Home Habari za michezo RAMOVIC:- USHINDI KIRAHISI LIGI KUU UMETUPONZA YANGA CAF…LIGI TZ NI DHAIFU….

RAMOVIC:- USHINDI KIRAHISI LIGI KUU UMETUPONZA YANGA CAF…LIGI TZ NI DHAIFU….

Habari za Yanga SC

KOCHA Mkuu wa Yanga, Saed Ramovic, amesema moja ya sababu zilizofanya timu yake ishindwe kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni udhaifu wa Ligi ya Tanzania, ambayo haina timu nyingi ngumu na zenye ubora, nguvu na kasi, ambazo zingesababisha timu yake kuzoea hali hiyo.

Akizungumza juzi baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria, wakilazimishwa suluhu Uwanja wa Benjamin Mkapa, na kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali kutoka Kundi A, Ramovic, aliwasifu wachezaji wake kwa kupambana kadri ya uwezo wao, lakini walikutana na timu ngumu, yenye wachezaji bora na wazoefu, tofauti na wale ambao wanakutana nao kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tunapaswa kuwa wakweli kwamba ligi ya hapa Tanzania, ugumu unaokutana nao unapocheza dhidi ya timu nyingine za Tanzania si wa kiwango kikubwa sana. Ukiona ligi za Algeria, Afrika Kusini, Morocco, Tunisia, tunahitaji nguvu hiyo ya juu ili kushindana na tuweze kuzoea hali hiyo.

“Ukali wa ligi ya Tanzania, ni mdogo sana ukilinganisha na nchi hizo, wao ligi yao ni ngumu na kila timu kali sana, tunahitaji ugumu kama wa ligi hizo ili tushindane,” alisema kocha huyo.

Alisema urahisi wa kupata ushindi katika michezo ya Ligi Kuu hauwajengi, badala yake unawafanya kudumaa na kupata shida wanapocheza na timu ambazo zinatoka kwenye ligi zenye ushindani, akisema suala hili likifanyiwa kazi haitokuwa faida kwa Yanga tu, bali kwa timu zote nchini ambazo zitakwenda kucheza mechi za kimataifa.

Aliwasifia wapinzani wao, MC Alger ambao walicheza zaidi nyuma ya mpira na kuwapa kazi kubwa kuwafungua kutokana na kuwa bora kwenye sanaa ya uzuiaji.

“Haikuwa rahisi kuweza kuwafungua, walicheza nyuma ya mpira, tulijitahidi sana, lakini sanaa yao ya uzuiaji ilikuwa nzuri na bora,” alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, alikiri kuwa wapinzani wao walichanga karata yao vizuri na imewalipa, huku akisema nguvu na hasira zao sasa wanazielekeza kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA.

“Tulifanya kila tunachoweza kukifanya, lakini jamaa walikuwa imara sana, hawakuja Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya kitu chochote kile zaidi ya kutafuta sare na wameipata, soka limeamua matokeo.

“Tumepoteza, tunakwenda kujipanga, tutarudi tukiwa imara zaidi. Hasira zetu sasa tunarudi kwenye ligi ili kutetee makombe yetu, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA,” alisema Kamwe.

Matokeo hayo, yameifanya MC Alger kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikifikisha pointi tisa, ikimaliza mechi sita za Kundi A, ikiwa nafasi ya pili na kuiacha Yanga ikimaliza nafasi ya tatu, ikiwa na pointi nane.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa MC Alger, Khaled Benyahia, alisema amefurahi kuingia hatua ya robo fainali licha ya kuwa mchezo haukuwa rahisi.

“Tumefurahi kwani malengo yetu yalikuwa ni kuingia hatua ya robo fainali ya mashindano haya, kwa sasa tunakwenda kujipanga kwa ajili ya michezo ijayo,” alisema Benyahia.

Alisema Yanga ni timu nzuri yenye wachezaji wengi wenye uzoefu, hivyo waliingia wakiwa na tahadhari ya kutowaruhusu kupata bao.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, alisema kutolewa kwa Yanga kunawafanya kwenda kufanya vzuri kwenye michezo ya Ligi Kuu.

“Yanga kutolewa hapa nafahamu watajipanga waweze kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu, hicho ni kitu cha kawaida kwenye mpira, kuna kufunga, kufungwa na kutoka sare, alisema Mwinjuma.

SOMA NA HII  MBRAZIL SIMBA AWATUPA DONGO HILI ZITO YANGA...MAYELE ATUMA SALAMU MSIMBAZI