Home Habari za michezo KUHUSU TAREHE MPYA YA MECHI YA DABI….HUU HAPA MSIMAMO WA SERIKALI…FIFA WATAJWA…..

KUHUSU TAREHE MPYA YA MECHI YA DABI….HUU HAPA MSIMAMO WA SERIKALI…FIFA WATAJWA…..

Habari za Michezo

SAKATA la kuahirishwa kwa dabi ya Kariakoo ya Yanga dhidi ya Simba limechukua sura mpya.

Serikali kupitia Wizara ya Michezo imepanga kukutana na Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu Tanzania ikiwa ni sehemu ya jitihada zake kutafuta maridhiano.

Akizungumza  jijini hapa wakati wa mkutano wa mawaziri na waandishi wa habari kueleza mafanikio ya miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paramagamba Kabudi alisema katika kikao kilichofanyika Machi 27 mwaka huu kati ya wizara hiyo na pande tatu; Yanga, Simba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lengo lilikuwa ni kuwakutanisha wahusika waongee.

“Masuala ya ligi yanasimamiwa na TFF na Bodi ya Ligi na waziri hawezi kuyaingilia kwa mujibu wa Kanuni za FIFA. Tuliwaleta pamoja ili kuanza mchakato wa kufikia maridhiano na maelewano ambayo yatafika kwa wale wenye dhamana ya kisheria na kikanuni kutoa tamko,” alisema.

Waziri Kabudi alisema mechi ya Simba dhidi ya Yanga ni miongoni mwa dabi zenye umaarufu kimataifa na jukumu lake ni kuwaleta pamoja wadau hao wa michezo huku akiwaomba mashabiki na watanzania kuendelea kuwa na subira wakati jambo hilo linashughulikiwa.

Hata hivyo, alisema hatazungumzia kilichofikiwa katika jitihada zao kumaliza mvutano huo kwa kuwa vyombo vinavyohusika, kwa maana ya TFF na Bodi ya Ligi ndio vyenye mamlaka ya kushughulikia.

Alisema anaamini mwafaka utafikiwa na vyombo hivyo vya kusimamia soka vitatoa tamko ya kile kilichokubaliwa.

Mchezo huo wa dabi awali ulipangwa kufanyika Machi 8 mwaka huu lakini Bodi ya Ligi iliuhairisha saa chache kabla ya muda wa mchezo na kutangaza kuwa itaupangia tarehe mpya.

Hiyo ni kutokana na klabu ya Simba kuwasilisha barua ya malalamiko ya kunyimwa haki ya kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa walau siku moja kabla ya mchezo.

Hata hivyo, hatua hiyo ilileta mvutano, klabu ya Yanga ikipinga vikali kuahirishwa kwa mchezo huo na kutoa kauli ya kutokuwa tayari kucheza tena mchezo huo kwa tarehe itakayopangwa. Yanga pia inataka ipewe pointi tatu na magoli matatu kwa kuwa Simba ilisusia mchezo huo kinyume cha taratibu vinginevyo itachukua hatua zaidi ikiwamo kufungua shauri katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

MADUDU KWA MKAPA

Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi alitoa ufafanuzu kuhusu maboresho ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, akisema umefanyiwa matengenezo na kwa sasa uko mbioni kukamilika. Maboresho yatakamilika mwishoni mwa mwezi huu, lakini hayakuhusu kiwanja (pitch).

“Pitch (kiwanja) itafanyiwa kazi baada ya michuano ya CHAN maana haikuwa sehemu ya maboresho ya sasa. Siku ya mechi ya Simba dhidi ya Al-Masry (kiwanja kili haribika) kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na mvua ilipokoma, baada ya nusu saa mechi ilichezwa na kusababisha changamoto ya uwanja. Ndio maana wizara yenyewe ilitangaza kuufunga na kuufanyia marekebisho.

“Hii hatua inalenga kutuwezesha katika mashindano ya sasa hadi CHAN, na baada ya CHAN ile pitch tutaondoa tena na tutatengeneza pitch nyingine kwa ajili ya AFCON,” alisema.

Alisema kuwa hadi sasa viti 40,000 vipya vimeshafungwa, taa 360 zimefungwa, mfumo mpya wa umeme, vyoo vimekarabatiwa na kuimarisha ulinzi kwa kufunga kamera.

Mwanzoni mwa mwaka jana, gazeti la Nipashe lilichapisha ripoti ya uchunguzi kuhusu Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikibainisha kuwa uwanja huo haukujengwa kuwa wa daraja “A” la FIFA, bali ulijengwa rasmi kuwa wa daraja “B”.

Ni kutokana na dosari hiyo, serikali iliamua kutenga Sh. bilioni 31 kwa ajili ya maboresho ili uwanja huo utumike katika mashindano yajao ya CHAN na AFCON, ambayo Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu mwenyeji. Nchi zingine ni majirani Kenya na Uganda.

SOMA NA HII  KISA MAAMUZI HAYA YA CAF KWA SIMBA..IBENGE ANG'AKA ..ABAKI KUKODOA MACHO...AITEGEMEA YANGA..