STRAIKA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Clement Mzize, amesema yeye ndiye alikuwa mshauri nasaha ‘mkubwa’ wa mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Dube,wakati alipokuwa akipitia kipindi kigumu cha ukame wa mabao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mzize, alisema ana urafiki wa karibu na Dube, hivyo ni mmoja wa watu ambao wamefurahi kuona mshambuliaji huyo anaanza kufunga mabao, kwa sababu alikuwa akikaa naye na kumpa ushauri wa nini cha kufanya.
Mzize anasema akiwa anapitia changamoto hiyo ya kushindwa kufunga mabao, Dube alikuwa kwenye hali ya kukata tamaa.
“Dube ni rafiki yangu mkubwa, ndiyo maana unaona siku ile dhidi ya Dodoma Jiji, alikuja kunipongeza kwa kunimwagia maji mechi ilipomalizika kwa sababu nilifunga mabao mawili, wote sisi ni mastraika, hata wakati alipokuwa anapitia wakati mgumu mimi nilikua mshauri wake, nilikuwa namwambia asikate tamaa kwa sababu vitu hivi vinatokea na mimi vimeshanitokea sana.
Unachotakiwa usikate tamaa, mechi yoyote utakayopewa wewe kuwa makini tu, naamini mabao yatakuja tu, ukiwa unawaza sana ndiyo unavyozidi kujipoteza,” alisema Mzize.
Aliongeza Mzimbabwe huyo alimsikiliza na kufuata kile alichomwelekeza na anafurahi kuona ‘kimezaa matunda’ kwa sasa kufunga mabao na kufikisha magoli matano kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea.
“Leo hii unaona kila kitu sasa kimebaki historia na kila anachofanya kinakubali, amekuwa mwenye furaha sana,” alisema Mzize.
Dube, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Azam FC, alikuwa katika wakati mgumu, akiwa anakosa mabao mengi ya wazi katika michezo mbalimbali kiasi cha kuzua mijadala kutoka kwa mashabiki na wachambuzi wa soka.
Bao alilofunga nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo dhidi ya TP Mazembe katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuifanya Yanga kutoka sare ya bao 1-1 ugenini, Desemba 14, mwaka huu lilikuwa kama limemfungulia milango kwa sababu baada ya hapo amekuwa akifunga mabao mfululizo.
Desemba 19,mwaka huu, alifunga hat-trick na kuiwezesha Yanga kuondoka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mashujaa FC, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, akifunga bao moja katika kila mchezo, dhidi ya Prisons na Dodoma Jiji, Jumatano iliyopita, wakishinda mabao 4-0 kila mechi.
Kutokana na kufunga mabao katika mechi tatu mfululizo ya za ligi na kufikisha mabao matano, ameingia katika nafasi ya nne ya wafungaji wa Ligi Kuu, akiwa sawa na Edgar William wa Fountain Gate, Leonel Ateba wa Simba, Peter Lwasa wa Kagera Sugar.
Kwa sasa ndiye kinara wa mabao kwenye kikosi cha Yanga, akifuatiwa na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Clement Mzize ambao wote wana mabao manne kila mmoja.
Mzize alisema mabao mawili aliyofunga kwenye mchezo uliopita dhidi ya Dodoma Jiji, yamemfanya awe na hamu ya kufunga mengi zaidi ili awe kinara si wa ufungaji ndani ya Yanga, ila Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Nafanya sana mazoezi na kufuata maelekezo ya mwalimu, naamini hilo litawezekana kama nitakapa nafasi ya kucheza,” alisema nyota huyo ambaye anawindwa na Waarabu wa Morocco.