Home Habari za michezo MASHABIKI YANGA KUIPATA ‘SAPRAIZI’ YA ZAWADI HII KWA KRISMASI YA LEO…?

MASHABIKI YANGA KUIPATA ‘SAPRAIZI’ YA ZAWADI HII KWA KRISMASI YA LEO…?

tetesi za usajili Yanga leo

KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema wamekwenda jijini Dodoma kwa lengo moja tu, kuwapa zawadi ya sikukuu ya Krismasi wananchi na mashabiki wa timu hiyo kwa ushindi leo dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Yanga leo itashuka dimbani saa 10:00 jioni kucheza dhidi ya wenyeji wao, kwenye Uwanja wa Jamhuri katika kampeni yake ya kutaka kutetea taji lake la ubingwa, ikitaka kulichukua kwa mara ya nne mfululizo.

Mjerumani huyo amesema ushindi wowote watakaoupata utakuwa ni muhimu kwao kwani utawapa pointi tatu na kuzidi kuelekea juu ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tumekuja hapa kwa lengo moja, tuchukue pointi tatu na kuwapa zawadi ya Krismasi mashabiki wetu, hili ndiyo jambo muhimu kwetu,” alisema kocha huyo.

Hata hivyo, alisema huenda akakibadilisha kidogo kikosi chake kutokana na kuhofia uchovu wa wachezaji wake ambao wametumika kwenye michezo miwili mfululizo waliyocheza.

“Itakuwa mechi ngumu kwa sababu tumecheza michezo miwili mfululizo ndani ya muda mfupi, kwa hiyo tunahitaji pia kufanya mabadiliko ya kikosi,” alisema.

Alhamisi iliyopita Yanga ilicheza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa FC na kushinda mabao 3-2, Jumapili iliyopita ikaingia tena dimbani kupepetana na Prisons, ikishinda mabao 4-0, mechi zote zikipigwa, Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.

“Nimefika hapa kama wiki tatu zilizopita, nimekutana na michezo mfululizo bado sijapata muda wa kukaa na vijana wangu kuwapa mazoezi ya kutosha, kuwaelekeza kwa utulivu kile ninachokihitaji, pia kuwafanya wachezaji wote wawe na utimamu wa mwili, nadhani baada ya wiki nne au tano hali itabadilika kabisa,” alisema kocha huyo aliyetwaa nafasi ya Miguel Gamondi.

Mchezo wa leo utakuwa wa 14 kwa Yanga ambayo ina pointi 33, ikiwa imeshinda michezo 11, ikipoteza miwili, mabao 23 ya kufunga na imeruhusu mabao sita na haijatoka sare yoyote mpaka sasa.

Ipo kwenye nafasi ya pili ya msimamo ikiwa kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Azam FC ambayo nayo ina pointi 33 ikiwa nafasi ya tatu.

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime, alisema itakuwa ni mechi ya tano kucheza na timu za Dar es Salaam, huku akisema itakuwa mechi ngumu akiwataka wachezaji wake kupunguza makosa kwani timu kubwa ikiwamo Yanga kuwa na tabia ya kutumia makosa yanayofanywa na timu ndogo na kuwaadhibu.

“Dar kuna timu tano, tumeshacheza nazo timu nne, mbili tumezifunga, mbili zimetufunga tunacheza na Yanga ambayo ni timu ya tano.

Ukicheza na Yanga siyo mchezo rahisi, inabidi kwanza mwalimu uwe makini, wachezaji wako wawe makini pia. Hizi timu Simba, Yanga, Azam zote zinafungika, lakini zinafungikaje? Kwenye makaratasi mechi hizi unaweza kuziona ni rahisi, lakini wachezaji wako makini kweli? Wanatakiwa kupunguza makosa na hapo ndipo ubora wa wachezaji wa hizi timu unapotofautiana.

Anaweza kukosea mchezaji wa Yanga sisi Dodoma Jiji tusimwadhibu, lakini wa Dodoma akifanya Yanga wanaadhibu, pale ndipo ubora na viwango vya wachezaji vinapozidiana,” alisema kocha huyo.

Maxime alisema kama wachezaji wake watafuata maelekezo yake, wanaweza kuwa na jioni nzuri leo kwenye uwanja wao wa nyumbani.

“Nimekaa na kuiangalia Yanga, nimekaa na vijana wangu kuwaelekeza, nafikiri itakuwa mechi nzuri,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUIFUNGA SIMBA KWA MKAPA...RAJA CASABLANCA WALIA KUFANYIWA HUJUMA...ISHU IKO HIVI..