debora Mavambo, Steven Mukwara, Jean Charles Ahoua, Joshua Mutale na Leonel Ateba.
Kutokana na kanuni, Simba inalazimika kumchomoa mmoja kati ya wachezaji 12 na taarifa kutoka Msimbazi ni kipa Ayoub ndiye aliyefyekwa kwa vile uongozi hauoni mantiki ya kuwa na makipa wawili wa kigeni, wakati Camara anaifanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa.
Awali, viongozi wa Simba walikuwa na mgongano kuhusu uamuzi wa mchezaji gani wa kigeni wataachana naye ili kumpisha Mpanzu, kwani kulikuwa na majina mawili mezani, likiwemo la Ngoma na Ayoub.
Hali hii ilizua mjadala mrefu kati ya viongozi wa Simba na benchi la ufundi kabla ya kuamua kufanya maamuzi magumu wa kula kichwa cha kipa huyo raia wa Morocco.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani kilichozungumza kwa sharti la kutotajwa jina kilisema: “Hivi sasa, Ngoma ni kipenzi cha kocha Fadlu Davids. kocha amebaini kiungo huyo anaendana vyema na mfumo wa uchezaji autakao, tofauti na ilivyokuwa mwanzoni alipopata wakati mgumu klabuni.”
Chanzo hicho kilieleza kiwango cha Ngoma kimebadilika na kumfanya kuwa mchezaji muhimu katika mfumo wa kocha Fadlu.
Kwa upande mwingine, Ayoub amekuwa na wakati mgumu tangu alipopona majeraha yake na kuonekana kuwa na changamoto ya kupenya kikosi cha kwanza mbele ya Moussa Camara.
Tangu kurejea kwa Ayoub kutoka katika majeraha, amecheza mchezo mmoja tu wa kirafiki na hajapata nafasi bado kikosi cha kwanza.
CHANGAMOTO KWA AYOUB
Ayoub alijiunga na Simba 2023 akitokea kwao Morocco. Akiwa ni kipa mwenye uzoefu baada ya kuichezea FAR Rabat, aliteuliwa kama kipa namba moja mbele ya Aishi Manula na alisaidia timu hiyo kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, msimu huu alikuwa na changamoto kubwa baada ya majeraha kumweka kando kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa chanzo cha karibu na mchezaji huyo, Ayoub alilazimika kufanya maamuzi magumu kuhusu hatma yake katika klabu hiyo.
“Ayoub amepitia mambo mengi magumu mbali na majeraha alikuwa na changamoto pia za kifamilia, hivyo anahitaji kurudi kwao.”
Ayoub alikubali kuwa na mazungumzo na viongozi wa Simba na kwa mujibu wa taarifa za ndani, alikubaliana kuondoka kwa heshima.
“Kama mchezaji, unahitaji kuelewa kuwa mabadiliko ni sehemu ya mchezo. Ayoub anahitaji kuangalia mbele,” kiliongeza chanzo hicho.
ELIE MPANZU SASA
Kwa upande mwingine, Elie Mpanzu anatarajiwa kuwa nyota mpya wa Simba katika kipindi kijacho. Winga huyo Mkongomani alijiunga na Simba tangu mwanzo wa msimu, lakini usajili wake ulichelewa. Hata hivyo, Mpanzu amekuwa akiendelea na mazoezi na timu kwa zaidi ya miezi mitatu, na sasa amekaribia kutimiza ndoto yake ya kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Simba.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa viongozi wa klabu ya Simba, Mpanzu anatarajiwa kuwa mchezaji muhimu kwa timu hiyo. “Tumemsubiri kwa muda mrefu, sasa tunafurahi muda sio mrefu tutaanza kumuona akitutumikia,” alisema ofisa habari wa timu hiyo, Ahmed Ally.