Home Habari za michezo AFRIKA KUSINI USO KWA USO NA TAIFA STAR….NGOMA KUCHEZWA UGENINI…

AFRIKA KUSINI USO KWA USO NA TAIFA STAR….NGOMA KUCHEZWA UGENINI…

Taifa Stars

Timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itacheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’, Juni 6, mwaka huu huko Afrika Kusini.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa katika Uwanja wa Peter Mokaba uliopo Polokwane, Afrika Kusini kuanzia saa 1:30 usiku kwa muda wa huko sawa na saa 2:30 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.

Hilo limefahamika kupitia taarifa iliyotolewa na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) baada ya kocha wa Bafana Bafana, Hugo Broos kutangaza kikosi cha wachezaji 41 kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo.

“Timu itaripoti kambini Johannesburg Jumapili, Juni Mosi, 2025 na baada ya hapo itasafiri hadi Polokwane siku hiyohiyo.

“Wachezaji wa Mamelodi Sundowns hawajachaguliwa kwa sababu watakuwa wakishiriki kwenye Kombe la Dunia la klabu la FIFA litakalochezwa Marekani kuanzia Juni 14 hadi Julai 13, 2025,” imefafanua taarifa hiyo ya SAFA.

Kwa mujibu wa SAFA, kikosi hicho cha wachezaji 41 wa Bafana Bafana kitapunguzwa na kubakiwa na wachezaji 23.

Kikosi cha Afrika Kusini kilichoitwa kinaundwa na kundi kubwa la wachezaji wanaocheza katika timu za Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL) ambao wataongezewa nguvu na wachache wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo.

Ni wachezaji sita tu wanaocheza soka la kulipwa nje ya Afrika Kusini waliojumuishwa katika kikosi hicho cha Bafana Bafana wakiongozwa na Mihlali Mayambela anayeitumikia Aris Limassol ya Cyprus.

Pia kuna Siyabonga Ngezana (FCSB), Samukelo Kabini (Molde), Luke le Roux (Varnamo) Bongokuhle Hlongwane (FC Minnesota) na Shandre Campbell (Club Brugge).

Nyota 41 wanaounda kikosi hicho ni Darren Johnson, Sinoxolo Kwayiba (Chippa United), Sipho Chaine, Nkosinathi Sibisi, Mbekezeli Mbokazi, Deano Van Rooyen, Simphiwe Selepe, Thalente Mbatha, Evidence Makgopa, Patrick Maswanganyi, Tshegofatso Mabasa, Relebohle Mofokeng na Mohau Nkota wanaochezea Orlando Pirates.

Kuna Bruce Bvuma, Yusuf Maart na Mduduzi Shabalala (Kaizer Chiefs), Ricardo Goss, Sydney Mobbie, Ime Okon na Gape Moralo (Supersport United) na kutokea Stellenbosch ni Thabo Moloisane, Fawaaz Basadien na Devin Titus.

Wapo Khuluman Ndamane, Puso Dithejane na Kamogelo Sebelebele wa TS Galaxy, Renaldo Leaner, Vuyo Letlapa na Siphesihle Mkhize (Sekhukhune), Keagan Allan na Fezile Gcaba (Richards Bay), Ndamulelo Maphangule na Oswin Appollis wanaoichezea Polokwane City.

Wengine ni Yanela Mbuthuma na Tshepang Moremi wa Amazulu na kuna Mayambela, Shandle Campbell, Hlongwane, Le Roux, Kabini na Ngezana.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA WAARABU...HIVI NDIVYO MABOSI WA YANGA WALIVYOTUA ALGERIA KININJA..