KATIKA dakika 270 sawa na mechi tatu za mwisho kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha wa Simba, Fadlu Davids ameonyesha kujipata kutokana na namna ya upangaji wa kikosi chake cha kwanza kilichompa heshima kubwa.
Mechi hizo tatu zilizochezwa ndani ya kipindi cha takribani siku 14, ziliipa Simba pointi zilizoivusha kwenda robo fainali ikiwa ni mara ya sita inafanya hivyo kwenye michuano ya CAF kati ya misimu saba kuanzia 2018-2019.
Ndani ya siku hizo ambazo Simba imecheza mechi ngumu katika mataifa matatu tofauti, Tunisia dhidi ya CS Sfaxien, Angola dhidi ya Bravos do Maquis na nyumbani Tanzania dhidi ya CS Constantine, timu hiyo ilikusanya pointi saba ikishinda mechi mbili na sare moja. Haijapoteza huku ikifunga mabao manne na kuruhusu moja ikiwa na clean sheet mbili, huku ikimaliza kinara wa Kundi A.
Msauzi huyo ni wazi kile ambacho alikuwa akikitengeneza kwa miezi mitano tangu akabidhiwe kikosi hicho sasa ni kama amekipata na anatamba nacho.
Katika michezo hizo tatu mfululizo, kikosi chake cha kwanza kilikuwa hivi; Moussa Camara, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein βTshabalalaβ, Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Elie Mpanzu, Fabrice Ngoma, Leonel Ateba, Jean Charles Ahoua na Kibu Denis.
Simba imeruhusu bao moja tu ambalo ilikuwa Januari 12 wakiwa Angola ambako walitoa sare ya bao 1-1 na ilikuwa ni baada ya Che Malone kufanya makosa, nyavu zao hazikuguswa wakiwa nyumbani, Januari 19 dhidi ya Constantine na hata walipokuwa ugenini pia, Januari 5 huko Tunisia dhidi ya CS Sfaxien.
Camara akiwa golini, amefanya kazi kubwa akisaidiwa na Kapombe, Tshabalala, Che Malone na Hamza huku mbele yao, Ngoma na Kagoma wakidumisha ulinzi.
Vijana hao wa Fadlu, wamefunga mabao manne katika michezo hiyo, ambayo wameonyesha ufanisi mkubwa kwa kushambulia mara 52, changamoto iliyopo bado ni katika utumiaji wa nafasi ambazo wanatengeneza, hili ni eneo ambalo Msauzi huyo anatakiwa kuendelea kulifanyia kazi.
Simba ilifanya mashambulizi mara saba dhidi ya CS Sfaxien walipoibuka na ushindi wa bao 1-0 huku mashuti yaliyolenga lango yakiwa mawili, walikuwa na umiliki wa mchezo kwa asilimia 44.
Katika mchezo uliofuata ambao walitoka sare dhidi ya Bravos do Maquis ilifanya mashambulizi mara 25, mashuti yaliyolenga lango yalikuwa saba, umiliki wa mchezo ni asilimia 56.
Katika mchezo wa mwisho ambao walikuwa nyumbani na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Constantine, Simba ilifanya mashambulizi 20, mashuti ambayo yalilenga lango ni matano, walikuwa na umiliki wa mchezo kwa asilimia 69.
Ukiachana na mechi hizo tatu za mwisho, zile mbili za kwanza kikosi kilikuwa na mabadiliko ya wachezaji kadhaa lakini wapo waliokuwa hawakosekani.
Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Bravos ambao Simba ilishinda 1-0, kikosi kilianza hivi; Camara, Kapombe, Tshabalala, Che Malone, Hamza, Ngoma, Ladack Chasambi, Augustine Okejepha, Steven Mukwala, Ahoua na Kibu.
Dhidi ya Constantine ugenini Simba ilopofungwa 2-1, kikosi kilikuwa hivi; Camara, Kapombe, Tshabalala, Chamou Karaboue, Hamza, Okejepha, Kibu, Ngoma, Ahoua na Ateba.
Mchezo wa tatu nyumbani dhidi ya Sfaxien ambao Simba ilishinda 2-1, kikosi kilikuwa hivi; Camara, Kapombe, Tshabalala, Che Malone, Hamza, Ngoma, Awesu Awesu, Debora Mavambo, Ateba, Ahoua na Kibu.
MSIKIE FADLU
Fadlu alisema wanachotakiwa kufanya ni kuendelea kuonyesha makali yao badala ya kubweteka kutokana na majukumu makubwa yaliyopo mbele yao, kuanzia katika mashindano ya ndani hadi kimataifa na wametinga hatua ya robo fainali.
βSio tu kwamba tumemaliza hatua ya makundi tukiwa vinara, lakini tunahitaji kuendelea kuwa makini. Hatuwezi kubweteka na hatuwezi kuridhika na kile tulichofanya.
βSafari yetu inaendelea na hatujafika mwisho. Tunapambana kwa ajili ya mafanikio makubwa zaidi. Tunahitaji kuendelea kuboresha kila kipengele cha mchezo wetu, kutoka kwa ulinzi hadi kwenye kumalizia nafasi,β alisema Fadlu.
Kocha huyo alisisitiza licha ya mafanikio haya, Simba inaendelea kupambana kwa kila mechi, ikiwemo michuano ya ndani kama Ligi Kuu na Kombe la FA.
βTunaendelea kupambana kwa ajili ya mafanikio katika mashindano ya ndani pia. Tunaongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi moja mbele ya Yanga, na kwa Kombe la FA, wikiendi ijayo tuna mechi. Haya yote ni mashindano makubwa ambayo lazima tuyazingatie,β alisema.