KOCHA Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema kuandaa kikosi ili kuikabili Yanga sio kazi rahisi, huku akidai kuwa wapinzani wao walikuwa bora zaidi ndio maana walishinda mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.
Taoussi alisema hayo muda mfupi baada ya kupokea kichapo hicho kilichozidi kuiweka pabaya timu hiyo katika kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, kwani imesalia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 51 – moja zaidi na ilizonazo Singida Black Stars inayoshika nafasi ya nne.
Azam kama ilivyo kwa Singida kila moja imesaliwa na mechi nne kufunga msimu zikiwania kumaliza nafasi ya tatu ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika..
Akizungumza baada ya mechi hiyo, alisema Yanga walikuwa bora kila eneo huku wao wakikosa nguvu katika maeneo mengi kuanzia beki ya kati na kuwachezesha wachezaji wa timu hiyo baadhi wakiwa hawapo kwenye ubora. “Nawapongeza Yanga walikuwa bora hasa kipindi cha kwanza ambacho wachezaji wangu walifanya makosa mengi hasa eneo la ulinzi kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi akiwemo Yeison Fuentes ambaye ni mzoefu wa dabi,” alisema Taoussi na kuongeza:
‘’Ukiondoa beki huyo nimemtumia Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Pascal Msindo wakiwa na maumivu lakini wamejitahidi kupambana na kuonyesha mchezo mzuri dhidi ya timu yenye wachezaji bora.”
Kocha huyo, aliyeongoza timu hiyo kupoteza mchezo wa pili mfululizo akianza na kichapo cha Singida Black Stars, alisema uchovu wa wachezaji kutoka kucheza mechi ya nguvu na kukutana na timu bora umechangia kupoteza mchezo huo.
Kipigo cha jana usiku kilikuwa cha tano msimu huu kwa Azam ikicheza mechi 26, ushindi 15, sare sita ikifunga mabao 39 huku yenyewe ikifungwa 15.