Home Habari za michezo TABORA UTD vs SIMBA ….HAYA HAPA UNAYOPASWA KUYAJUA LEO KABLA YA MECHI….

TABORA UTD vs SIMBA ….HAYA HAPA UNAYOPASWA KUYAJUA LEO KABLA YA MECHI….

Tabora vs Simba

NGOJA tuone leo itakuwaje pale ambapo Tabora United, vijana wa kocha Anicet Kiazayidi watakapokuwa wenyeji wa Simba inayonolewa na Fadlu Davids katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao unatolewa macho na kila mmoja kutokana na rekodi zilivyo na ushindani wa duru la pili la Ligi Kuu Bara.

Mchezo huo uliopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora kuanzia saa 10:00 jioni, wenyeji wanaingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya duru la kwanza kuchakazwa 3-0 na Simba.

Hiki ni kiporo kingine baada ya jana kushuhudia Yanga ikipambana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam. Kumbuka baada ya leo, mechi za duru ya pili raundi ya 17 zitaendelea Februari 5, kukiwa na mchakamchaka wa hadi Mei 25 mwaka huu msimu utakapofikia tamati.

TABORA KUENDELEZA UBABE KWA VIGOGO?

Simba wanaingia katika mchezo vichwani mwao wakitambua wanakutana na timu tishio kwa vigogo.

Tabora United msimu huu imekuwa tishio kwa Yanga na Azam ambazo zilipokutana duru la kwanza imeshinda dhidi yao, lakini kabla ya hapo ilikwama kwa Simba.

Kushinda dhidi ya timu hizo, inatoa tahadhari kwa Simba ambayo ilimaliza duru la kwanza ikiwa kileleni mwa msimamo huku hesabu zao ni kuona pia inaendelea kukaa hapo hadi mwisho wa msimu. Kitendo cha Simba kupoteza pointi leo kitaashiria kwamba hesabu zao zitaingia doa.

Kocha Fadlu ameizungumzia Tabora na namna ilivyozisumbua Yanga na Azam huku akitoa tahadhari ya kwenda kukabiliana nayo sambamba na walivyowasoma wapinzani wao hao.

“Ni timu ngumu, tuliiona ilivyocheza dhidi ya Yanga, wapo haraka katika kushambulia, unapowashambulia huwaacha washambiliaji kwa ajili ya kusubiri mashambulizi ya kushtukiza, hivyo basi unapopoteza mpira hutakiwa kuruhusu wapate nafasi ya kufanya shambulizi la haraka wala kuiwahi mipira inayorejea wanapokushambulia.

“Hatutacheza kwa kuacha nafasi kubwa, tutabana nafasi na kuhimili mashambulizi ya haraka kutoka kwao kwani wana wachezaji wenye kasi ambao ni hatari kukabiliana nao, mawinga wao wana uwezo wa kuingia ndani na kupiga mashuti.

“Tumewachambua kwa kina, tunafahamu namna ya kujilinda na kuwashambulia. Tunawaheshimu kwani tunajua ni timu hatari,” alisema Fadlu na kuongeza:

“Hatujajiandaa kwa Tabora pekee, bali kwa ajili ya mechi zote zilizobaki kumalizia msimu. Tunawaheshimu Tabora, ni timu tofauti na tuliyocheza nayo mara ya mwisho wakiwa na kocha mpya, wanaonekana kuimarika vizuri.

“Nimejaribu kuangalia mchezo tuliocheza duru la kwanza nimeona ni timu tofauti kwa sasa, itakuwa mechi ya tofauti kutokana na kuimarika kwao lakini hata sisi tuna timu ya tofauti.

“Kama nilivyosema Tabora tunaiheshimu, kama tunavyocheza dhidi ya Yanga, KenGold, Kagera au timu yoyote tunajiandaa kulingana na mpinzani tunayekwenda kukutana naye kwani huwa ni mechi tofauti.

“Hata staili ya kushambulia itakuwa tofauti, haiwezi kuwa sawa na ilivyokuwa dhidi ya Constantine au Kilimanjaro. Tusubiri tuone itakuwaje licha ya kwamba uwanja nao utaamua namna ya uchezaji wetu kwa sababu hauruhusu kupiga pasi nyingi lakini tutajaribu kucheza kwa mtindo wetu na kufunga mabao mengi kitu ambacho ni muhimu sana.

“Awesu hatakuwepo, alitolewa kipindi cha kwanza dhidi ya Kilimanjaro, nilitarajia atakuwa sawa lakini hatuwezi kuhatarisha afya yake ndiyo maana hatujasafiri naye, pia Aishi hatakuwepo kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya.”

Simba wakali wa hizi kazi

Wakati Tabora wakionekana kuwa kiboko ya vigogo, rekodi zinaonyesha Simba imekuwa na matokeo mazuri inapokutana na timu hiyo.

Hii itakuwa ni mara ya nne kukutana kwao ambapo mara tatu zote Simba ilipata ushindi, mbili nyumbani na moja ugenini.

Katika mechi hizo tatu ambazo Simba imeshinda, Tabora United haijafunga bao lolote huku mara ya mwisho uwanjani hapo Simba ikishinda 4-0. Matokeo yapo hivi; Simba 3-0 Tabora United, Simba 2-0 Tabora United na Tabora United 0-4 Simba. Pia Simba msimu huu katika mechi saba za ugenini ndani ya ligi, imeshinda zote ikifunga mabao 12 na kuruhusu mawili ikiondoka uwanjani na clean sheet sita.

Kwa upande wa Tabora ikiwa nyumbani, imecheza mechi nane, imeshinda nne, sare tatu na kupoteza moja ikifunga mabao 10 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba, ikiambulia clean sheet nne.

Kocha wa Tabora United, Anicet Kiazayidi alisema tayari amewaandaa vijana wake licha ya kwamba kuna baadhi wameondoka akiwemo kiungo Morice Chukwu aliyerejea Singida Black Stars, lakini anaamini waliopo watafanya vizuri.

“Tuna wachezaji ambao wapo tayari kwa mechi hii, haijalishi nani hayupo wala nani hana kibali, kesho (leo) wachezaji watakaocheza ndiyo hao walioandaliwa na tunaamini watafanya vizuri,” alisema kocha huyo.

Vita ya nafasi

Simba inapamabana kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kutokana na sasa kuwa na pointi 40, wakati Tabora inahitaji ushindi ili kujikita zaidi nafasi ya tano ikikusanya pointi 25.

Mwamuzi sasa

Mchezo huo utaamuliwa na mwamuzi Amina Kyando kutoka Morogoro akisaidiwa na Robert Luhemeja na Fatma Mambo.

Huu utakuwa mchezo wa pili kwa mwamuzi huyo kuziamua timu hizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita Mei 6, 2024 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Simba iliposhinda kwa mabao 2-0.

SOMA NA HII  NEEMA ZAZIDI KUMIMINIKA YANGA....WASAINI MKATABA WA KUIPA KLABU MABILIONI YA PESA KAMA SIMBA....KAZI NDIO INAANZA...