Home Habari za michezo MTEGO WA UBINGWA LIGI KUU HUU HAPA….SIMBA AU YANGA MMOJA AKIJIKWA TUU...

MTEGO WA UBINGWA LIGI KUU HUU HAPA….SIMBA AU YANGA MMOJA AKIJIKWA TUU KWISHAA…

Habari za Michezo leo

BAADA ya Yanga kupata ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Tabora United hivi karibuni, hakika mechi saba zilizobaki kwa Simba na Yanga zimewekewa mtego wa ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2024/2025.

Simba haitakuwa na mchezo wowote wa Ligi Kuu kwa mwezi huu wa Aprili, labda kama itatolewa kimataifa na Al Masry, huku kwa upande wa Yanga ikiwa na michezo minne na kati ya hiyo tayari imeshacheza mmoja na kushinda, jambo linaloifanya kuzidisha wigo wa pointi kwa wapinzani wao. Hivyo ili Yanga iwe na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa inatakiwa kuiombea Simba iitupe nje Al Masry ili ratiba ibaki kama ilivyo.

Katika michezo minne ya Yanga, imepata pointi tatu za Tabora United ikiwa ni kisasi baada ya mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam, kikosi hicho kuchapwa mabao 3-1, Novemba 7, 2024.

Kitendo cha Yanga kushinda mchezo huo, kimeifanya kufikisha pointi zake 61, baada ya kucheza michezo 23, nyuma ya Simba iliyopo nafasi ya pili na pointi 57, ila ikiwa na mechi 22 tofauti ya moja na washindani wao katika msimamo wa Ligi Kuu. Simba haitokuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara hadi Mei 2, mwaka huu itakapoikaribisha Mashujaa FC kutoka Kigoma, huku kwa upande wa Yanga ikiwa na mechi tatu, kabla ya miamba hiyo kupisha ratiba ya Kombe la Muungano itakayoanza Aprili 21 hadi 27.

Ukiacha mchezo wa Yanga dhidi ya Coastal Union na Yanga dhidi ya Azam, ambayo itakuwa karibukaribu, Yanga itapumzika kwa zaidi ya wiki moja kabla haijavaana na Fountain Gate na hivyo kuwa na wigo mpana wa kujiandaa. Yanga itacheza na Coastal Union Aprili 7, kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, huku ikiwa na kumbukumbu ya nzuri kushinda raundi ya kwanza bao 1-0, mchezo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Oktoba 26, 2024.

Baada ya hapo, Yanga itacheza na Azam FC Aprili 10, safari hii ikiwa ugenini huku ikihitaji kulipa kisasi pia, kufuatia mchezo wa kwanza kuchapwa kwa bao 1-0, Novemba 2, 2024. Mchezo wa mwisho kwa Yanga wa Ligi Kuu Bara kwa mwezi huu, utakuwa ni Aprili 20, ambapo itasafiri kuifuata Fountain Gate kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Manyara, huku mechi ya kwanza ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mabao 5-0, Desemba 29, 2024.

Ikiwa Yanga itashinda michezo yote mitatu ijayo, itafikisha pointi 70, huku Simba ikiendelea kusalia na pointi 57 tofauti ya pointi 13, jambo litakalozidisha presha zaidi kwa kikosi hicho cha Msimbazi kinachosaka ubingwa huo baada ya kuukosa kwa misimu mitatu.

Hii ina maana kuwa Simba itacheza zaidi ya michezo minne mfululizo kila baada ya siku tatu bila Yanga ambayo inawania nayo ubingwa kucheza mchezo wowote. Huu ni mtego mkubwa kiufundi ambao unahitaji si pumzi tu bali hesabu,maarifa makubwa.

Ratiba kwa Mei, itakuwa ngumu kwa miamba hii yote miwili katika kusaka tiketi ya ubingwa lakini hatari zaidi kwa Simba, kwani kabla ya michezo yao na timu zingine, ila kuna mchezo wa wenyewe kwa wenyewe, ambao haukuchezwa mwanzoni baada ya kuota mbawa Machi 8, 2025.

Katika michezo ya Yanga kwa mwezi Mei, ratiba inaonyesha timu zote ilizocheza nazo imeshinda raundi ya kwanza, hivyo kuzidisha presha zaidi kwa wapinzani wao Simba, japo haina maana inaweza kushinda kirahisi kutokana na ushindani uliopo dakika za lala salama.

Yanga itacheza na Namungo FC, ambayo mechi ya kwanza ilishinda mabao 2-0, Novemba 30, 2024, kisha kusafiri hadi jijini Mbeya kucheza na Tanzania Prisons Mei 21, huku ikiwa na kumbukumbuku nzuri ilipoichapa mabao 4-0, Desemba 22, 2024.

Baada ya hapo, itacheza na Dodoma Jiji Mei 25, huku mechi ya kwanza zilipokutana ilishinda mabao 4-0, Desemba 25, 2024, kisha kusubiria ratiba dhidi ya Simba ambayo haikuchezwa Machi 8, 2025, huku ikiibuka kidedea bao 1-0, Oktoba 19, 2024, hapa Yanga itakuwa imemaliza mziki wake. Kwa upande wa Simba itakuwa bize. Itakiwasha na Mashujaa Mei 2, Mchezo wa raundi ya kwanza, Simba iliichapa Mashujaa bao 1-0, Novemba 1, 2024. JKT itacheza nao Mei 5, yaani siku tatu tu mbele.

Kumbuka mchezo wa kwanza ilishinda bao 1-0, siku tatu mbele itaikaribisha Pamba KMC Complex.

Mechi ya kwanza Simba iliifunga Pamba bao 1-0, Novemba 22, 2024. Siku tatu mbele Simba itakuwa tena nyumbani kuivaa KMC, siku tatu tena mbele, itacheza mchezo mgumu dhidi ya Singida Black Stars yaani Mei 14, 2025, baada ya hapo itapumzika siku tatu na kwenda kwa vibonde KenGold ugenini.

Kutoka hapo ratiba inaonyesha kuwa Simba itamaliza mechi zake siku nne mbele dhidi ya Kagera Sugar iliyoichapa 5-2, Desemba 21, 2024, hapa katikati kunaweza kuwa na mchezo wa kiporo dhidi ya watani wao Yanga. Atakayechanga karata vizuri atakuwa na nafasi nzuri ya ubingwa.

SOMA NA HII  YANGA YAZIPIKU SIMBA, AZAM FC UPIGAJI MASHUTI...YASUBIRI TUZO ZA TFF