Home Habari za michezo BAADA YA KUWATUNGUA MAZEMBE JUZI…JINA LA MZIZIE LATUA KWA KATUMBI…ISHU HII HAPA….

BAADA YA KUWATUNGUA MAZEMBE JUZI…JINA LA MZIZIE LATUA KWA KATUMBI…ISHU HII HAPA….

Habari za Yanga leo

KOCHA mkuu wa Yanga, Sead Ramovic amesema hadi sasa hesabu za timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika zipo sawa baada ya kuifumua TP Mazembe kwa mabao 3-1 na kudai kipigo hicho ni kidogo kuliko nafasi walizotengeneza, huku mshambuliaji Clement Mzize akiwashtua Wakongo Kwa Mkapa.

Yanga ilipata ushindi huo katika mechi ya raundi ya nne ya Kundi A na kumfanya Ramovic achekelee akisema kwa sasa imewapa majibu kuwa, wana hesabu sahihi za kutinga robo fainali japo imesaliwa na vikwazo viwili mbele ya Al Hilal ya Sudan na MC Alger zilizokuwa uwanjani usiku wa jana.

Ramovic, aliyepata ushindi wa kwanza CAF akiwa kocha wa Yanga, alisema kuimarika kwa wachezaji wakishika haraka na vizuri falsafa alizowapa zinampa imani wanaweza kushinda mbele ya Al Hilal wikiendi hii ugenini, kisha kurudi nyumbani kuikaribisha MC Alger Januari 18, huku akimtaja Mzize aliyefunga mabao mawili katika ushindi huo wa 3-1, jingine likifungwa na Stephane Aziz KI.

“Ni matokeo yaliyotupa imani kuwa, bado tunaweza kufanya kitu kufikia lengo la kutinga robo fainali, hii ni mechi kubwa tumeiamua kwa nguvu kubwa ya ubora wetu,” alisema Ramovic na kuongeza;

“Tunahitaji kuendeleza matokeo kama haya katika mechi mbili zinazofuata, nafurahi namna wachezaji wanavyoendelea kuimarika, tunacheza mpira tunaotaka tuucheze kwa kumnyima mpinzani nafasi ya kupumua.”

Ramovic pia alisema juzi, Yanga ilistahili kushinda kwa idadi kubwa ya mabao zaidi, kwani ilitengeneza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza na hata cha pili ilipofunga mawili muhimu baada ya kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa ya 1-1 na Mazembe.

“Tunawaheshimu sana wapinzani wetu (Mazembe) lakini tulistahili ushindi mkubwa zaidi jana (juzi) tungeweza kufunga mabao matano hadi sita kama tungeongeza umakini. Ilikuwa ni mechi yenye presha kubwa ya ushindi kwa kila mchezaji lakini tuliendelea kuwatuliza wacheze kwa umakini ili tupate tunachokitaka.”

Kuhusu Mzize, kocha Ramovic alisema licha ya na kufunga mabao mawili, bado anahitaji mwaka mmoja kumzungumzia anafiti nafasi ipi uwanjani.

Kocha huyo alisema hana winga asilia, kiungo mshambuliaji asilia wala beki namba mbili asilia ndio maana amekuwa akifanya mabadiliko kila mara kusaka mchezaji anayefiti nafasi hizo akimgusia zaidi Mzize ambaye ni mshambuliaji anayemtumia zaidi pembeni kama winga na amekuwa akimpa matokeo mazuri.

“Siwezi kusema Mzize sasa nitamtumia kama winga kwa vile amefanya vizuri juzi akifunga mara mbili, hapana nimekuwa nikifanya mabadiliko kila mara nikiwa natafuta nafasi sahihi kwa kila mchezaji akiwamo yeye (Mzize),” alisema Ramovic na kuongeza;

“Ndio maana kiungo mshambuliaji naweza nikamtumia kama mshambuliaji wa mwisho na straika akatumika kama winga, hivyo kuhusu nafasi sahihi ya Mzize naomba niulizwe tena baada ya mwaka mmoja.”

Pia alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wasaidizi anaofanya nao kazi katika benchi la timu hiyo kwa kumsaidia kuboresha utimamu wa wachezaji kwa haraka tofauti na alivyoikuta timu, huku akiweka wazi anafurahishwa na mapokeo ya haraka kwa wachezaji.

ASHTUA TP, KATUMBI AACHIWA KESI

Wakati mashabiki wa Yanga wakitamba na Mzize aliyeitungua kikatili Mazembe, ndani ya timu hiyo ya DR Congo mambo ni tofauti kwani jina la mshambuliaji huyo likipelekwa kwa bilionea wa klabu hiyo, Moise Katumbi.

Kocha msaidizi wa Mazembe, Pamphil Mihayo alisema kuwa anakwenda kumlilia Katumbi avunje benki ili amsajili Mzize na ikishindikana basi iletwe mashine kali mithili ya kinda hilo la Yanga.

Mihayo alisema Mzize ni kama mshambuliaji wa zamani timu hiyo, Mbwana Samata aliyekutana naye katika mechi kama hizo akiwaonyesha balaa zito kisha bosi wao akamsajili.

Aliongeza, Mzize ni mchezaji hatari aliyewasumbua sana juzi Kwa Mkapa.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  ILIBIDI MATAIFA MATATU YAUNGANE KUPATA USHINDI SIMBA