Home Habari za michezo TAREHE MPYA DABI YA SIMBA, YANGA SHAKANI….RAGE AIBUKA NA HILI JIPYA…

TAREHE MPYA DABI YA SIMBA, YANGA SHAKANI….RAGE AIBUKA NA HILI JIPYA…

Habari za Michezo

WAKATI Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ikiwataka wadau wa soka kuwa watulivu kipindi hiki wakiendelea kusubiri taarifa itakayotolewa kueleza kwa nini mchezo wa Simba na Yanga uliokuwa uchezwe Machi 8, mwaka huu haukuchezwa na hatima yake, mechi hiyo kwa sasa inaonekana kuwa ‘njiapanda’ kufanyika.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Steven Mguto, alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote mpaka hapo kikao kitakapokaa na kutoa maamuzi.

“Kwa sasa siwezi kuzungumza chochote juu ya sakata hilo ninaomba wadau wa soka wawe na subira tukimaliza kikao chetu tutatoa taarifa kwa umma,” alisema Mguto.

Mwenyekiti huyo alisema maamuzi yatatolewa hivi karibuni kwani uchunguzi bado unaendelea kufanyika mpaka sasa.

Alisema licha ya Yanga kutoa taarifa ya kutaka uongozi huo uachie ngazi hawezi kusema mpaka hapo watakapotoa tamko lingine.

“Subirini kupata tamko lingine kutoka kwetu nasisitiza kila kitu kitawekwa sawa, maana kwa sasa kila mtu anazungumza anachojua,” alisema.

Klabu ya Yanga jana ilitoa tamko rasmi kuwa inataka haki yake ya ushindi wa pointi tatu na mabao matatu, baada ya kile walichoeleza kuwa wapinzani wao Simba kugomea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliotakiwa kucheza, Jumamosi iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo, ilieleza kuwa baada ya kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika kwa njia ya mtandao, kamati ilijadiliana na kukubalia mambo mbalimbali, ikiwamo kutaka haki yake ya ushindi kama ilivyoelezwa kwenye kanuni pindi timu moja inapogomea mechi.

“Klabu ya Yanga inataka kupewa haki yake ya ushindi kama ilivyoelezwa kwenye kanuni pindi timu moja inapogomea mechi.

“Kamati ya Utendaji, pia imekubaliana kutoshiriki mchezo namba 184, kwa tarehe yoyote itakayopangwa,” ilieleza taarifa hiyo.

Mbali na hilo, Kamati hiyo ililitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), kuivunja Kamati ya Uendeshaji wa Ligi Kuu.

“Kutokana na mfululizo wa uvunjifu na kushindwa kusimamia Kanuni za Ligi Kuu, Klabu ya Yanga imekosa imani na Kamati ya Uendeshaji wa Ligi Kuu, hivyo tunaliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), kuivunja na kuteua viongozi waadilifu, wenye nia njema kwa maslahi mapana ya mpira wetu,” taarifa hiyo ya Yanga ilibainisha.

Aidha, ilidai kuwa katika kikao kilichohudhuriwa na klabu zote mbili, wasimamizi wa michezo, watathmini, waamuzi na makamishna, Klabu ya Simba haikutoa taarifa ya kutaka kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa, siku moja kabla ya mchezo husika kwa ajili ya kufanya mazoezi.

“Katika hali ya kushangaza, usiku wa Machi 7, Klabu ya Simba iliwasili uwajani ikiwa na magari kadhaa kwa ajili ya kufanya mazoezi huku wakifahamu hawakufuata taratibu za kupata haki yao kikanuni kama ilivyoanishwa na Bodi ya Ligi, huku mamlaka ya uwanja ikikataa kuwaruhusu kuingia ndani ya uwanja, lakini usiku wa kuamkia siku ya mchezo, ikatoa tamko rasmi la kugomea mchezo huo kwa kigezo cha kutopata nafasi ya kufanya mazoezi, huku wakielewa dhahiri kwamba hawakuwa wamefuata taratibu,” taarifa ya Yanga ilieleza.

