Home Habari za michezo HII HAPA TAMU, CHUNGU YA SIMBA KUCHEZA BILA MASHABIKI KWA MKAPA…..

HII HAPA TAMU, CHUNGU YA SIMBA KUCHEZA BILA MASHABIKI KWA MKAPA…..

Habari za Simba leo

IKIWA ndio timu pekee iliyobakia katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kutoka Afrika Mashariki na Kati, wachezaji wa Simba wamesema walikutana na wakati mgumu kucheza mechi kwa mara ya kwanza wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani bila ya mashabiki.

Simba iliwakaribisha CS Constantine kutoka Algeria kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ikiwa bila ya mashabiki, ingawa mechi hiyo ilimalizika kwa wenyeji kupata ushindi wa mabao 2-0 na kuifanya ifikishe pointi 13 ambazo ziliwapelekea kuongoza Kundi A katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

CAF iliwaadhibu Simba kucheza bila mashabiki na kulipa faini ya Dola za Marekani 40,000 kufuatia vurugu za mashabiki zilizojitokeza katika mechi ya hatua ya makundi dhidi ya CS Sfaxien kutoka Tunisia iliyochezwa Desemba 15, mwaka jana.

Wachezaji wa Simba walisema iliwaweka katika nafasi ngumu kwa sababu hawajazoea kucheza bila mashabiki wakiwa nyumbani.

Shomari Kapombe, Edwin Balua na Yusuph Kagoma, walisema mwanzoni mwa mchezo iliwaathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu siku zote hucheza huku wakishangiliwa, kutiwa moyo na kuhimizwa, lakini siku hiyo kila wanapogusa mpira hawakuwa wakisikia chochote.

Kapombe alisema hali hiyo ‘iliwaumiza’, lakini kadri muda ulivyozidi kwenda walikumbuka nini wanatakiwa kufanya katika mchezo huo.

“Mechi ile uwanjani ilikuwa nzuri sana, jamaa walizuia sana, mwanzo tulipata shida, tukatengeneza nafasi chache tukashindwa kuzitumia, kipindi cha pili mwalimu alituambia udhaifu wao na jinsi ya kuvunja ukuta wao.

Lakini kwa upande wa pili ‘hatukuinjoi’ kucheza bila mashabiki, binafsi nainjoi tunapocheza zaidi tukiwa kando na mashabiki wetu, walihitajika sana siku ile, lakini hatuwezi kulalamika ni kitu ambacho kimetokea, tunaamini mechi ijayo tutakuwa wote na sisi tutakuwa na furaha sana, na kwa sababu hawakuwapo mechi iliyopita, mechi ya robo fainali watajaza uwanja, watashangilia sana, na watatupa moyo sana wa kupambana kwa sababu tuliwamisi mechi iliyopita, nao walitumisi pia,” alisema Kapombe.

Kwa upande wa Kagoma alisema kwake pia lilikuwa jambo gumu, lakini baadaye alikumbuka mashabiki wao wapo sehemu fulani wamekusanyika pamoja kwa ajili ya kuwashangilia.

“Mechi ilikuwa ngumu sana, jua kali mno, pia kucheza bila mashabiki ilikuwa ngumu, ila nilikuwa nikicheza nawakumbuka, najua wapo sehemu wamekusanyana wanaangalia mpira, wanatushangilia, wengine vibanda umiza, nikivuta picha yao jinsi watakavyokuwa wanashangilia basi inanipa nguvu ya kupambana uwanjani,” alisema Kagoma.

Winga Balua amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kumalizia deni katika ule mpango wa ‘tunawajibika pamoja’, ili mechi ya robo fainali wajumuike pamoja uwanjani.

“Ilikuwa ngumu kucheza hivi, kwa sababu mashabiki wa Simba lile vibe lao huwa wanatuongezea kitu kikubwa sana, watuongezea umakini, kasi, nguvu na kupambana zaidi hata maeneo ambayo unaona ni magumu, lakini hatukuwa na jinsi.

Hatua inayokuja ya robo fainali nadhani mechi itakuwa bora zaidi kwa sababu tutaongeza umakini sana, mashabiki wetu tunawaomba wakamilishe ile pesa wanayochanga ili waweze kuingia katika mchezo wa robo fainali na watushangilie kwa nguvu, ila wajitahidi kutorudia kilichopita,” Balua alisema.

CAF pia iliwapiga faini ya Dola za Marekani 60,000 Waarabu hao wa Tunisia kufuatia wachezaji, mashabiki na viongozi wao wa benchi la ufundi kufanya vurugu katika mechi hiyo.

Ikicheza bila mashabiki, Simba ilipata ushindi wa mabao 2-0, shukrani kwa Kibu Denis na Leonel Ateba.

Simba sasa inasubiri kufahamu mpinzani wake wa hatua ya robo fainali kupitia droo itakayochezwa mwishoni mwa mwezi huu.

SOMA NA HII  HIVI NDIVYO THANK YOU ZA SIMBA, YANGA ZILIVYOGEUKA NA KUWA WELCOME