Home Habari za michezo HATMA YA SIMBA, YANGA KUFUZU 16 BORA CAF MIKONONI MWA WAAMUZI HAWA….

HATMA YA SIMBA, YANGA KUFUZU 16 BORA CAF MIKONONI MWA WAAMUZI HAWA….

Habari za Michezo

SIMBA na Yanga zipo ugenini kwa sasa zikijiandaa na mechi za raundi ya tano za michuano ya kimataifa inayopigwa wikiendi hii, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likitangaza waamuzi watakaozihukumu mbele ya wenyeji wao, Bravos ya Angola na Al Hilal ya Sudan.

Simba inayoshika nafasi ya pili katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, itakuwa jijini Angola kuumana na Bravos do Maquis, wakati Yanga iliyo nafasi ya tatu katika Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika itakwaruzana na Al Hilal huko Mauritania zote zikiwania tiketi ya kucheza robo fainali kwa mara nyingine.

Kwa mujibu wa uteuzi wa CAF, mechi ya Simba na Bravo itakayopigwa kuanzia saa 11:00 jioni kwa saa za Angola ambazo ni sawa na saa 1:00 usiku kwa Afrika Mashariki na Kati itaamuliwa na waamuzi kutoka Burkina Faso, wakati ile ya Al Hilal na Yanga wamepewa waamuzi kutoka Rwanda.

Waamuzi wa mechi ya Bravos na Simba wanatarajiwa kuwa, Jean Ouattara anayetekuwa kati akisaidiwa na Seydou Tiama atakayekuwa laini namba moja na Levy Sawadogo atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba mbili, wakati mwamuzi wa akiba atakuwa ni Hamidou Diero.

Rekodi zinaonyesha mwamuzi Jean Ouattara ni mzoefu wa mechi za CAF akitumika zaidi kucheza mechi za timu za taifa zikiwamo za mtoano za Afcon, huku akitajwa sio mtu anayependa sana kutoa kadi uwanjani, lakini huwa ni mkali wachezaji wanapozingua.

Katika mechi hii Simba inahitaji angalau sare tu ili kujihakikisha nafasi ya kucheza robo fainali ya sita kati ya misimu saba iliyoshiriki michuano ya CAF tangu 2018-2019, kwani kwa sasa ina pointi tisa kama walizonazo vinara wa Kunid hilo la A, Cs Constantine ya Algeria ila zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, ilihali Bravos ipo nafasi ya tatu na pointi sita kila timu ikicheza mechi nne hadi sasa.

Timu hizo zilipokutana mwishoni mwa mwaka jana, Simba ilishinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Jean Ahoua kwa mkwaju wa penalti, huku safari hii zinaenda kukutana kila moja ikitoka kupata matokeo tofauti ugenini, Waangola wakilala kwa mabao 4-0 mjini Constantine, wakati Simba ikishinda 1-0 dhidi ya CS Sfaxien.

AL HILAL v YANGA

Kwa upande wa mechi ya Ligi ya Mabingwa itakayopigwa kuanzia saa 4:00 usiku, waamuzi waliopangwa kuchezea mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Cheikha Boidiya wote wanatokea Rwanda ambao ni Samuel Uwikunda atakayesimama kati, huku wasaidizi wakitarajiwa kuwa, Dieudonne Mutiyimana na Didier Ishimwe na mezani atakuwepo Rurisa Fidele.

Katika mchezo huo, Yanga inahitaji ushindi wa aina yoyote kama inahitaji kuweka hai tumaini la kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita na kutolewa kwa penalti na Mamelodi Sundowns ya Afrika iliyotoshana nao nguvu kwa kutoka suluhu mechi zote mbili.

Yanga yenye pointi nne kwa sasa ikishika nafasi ya tatu, ilipoteza mbele ya vinara hao wa Kundi na timu pekee iliyofuzu robo hadi sasa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 2-0 zilipokutana jijini Dar es Salaam.

Msimu huu Yanga haijaanza vizuri hatua ya makundi kwani kwenye mechi tatu imeambulia pointi nne dhidi ya Mazembe ilipotoka sare ya 1-1 na kuichapa nyumbani mabao 3-1, ikipoteza dhidi ya Al Hilal na MC Alger kwa mabao 2-0.

Rekodi zinaonyesha Uwikunda katika mechi saba za kimataifa alizochezesha alitoa kadi za njano 23, ikiwa ni wastani wa kutoa kadi tatu kwa kila mchezo mmoja, lakini akiwa na bahati kwa timu mweyeji kupata matokeo mazuri, kwani katika mechi hizo ni mara moja tu mgeni ametoka na ushindi na ilikuwa ni Petro de Luanda iliyoitandika Etoile du Sahel kwa mabao 2-0 Desemba mwaka jana.

Mwamuzi huyo inakuwa mara ya pili kuzihukumu Yanga na Al Hilal kwani ndiye aliyeuamua mchezo wa raundi ya pili baina ya timu hizo Oktoba 08, 2022 na kumalizika kwa sare ya 1-1, kisha Yanga kwenda kupasuka ugenini 1-0 na kungโ€™olewa Ligi ya Mabingwa na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika ilipofika fainali.

SOMA NA HII  JULIO:- YANGA WALE WALE TU....HAWANA JIPYA MPAKA SASA...