Home Habari za michezo SIMBA:- UBINGWA WETU CAF TUNAMPA RASI MWINYI…..

SIMBA:- UBINGWA WETU CAF TUNAMPA RASI MWINYI…..

Habari za Simba leo

KATIKA hekaheka za maandalizi kuelekea mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, klabu ya Simba imedhihirisha dhamira yake ya dhati kuhakikisha historia haijirudii. Ni dhamira iliyojaa heshima, kumbukumbu na kiu ya mafanikio ambayo yamecheleweshwa kwa zaidi ya miongo mitatu.

Mnamo mwaka 1993, Simba ilifika hatua ya fainali ya mashindano ya Afrika, na mgeni rasmi katika mchezo huo alikuwa Hayati Ali Hassan Mwinyi, Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania Bara. Lakini, kama ilivyoandikwa katika historia, Simba walishindwa kunyakua ubingwa huo mbele ya macho ya kiongozi huyo, jambo lililowaumiza mashabiki wengi, hasa kutokana na heshima waliyotaka kumpa kiongozi wao kupitia ushindi.

Miaka 32 baadaye, historia inaandika ukurasa mwingine. Simba imetinga tena fainali, safari hii wakikabiliana na RS Berkane ya Morocco. Wanalazimika kushinda kwa mabao 3-0 ili kulibakisha kombe hilo nyumbani. Mchezo huo wa marudiano utafanyika Jumapili, Mei 25, 2025, Uwanja mpya wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Katika kuonesha uzito wa mchezo huo, uongozi wa Simba ulifanya dua maalum walipotembelea kaburi la Hayati Ali Hassan Mwinyi lililopo Manga Pwani, Visiwani Zanzibar. Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema:

“Tunakumbuka mwaka 1993, Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi alikuwa mgeni rasmi lakini hatukufanikiwa kumpa zawadi ya ubingwa. Leo, miaka imepita na mtoto wake, Rais Hussein Mwinyi, atakuwa sehemu ya mashuhuda wa fainali nyingine. Kwa mapenzi ya Mungu, tunalenga kumpa kile ambacho baba yake hakukipata ubingwa wa Afrika.”

Kauli hii si tu inagusa hisia za kihistoria, bali pia inawasha moto wa matumaini kwa mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla. zaidi ya mpira ni kizazi kimoja kikikamilisha ndoto ya kingine.

SOMA NA HII  BEKI WA SIMBA SHOMARI KAPOMBE "MECHI NA RAJA CASABLANCA...NI MAZOEZI TU