Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuacha kuwapa nafasi watu wanaoibeza timu yao, akisisitiza kuwa Simba haijaenda kukamilisha ratiba bali inapigania hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba SC inajiandaa kwa mchezo wa marudiano wa robo fainali dhidi ya Al Masry, baada ya kupoteza mechi ya kwanza iliyochezwa nchini Misri kwa mabao 2-0. Timu hizo zitavaana tena Jumatano, Aprili 9, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu mchezo huo, Ahmed amesema ni wakati wa kila mshabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanjani na kuisapoti timu yao, kwani wana dhamira ya kweli ya kwenda kuvunja mwiko wa kuishia robo fainali.
“Shabiki yeyote anayekereka na kuumizwa na Simba kuishia robo, basi suluhisho lake ni moja tu—kununua tiketi na kufika uwanjani kushuhudia mnyama akienda nusu fainali. Hakuna njia nyingine, lazima tumtoe Mwarabu, lazima tushinde,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa timu ya Simba itapambana kwa nguvu zote kuhakikisha inashinda nyumbani na kuwatoa Al Masry, huku akisema kuwa siyo muda wa kuiaibisha klabu wala taifa katika uwanja wa nyumbani.
“Tutafanya kila kinachowezekana kuhakikisha Simba inaingia nusu fainali. Hatuko tayari kwa namna yoyote kuiaibisha Benjamin Mkapa wala Watanzania,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Ahmed, mafanikio ya Simba si jukumu la wachezaji pekee, bali ni wajibu wa kila shabiki kuhakikisha wanafika uwanjani na kuonyesha sapoti yao ya dhati.
“Wapo watu wamekaa kusubiri Simba ifeli ili wacheke. Hatuwapi nafasi! Tunaangalia Al Masry, tuna imani tutawatoa. Hawa si Waarabu wa kutisha—ni wa kawaida tu,” amesema kwa msisitizo.
Ahmed amehitimisha kwa kusema kuwa Simba ni klabu ya kupambana hadi mwisho na haitishwi na matokeo ya ugenini. Amesisitiza kuwa hasira ya kufungwa Misri imeongeza ari ya ushindi nyumbani.
“Kama tuliweza kumfunga Al Ahly, kwa nini tushindwe kwa Al Masry? Kabati lilidondoka kule, lakini sasa limesimama imara nyumbani kwa ajili ya vita,” amesema.
Katika mchezo huo wa marudiano, wageni maalum watakaohudhuria ni pamoja na Rais wa TFF, Wallace Karia, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, na Mchungaji Boniface Mwamposa.