Home Habari za michezo BAADA YA KUWAPASUA WAARABU DAR…..FADLU APANDISHA ‘KIBRI’ SIMBA…

BAADA YA KUWAPASUA WAARABU DAR…..FADLU APANDISHA ‘KIBRI’ SIMBA…

Habari za Simba leo

WAKATI Simba ikitarajiwa kukutana na timu moja kati ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, Asec Mimosas ya Ivory Coast au Al Masry ya Misri, Kocha Mkuu wa Klabu hiyo, Fadlu Davids, amesema haiogopi timu yoyote ambayo watapangwa kucheza nayo hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Aidha, amesema lengo la kutaka kuongoza kundi lilikuwa na nia moja tu ya kuanzia mechi ugenini na kupata faida ya kumalizia nyumbani na si vinginevyo.

Fadlu alisema hayo juzi, baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-0 Jumapili iliyopita dhidi ya CS Constantine ya Algeria, ikiwa ni mechi ya mwisho Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika, iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Alisema haiogopi timu yoyote hata zile ambazo zimemaliza nafasi ya kwanza angepambana nazo vizuri tu, lakini alipigania zaidi kushinda ili kuongoza kundi kwa ajili ya kumalizia mechi nyumbani bila kujali ni timu gani atakayocheza nayo.

“Tumepata tulichokitaka, nacho ni kumalizia nyumbani tu na kuanzia ugenini, wala hatujali tutacheza na nani, hata hizo timu zilizomaliza juu ya makundi tungeweza kucheza nazo, na tutacheza nazo kama tukivuka hapa.

“Kwa mimi hapa, michuano ya Kombe la Shirikisho sasa ndiyo inaanza. Tunafahamu kufika robo fainali ni mafanikio, lakini kwetu hatuwezi kushangilia sana. Ni mashabiki tu ndiyo wanaopaswa kushangilia kwa sababu ni rekodi na mafanikio ya klabu, lakini kwangu na wachezaji wangu nimewaambia, wasishangilie sana mashindano yenyewe ndiyo yanaanza sasa tunatakiwa kuhakikisha tunakuwa tayari kwa robo fainali,” alisema Fadlu.

Kuhusu mechi hiyo, alisema awali wachezaji wake waliathirika kucheza bila mashabiki, lakini baadaye walizoea.

“Tulicheza mechi bila mashabiki, mwanzo iliathiri timu yangu kwa kiasi fulani, lakini baadaye walizoea, napenda kuwashukuru wachezaji wangu wameonekana wameanza kukomaa kiasi cha kutosha, toka siku ya kwanza tulipocheza michezo hii dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya, hadi leo, kikosi kinaonekana kujengeka na kuwa imara siku hadi siku, wakiwa na mpira wanafanya kazi, na wanapokuwa hawana mpira wanasaidiana kuutafuta,” alisema.

Simba itakutana na timu moja kati ya tatu zilizoshika nafasi ya pili kwenye makundi mengine, Stellenbosch, kutoka Kundi B, Asec Mimosas kutoka Kundi C ama Al Masry kutoka Kundi D.

Mechi za kwanza zitachezwa kati ya Machi 28 hadi 30, Simba na timu zingine zilizoshika nafasi ya kwanza kwenye makundi yao ambazo ni RSB Berkane ya Morocco kutoka Kundi B, USM Alger ya Algeria kutoka Kundi C pamoja na Zamalek ya Misri kutoka Kundi D, zikianzia ugenini na mechi za marudiano zitachezwa, Aprili 4 hadi 6 nyumbani, ambapo Wekundu wa Msimbazi watamalizia mechi yake Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kocha Mkuu wa CS Constantine, Kheireddine Madoui, ambaye awali alionekana kufurahi Simba kucheza bila mashabiki, aliipongeza timu hiyo, akisema ilicheza vizuri zaidi kuliko alivyodhania.

“Mchezo ulikuwa mgumu sana, kipindi cha kwanza tulikuwa vizuri, lakini cha pili wachezaji wangu walionekana kuchoka, Simba ilionekana kutawala zaidi, hatukuweza kuhimili mashambulizi.

“Mwanzo tulidhani kukosekana kwa mashabiki ingetusaidia kucheza vizuri bila presha maana wanajulikana Afrika kwa kuwapa morali wachezaji wao ili kushinda, lakini nimeshangazwa wamecheza vizuri zaidi ya nilivyotarajia, nawapongeza kwa hilo,” alisema.

Kocha huyo ambaye timu yake imeshika nafasi ya pili, ikitarajiwa kucheza hatua ya robo fainali na zilizoshika nafasi ya kwanza makundi mengine, alisema angependa kukutana na wapinzani wao kutoka nchi moja, USM Alger.

“Mimi ningependa zaidi kukutana na wapinzani wetu USM Alger kwa sababu moja kati ya timu ya Algeria, itakuwa imejikatia tiketi ya kwenda nusu fainali

“Ningependa zaidi kukutana na wapinzani wetu USM Alger kwa sababu mbalimbali ambazo sitozisema hapa, lakini moja kati ya timu ikishinda itakuwa imejikatia tiketi ya kwenda nusu fainali itakuwa ni faida kwa nchi ya Algeria,” alisema kocha huyo.

Ikumbukwe pia Novemba 21, mwaka jana, CS Constantine ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya USM Alger zilipokutana kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Algeria, jambo ambalo linaonesha kocha huyo anajua anaweza kuwamudu wapinzani wao hao.

SOMA NA HII  MRITHI WA MGUNDA SIMBA APATIKANA