Hata hivyo, wakati Yanga ikitaka kupewa ushindi wa chee, Rais wa zamani wa Simba na aliyewahi kuongoza Chama cha Soka nchini (FAT) kwa sasa TFF, Ismail Aden Rage, amesema haiwezekani kwa Yanga kupata ushindi kwa sababu mechi hiyo iliahirishwa na mamlaka za soka na si Simba.

Rage alipingana na madai hayo ya Yanga ya kutaka kupewa pointi tatu na mabao matatu, akisema kilichopo sasa ni kwamba TFF na Bodi ya Ligi wameahirisha mchezo huo na si Simba wamegomea.

Akizungumza kwa simu kutoka nchini India, Rage alisema katika sakala lote hili wa kulaumiwa ni mabausa wa Yanga kwa kuwazuia wachezaji wa Simba kufanya mazoezi, hicho ndicho chanzo cha yote yaliyotokea.

“Kisheria ni kwamba Simba hawajagomea mchezo, hapa tunasema tukio limeshapitwa, hilo suala halipo tena, hapa kuna suala la Shirikisho la Mpira wa Miguu na Bodi ya Ligi wameahirisha mechi, kwa hiyo Simba hapa unawatoa kabisa hawapo kwenye tukio la kugomea mechi.

“Mwenye kuendesha mashindano ndiye mwenye mamlaka ya kuahirisha mchezo, ndiyo maana hata Yanga walipoenda uwanjani hakukuwa na yeyote yule, si viongozi, makamishna wala waamuzi, hii ina maana mechi ilikuwa tayari imeahirishwa, huwezi kudai wala kupewa pointi kwa hali hiyo, kama tamko la Simba lilivyokuwa mwanzo na mamlaka isingeahirisha, hapo ndiyo tungezungumza vingine,” alisema Rage.

Alitupa lawama kwa walinzi wa Yanga, akisema wao ndiyo chanzo cha yote yaliyotokea, ambapo kazi yao ilikuwa ni kulinda usalama ndani ya uwanja na si nje kwani kazi hiyo ni ya askari polisi.

“Kanuni ipo wazi timu ngeni lazima ipewe uwanja ifanye mazoezi, lawama kubwa ziende kwa hao mabausa ya Yanga, walikuwa wanafanya nini siku hiyo uwanjani? Jibu utakalopata utaambiwa kuwa walikuwa wanalinda, unajua kwa sasa mabaunsa wa Simba na Yanga hivi sasa wanaitwa walinzi wa uwanjani.

“Wanalinda wakati mechi inachezwa, sio walinzi wa kulinda nje ya uwanja, walifanya kazi ambayo si yao, wao walitakiwa kulinda usalama wa ndani, siku hizi FIFA hawataki askari polisi ndani ya uwanja, badala yake walinzi hao ambao wana mafunzo, wanakaa ndani ya uwanja, askari wao nje, hivyo kazi ya huko nje ya uwanja ilikuwa ya polisi,” alisema kiongozi huyo wa zamani wa soka nchini.

Naye Wakili Alex Mgongolwa, alisema kuwa, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), haikuwa na jukumu la kuiahirisha mechi hiyo, kwani hakukuwa na kanuni iliyowataka kufanya hivyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, wakili huyo alisema maombi yaliyopelekwa mbele yao na Klabu ya Simba hayakuwa ya kuahirisha mchezo huo, hivyo hawakuwa na mamlaka ya kuliamua kwa wakati ule.

“Maombi mbele yao hayakuwa ya kuahirisha mchezo, hata kama yangekuwa hivyo wangetamka kuwa hawana mamlaka ya kuliamlia kwa wakati ule.

“Maana ya kikanuni na kutafuta haki kwenye vyombo vya haki, unachopeleka ni malalamiko na maombi ya nini unakitaka ili kamati inapothibitisha ikuzawadie au ikupe nafuu gani, wewe huiambii kamati kuwa kama bila kufanya hivi hatufanyi hivi, hatuendi mahakamani kuiambia kuwa bila kumfunga huyu sisi hatuji tena mahakamani, taratibu za utafutaji wa haki haziko hivyo,” alisema Mgongolwa.

SOMA NA HII  MBEYA CITY YAMALIZA SHOO MAPEMA...YANYAKUWA KIUNGO MKALI WA SIMBA KIULAINIII..