Home Habari za michezo YANGA BILA GAMONDI…HIZI HAPA SIKU 40 ZA RAMOVIC YANGA….MAAJABU YAKE NI HAYA…

YANGA BILA GAMONDI…HIZI HAPA SIKU 40 ZA RAMOVIC YANGA….MAAJABU YAKE NI HAYA…

Habari za Yanga leo

Sead Ramovic alitambulishwa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga ikiwa ni muda mchache baada ya klabu hiyo kutangaza kuachana na Miguel Gamondi.

Ramovic ambaye ametua Yanga akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini, leo Desemba 25, 2024 ametimiza siku 40 tangu utambulisho wake huo ufanyike huku akifanikiwa kuiongoza timu hiyo kucheza mechi sita za kimashindano.

Katika mechi hizo sita, unaweza kusema Ramovic alianzia pale ambapo mtangulizi wake, Gamondi alipoishia.

Ukiangalia Gamondi aliondoka Yanga ikiwa ni baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za ligi dhidi ya Azam kwa kufungwa bao 1-0, kisha kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Tabora United.

Kabla ya Gamondi hajaondoka, aliiongoza timu hiyo kucheza mechi nne za hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kushinda zote kwa kufunga mabao 17 huku nyavu zake zikiwa hazijaguswa.

Kwenye ligi, alicheza mechi 10, akishinda nane na kupoteza mbili timu ikifunga mabao 16 na kuruhusu manne.

Upande wa Ngao ya Jamii, mechi mbili alishinda zote na kubeba ubingwa akifunga mabao matano na kuruhusu moja akizifunga Simba (1-0) na Azam (4-1).

Katika siku za mwisho za Gamondi, Yanga ilionekana kucheza chini ya kiwango huku mabao yakipungua kulinganisha na awali.

NINI AMEBADILISHA RAMOVIC?

Ukilinganisha kipindi cha Gamondi na Ramovic ndani ya ligi, utaona namna ambavyo Yanga imekuwa na mabadiliko makubwa sana ya kiuchezaji licha ya kwamba hapo awali ilionekana ni kama haichezi kitimu.

Ramovic alianza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo ugenini, kisha akashinda 3-2 nyumbani dhidi ya Mashujaa na akaichapa Tanzania Prisons 4-0.

Ukilinganisha na Gamondi, mechi tatu za kwanza msimu huu kwenye ligi naye alishinda zote, lakini mabao yalikuwa machache akifunga manne huku nyavu zake zikiwa hazijatikiswa wakati tayari Ramovic kikosi chake kimeruhusu mabao mawili.

Mbali na hilo, wakati wa Gamondi, ilionekana wachezaji baadhi ndiyo wenye uhakika wa kucheza huku wengine wakitupwa nje kabisa.

Wachezaji kama Farid Mussa, Kibwana Shomari na Aboutwalib Mshery hawakuwa wakipewa nafasi lakini sasa tumewaona wakicheza.

Ramovic anachokifanya ni kutoa nafasi kwa kila mmoja ambaye yupo fiti kuonyesha uwezo wake jambo ambalo kama ukishindwa ni juu yako, yeye hana lawama.

Katika mechi tatu za ligi, alianza kwa kumpa nafasi Khomeiny Abubakar dhidi ya Namungo ambaye ulikuwa ni mchezo wa pili kucheza msimu huu baada ya kuikabili Coastal Union. Lakini pia Khomeiny akadaka tena dhidi ya Mashujaa.

Katika mchezo huo wa Mashujaa, pia ilikuwa ni mara ya kwanza kumshuhudia Kibwana Shomari akicheza msimu huu mechi yake ya kwanza tena alianza kikosini akitumika kwa dakika 79 kabla ya juzi dhidi ya Tanzania Prisons kumaliza dakika zote tisini.

Farid Mussa naye alirejea uwanjani kwa mara ya kwanza dhidi ya Mashujaa akitoka kuuguza majeraha kwa muda mrefu akiingia dakika ya 79 huku juzi dhidi ya Tanzania Prisons akianza kikosi cha kwanza na kucheza kwa dakika 65. Katika mchezo huo, pia Mshery alidaka kwa mara ya kwanza msimu huu.

“Kuaminiwa kwa kucheza dakika nyingi mchezo wa kwanza baada ya kukaa nje kwa muda mrefu sio rahisi, nashukuru Mungu nimepokelewa na kuaminiwa, naomba hili liendelee ili kunijengea kujiamini zaidi na kuipambania timu ili iweze kufikia malengo ya kutetea taji.

