KATIKA kuhakikisha wanaboresha timu yao, uongozi wa Pamba jiji FC, umefunga safari kwenda nchini Zambia kwa ajili ya kukamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo wa Simba, Larry Bwalya anayekipiga katika timu ya Napsa Stars.
Imeelezwa kuwa viongozi hao wapo nchini humo ili kukamilisha mazungumzo na klabu ya Napsa Stars ambayo anaichezea kiungo huyo kumsajili kipindi cha dirisha ambalo limefunguliwa Jumapili, Desemba 15.
“Mazungumzo baina ya klabu mbili yameenda vizuri, kazi iliyobakia mazungumzo na mchezaji na viongozi wa Pamba makubaliano yaliyopo ni kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia kikosi chetu,” kimeeleza chanzo chetu.
Ofisa Habari wa Pamba Jiji FC, Mosses William amesema dirisha la usajili limefunguliwa na wapo kwenye mazungumzo na wachezaji mbalimbali ikiwa sehemu ya kuboresha kikosi cha timu hiyo.
“Kuhusu Bwalya (Larry) ni mchezaji mzuri na hakuna timu itakataa huduma ya kiungo huyo, amewahi kucheza Tanzania na anaifahamu ligi yetu, suala la kusajiliwa tusubiri muda ukifika tutaweka wazi majina ya wachezaji ambao tumewasajili kipindi hiki,” amesema.
Mosses amesema wako katika maboresho ya kikosi cha timu hiyo kwa kusajili wachezaji ambao wamependekezwa na benchi la ufundi.