KAMPUNI ya vifaa vya michezo na viatu, Diadora ya Italia yenye maskani yake mjini Caerano di San Marco imeingia mkataba wa kuitengenezea jezi klabu ya Simba ya Dar es Salaam.
Akizungumza leo Jijini Durban, Afrika Kusini Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jayrutty Investment Limited, Joseph Rwegasira amesema kwamba kuanzia msimu ujao Simba itavaa jezi za Diadora.
“Wakati tunatangazwa kuingia mkataba huu na kutengeneza vifaa vya Simba kuanzia msimu ujao niliahidi. Kutokana na ukubwa wa Simba ni wakati wa kwenda kimataifa,”:
“Na leo tupo makao makuu ya Diadora ukanda wa SADC na kwa mara ya kwanza tunakwenda kutangaza ushiriki wa pamoja kati ya Simba, Jayrutty na Diadora,” amesema Rwegasira.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu Diadora Afrika Kusini, Yusuf Vadi amesema kwamba ameahidi kutumia fursa hiyo kuendelea kuutangaza ubora wao katika utoaji wa vifaa bora vya michezo.
“Tumefurahi kupata nafasi hii ya kuwa sehemu ya udhamini wa miongoni mwa klabu kubwa Afrika na tunahidi kwenda kutengeneza bidhaa bora kama ilivyokuwa kwa timu tulizowahi kuzivalisha kwa muda mrefu ikiwemo AS Roma ya Italia,” amesema Vadi.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana amesema kwamba Simba kupata jezi na vifaa vingine bora kutoka kwenye kampuni kubwa ulimwenguni kama Diadora ni kuashiria kuendelea kukuwa kwake kama klabu na kujitangaza ulimwenguni kote.
Akizungumza pia kwenye Mkutano huo maalum wa kutangaza dili hilo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma amesema kwamba ameipongeza Jayrutty Investment Limited kwa kuanza mapema mno kutekeleza mkataba wake na Simba SC.
“Nimekuja nikiwa na furaha kushuhudia utekelezaji wa mkataba kati ya Simba na Jeyrutty walioingia wiki mbili zilizopita nikiwa mgeni rasmi na nimeshangazwa na jambo hili kutekelezwa kwa haraka kama ilivyoahidiwa. Hongera sana Jayrutty kwa kuanza mapema utekelezaji.”
“Nimekuja kuiwakilisha serikali hapa Afrika Kusini kwa ajili ya kuendelea kuwapa ushirikiano Klabu ya Simba kuhakikisha wanacheza wanafanya vizuri kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili na kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).”
“Niwatakie kila la kheri na ushindi mnono kwenye mechi ya Jumapili ambayo itachezwa kule Durban na katika kipindi cha hivi karibuni hakuna timu inatamani kukutana na Simba na serikali imewapa ushirikiano mkubwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.”- Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma.
Jayrutty Investment Limited ilitambulishwa kuwa mshindi wa Tenda ya Usambazaji jezi za Simba SC kwa mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Sh. Bilioni 38.1 (Sh. 8,120,400,000).