“Mechi zote mbili nilizocheza nashukuru Mungu zimekuwa na baraka kwangu kwa sababu timu imepata matokeo na najiona nikianza kurudi kwenye mstari na nacheza kwa kujiamini, nafikiri kama nitaendelea kupata nafasi hii mara kwa mara nitajiweka kwenye ushindani,” alisema Kibwana ambaye katika mechi hizo mbili alitoa asisti moja.

Beki huyo aliyetua Yanga msimu wa 2020-2021 akitokea Mtibwa Sugar, kabla ya kupitia wakati mgumu kipindi cha Gamondi, alitumika zaidi wakati timu hiyo ikinolewa na Nasreddine Nabi akitumika beki zote mbili kushoto na kulia.

Hayo yakijiri, katika uchezaji wa Yanga hivi sasa umemfanya hadi mshambuliaji wa timu hiyo Prince Dube kuanza kufunga kwenye ligi.

Dube aliyetua Yanga msimu huu akitokea Azam, takwimu zinaonyesha amehusika kwenye mabao mengi zaidi akicheza mechi chache chini ta Ramovic baada ya kupita kipindi kirefu bila ya kufunga.

Kitendo cha Dube kufunga mabao manne kwenye ligi katika mechi mbili zilizopita ikiwemo hat trick, imewafanya mashabiki wa timu hiyo kuanza kuona straika wao hivi sasa amejipata. Si kufunga tu, hata kutoa asisti yupo vizuri.

Tangu awe chini ya Ramovic, Dube ameonekana kufanya vizuri zaidi tofauti na wakati wa Miguel Gamondi.

Takwimu za kwenye ligi zinaonyesha Dube chini ya Gamondi alicheza mechi tisa bila ya kufunga bao zaidi ya kutoa asisti moja katika mchezo wa mwisho ambao Gamondi aliisimamia timu hiyo.

Ukiweka kando ligi kuu, Ngao ya Jamii alifunga bao moja na asisti moja akiisaidia timu yake kubeba ubingwa.

Kimataifa wakati wa Gamondi, Dube alifunga mabao matatu yote hatua ya awali na asisti mbili, hivyo kumfanya kuwa na jumla ya mabao manne na asisti nne chini ya Gamondi kwenye mechi 15 za mashindano tofauti.

Katika mechi sita za Ramovic michuano tofauti, Dube amehusika kwenye mabao sita akiwa na wastani wa bao kila mechi kutokana na kufunga matano na asisti moja huku akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu kupiga hat trick.

Takwimu za jumla zinaonyesha Dube amecheza mechi 21 kati ya 22 za michuano tofauti tangu atue Yanga msimu huu akitokea Azam akifanikiwa kufunga mabao manane na asisti tano. Katika mabao hayo manane, matano kipindi cha Ramovic na matatu wakati wa Gamondi.

Kimataifa amecheza mechi zote saba tangu hatua ya awali kwa dakika 306. Upande wa ligi, dakika zake ni 626 akicheza mechi 12 kati ya 13, amekosa moja pekee dhidi ya JKT Tanzania.

Kuhusu anachokifanya Dube hivi sasa, Ramovic alisema: “Dube ni mshambuliaji mzuri ndio maana tupo naye hapa, tangu nimefika alikuwa hajafunga bao kwenye ligi, ilikuwa inaumiza kumuona kwa kuwa anapambana sana mazoezini na hata uwanjani.

“Kuna nyakati tulilazimika kukaa naye na kumjenga kisaikolojia tukimsihi asikate tamaa kwani kwenye soka kwa washambuliaji ukame kama huu wa mabao unatokea lakini haitakiwi kukata tamaa. Tulipambana kuiweka sawa saikolojia yake na sasa anaendelea sawa.”

Aidha Ramovic alisema anavutiwa na ushirikiano wa wachezaji wote wanaocheza kwenye kikosi chake hatua ambayo itaendelea kuzalisha mabao mengi zaidi endapo watatulia na kutumia nafasi wanazotengeneza.

“Tunatakiwa kuendelea kucheza kama timu kama hivi, unaona namna wachezaji wanavyoshirikiana, unaweza kuona Dube anamtengenezea nafasi mwenzake na Clement (Mzize) anamtengenezea nafasi mwenzake, kitu muhimu hapa ni kuiweka timu mbele.

“Tunaweza kufunga mabao mengi zaidi kama hali ya namna hii ikiendelea hivi, tunatakiwa kuendelea kutumia nafasi kwa wingi kwenye kila mchezo,” alisema Ramovic.

Credit:- MwanaSpoti leo.

SOMA NA HII  HALMASHAURI KUJENGA VIWANJA VYAO...SIMBA NA YANGA VICHEKO TU