Home Habari za michezo YA MWAKA 93 KUJIRUDIA SIMBA…? HIZI HAPA DK 90 ZA SAUZI ZILIVYOUA...

YA MWAKA 93 KUJIRUDIA SIMBA…? HIZI HAPA DK 90 ZA SAUZI ZILIVYOUA HISTORIA YA YANGA….

Habari za Simba leo

KLABU ya Simba ya Tanzania imeandika historia mpya baada ya kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya pili katika historia yao.

Simba imefuzu baada ya kutoka sare tasa (0-0) dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa katika Uwanja wa Moses Mabhida, mjini Durban, Afrika Kusini.

Simba imetinga hatua hiyo kwa faida ya ushindi wa bao 1-0 walioupata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Bao hilo muhimu lilifungwa na kiungo wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Jean Charles Ahoua, ambaye aliiongoza timu yake kuibuka na ushindi huo wa nyumbani.

Katika mchezo wa marudiano, timu zote zilicheza kwa nidhamu kubwa ya kiufundi, huku kipindi cha kwanza kikiisha bila timu yoyote kufunga bao. Stellenbosch walijaribu kusukuma mashambulizi wakitafuta bao la kusawazisha matokeo ya jumla, lakini ukuta wa Simba uliokuwa imara uliwazuia.

Kwa mafanikio haya, Simba inayonolewa na kocha raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids, imefuzu kucheza fainali ya mashindano ya CAF kwa mara ya pili baada ya miaka 32. Mara ya mwisho Simba walicheza fainali ya mashindano ya CAF mwaka 1993, katika Kombe la CAF (CAF Cup) dhidi ya Stella Adjame kutoka Ivory Coast.

Katika fainali ijayo, Simba itakutana na mshindi kati ya RS Berkane ya Morocco na CS Constantine ya Algeria, ambao walitarajiwa kumenyana katika mchezo wa pili wa nusu fainali usiku wa kuamkia leo.

Simba sasa wana nafasi ya kipekee kuandika historia mpya kwa kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kushinda Kombe la Shirikisho Afrika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004, ikiwa watafanikiwa kunyanyua taji hilo.

SOMA NA HII  SELEMAN MATOLA: KAZI BADO INAENDELEA