Home Habari za michezo BAADA YA CAS ‘KUWABANIA’…HII HAPA ‘TURN OUT’ YA KIBABE YA YANGA KUHUSU...

BAADA YA CAS ‘KUWABANIA’…HII HAPA ‘TURN OUT’ YA KIBABE YA YANGA KUHUSU MECHI NA SIMBA

Habari za michezo

KLABU ya Yanga imetangaza rasmi  Jumatatu hii kutoshiriki mechi yao dhidi ya watani wa jadi Simba SC, ikiwa ni sehemu ya kupinga kile walichokiita “dhulma na uvunjwaji mkubwa wa kanuni” katika uendeshaji wa soka nchini.

Taarifa rasmi iliyotolewa kwa umma, Yanga imethibitisha kuwa imepokea majibu kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kuhusu kesi yao namba CAS 2025/A/11298, ambapo walielekezwa kurejea kwanza kwenye kamati za ndani za soka kabla ya hatua ya rufaa.

Hata hivyo, Yanga imesema haina imani na kamati hizo kutokana na kile ilichokitaja kuwa ni uonevu na upendeleo wa wazi kwa baadhi ya timu.

“Kutokana na uonevu, uvunjwaji mkubwa wa kanuni na upendeleo wa dhahiri kwa baadhi ya timu unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka Tanzania, uongozi wa Young Africans Sports Club hauna imani na hauko tayari kupeleka shauri hilo kwenye mamlaka ambazo zinatenda dhulma,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Kuhusiana na mchezo dhidi ya Simba SC, ambao ni mechi namba 184 ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Yanga imesisitiza:

“Msimamo wa klabu yetu juu ya mchezo namba 184 wa Ligi Kuu msimu huu uko palepale kuwa hatutashiriki kwenye mchezo huo kwa namna yoyote ile.”

Taarifa hiyo pia imewahakikishia mashabiki kuwa klabu hiyo ipo tayari kupambana kwa njia zote kuhakikisha haki inapatikana.

“Wanayanga wote, watakuwa tayari kuipambania haki yao kivyovyote vile ili kukomesha dhulma na uvunjwaji mkubwa wa kikanuni unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka kwa maslahi mapana ya maendeleo ya soka nchini.”

SOMA NA HII  BAADA YA KIMYA KIREFU....MWAKALEBELA AIBUKA NA JIPYA NDANI YA YANGA...ATAJA HUJUMA