Home Habari za michezo KUHUSU YANGA KUINGILIA DILI LA SIMBA KWA RUPIA…ISHU NZIMA IMEKAA HIVI…

KUHUSU YANGA KUINGILIA DILI LA SIMBA KWA RUPIA…ISHU NZIMA IMEKAA HIVI…

Tetesi za Usajili Simba

KLABU ya Yanga imetangaza kuwa inaelekea kukamilisha usajili mmoja mkubwa ambao inatarajia kuutangaza hivi karibuni na kushtua nchi, huku taarifa zikisema imeingilia kati dili la Simba la kumwania straika anayeongoza kwa mabao mpaka sasa kwenye Ligi Kuu, Elvis Rupia.

Awali Simba ilitajwa kuwa kwenye mchakato wa kumsajili mshambuliaji huyo raia wa Kenya na tayari mazungumzo yalishaanza baina ya pande hizo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, alisema kipindi hiki cha dirisha dogo Yanga inafanya usajili wa kuboresha kikosi chake na wanamalizia vitu vichache tu ili kuweza kumtangaza mmoja wa wachezaji ambaye atakuwa gumzo kwenye usajili kipindi hiki.

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa ilikuwa kwenye harakati za mwisho kupata saini ya Rupia na ndio wanatarajia kumtangaza wakati wowote kuanzia sasa akitokea Singida Black Stars.

“Katika dirisha hili dogo la usajili tumeshafanya usajili wa kwanza kwa kumsajili Israel Mwenda kwa mkopo hadi mwisho wa msimu akitokea Singida Black Stars, kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wetu Andre Ntine alinidokeza kuwa wapo wachezaji wengine ambao wataongezwa kwenye kikosi chetu, katika mapendekezo ambayo yametolewa, siku hizi mbili tutakwenda kukamilisha moja ya sajili kubwa sana.

Nimeshuhudia mchakato wake ulivyokuwa wa kusumbuana sana, lakini hatimaye uongozi umeweza kukamilisha dili hilo, kila kitu kimekwenda vizuri bado vitu vichache sana tutakuja kumtambulisha. Uzuri ni kwamba usajili huu hauna mbwembwe sana, ukipata mtu anatakiwa kutambulishwa mapema, watu watashangaa sana na wengine tutawaliza,” alisema Kamwe.

Alisema mbali na huyo, wapo wengine ambao uongozi unaendelea na mazungumzo ingawa kumekuwa na ugumu kupata wachezaji kipindi hiki.

“Hawa wengine tukiwapata sawa, lakini tukiwakosa pia hakuna tatizo kwa sababu dirisha hili ni gumu, unatakiwa umchukue mchezaji ambao anacheza kwenye timu yake, kwa hiyo wakati mwingine ni ngumu sana klabu kukubali kuwaachia,” alisema.

Wakati huo huo kuelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi cha TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kinatarajiwa kuwasili nchini leo saa 11:00 jioni kwa ajili ya mchezo wa raundi ya nne hatua ya makundi unaotarajiwa kupigwa Jumamosi, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, saa 10:00 jioni.

Kamwe amesema maandalizi ya mchezo huo yanaendelea chini ya Kocha Mkuu, Sead Ramovic ambaye ameonekana kukibadilisha kikosi hicho kwa muda mfupi.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa, Desemba 4 mwaka jana, kwenye Uwanja wa Mazembe, Lubumbasi, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Yanga ambao wapo Kundi A, wanahitaji ushindi kwa udi na uvumba kwani ina pointi moja tu mpaka sasa katika michezo mitatu iliyocheza, huku ikiwa inaburuza mkia kwenye msimamo wa kundi hilo.

SOMA NA HII  MAXI AMTAJA MAYELE KWENYE KIKSOSI CHA YANGA TAMAA YAKE IKO HIVI