Home Habari za michezo HIVI NDIVYO YANGA WALIVYOFUNGA MSIMU KIBABE JANA MBELE YA SINGIDA BS….

HIVI NDIVYO YANGA WALIVYOFUNGA MSIMU KIBABE JANA MBELE YA SINGIDA BS….

Habari za Yanga leo

DUKE Abuya na Clement Mzize, wamekata kiu ya mashabiki wa Yanga baada ya kufanikisha kutwaa Kombe la Shirikisho (FA) katika mchezo wa fainali uliofanyikwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Nyota hao wawili ndio waliotikisa nyavu za Singida Black Stars katika ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Yanga.

Abuya alikuwa wa kwanza kufunga bao dakika ya 39 akimalizia mpira uliookolewa na kipa Amas Obasogie kufuatia krosi ya Israel Mwenda. Kwa Duke, ni bao la tatu msimu huu kwenye michuano hiyo.

Bao hilo liliamsha mashambulizi zaidi ya Yanga ambapo muda mfupi baada ya Singida Black Stars kuanzisha mpira kati, wakashambuliwa tena lakini Clement Mzize hakutumia vizuri shambulizi hilo na mpira kutoka nje, likawa pigo la kona, halikuzaa matunda.

Kipindi cha kwanza kilikuwa na mvutano wa hapa na pale huku eneo la katikati kukiwa na vita kubwa kutoka kwa viungo wa Yanga, Khalid Aucho na Duke Abuya dhidi ya wale wa Singida Black Stars, Mohamed Damaro na Morice Chukwu.

Muda mfupi kabla ya kwenda mapumziko, kipa wa Yanga, Djigui Diarra aliokoa mashambulizi mawili ya haraka kutoka kwa Jonathan Sowah na Ande Koffi na kuifanya Yanga kwenda kupumzika ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma, aliona mpango wake wa kipindi cha kwanza haukufanikiwa, akafanya mabadiliko ya haraka wakati kipindi cha pili kinataka kuanza akiwatoa Gadiel Michael na Marouf Tchakei, wakaingia Ibrahim Imoro na Edmund John.

Mabadiliko hayo hayakuwa na faida kwa Singida Black Stars kwani ilijikuta ikiruhusu bao la pili dakika ya 50 likifungwa na Mzize ambaye alimalizia pasi ya Maxi Nzengeli. Hilo ni bao la pili kwa Mzize msimu huu.

Katika kipindi hicho cha pili, Yanga ilifanya mashambulizi kadhaa lakini umakini hafifu wa nyota wa kikosi hicho wakashindwa kuongeza mabao.

Hata hivyo, Mzize na Pacome Zouzoua, watakuwa wanajiuliza muda wote kufuatia kukutana na ulinzi mkali wa beki wa kulia wa Singida Black Stars, Ande Koffi ambaye aliwadhibiti kwa nyakati tofauti kila walipokwenda upande wake.

Kutokana na faulo za hapa na pale zilizokuwa zikifanyika, mwamuzi Ahmed Arajiga hakusita kuwaonyesha wachezaji kadi za njano akiwemo Duke Abuya, Khalid Aucho, huku dakika ya 86 Jonathan Sowah wa Singida Black Stars akionyeshwa kadi ya pili ya njano kisha nyekundu.

Ushindi huo unaifanya Yanga kutetea ubingwa wa michuano hiyo na kubeba mara ya nne mfululizo kama ilivyokuwa Ligi Kuu Bara. Pia ni mara ya tano tangu michuano hiyo iliporejea msimu wa 2015-2016 ikiwa ndiyo timu iliyotwaa mara nyingi zaidi.

Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, ametangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo na kupewa hundi ya Sh2 milioni.

SOMA NA HII  ULAYA NI ULAYA TU....WAFANYAKAZI REAL MADRID WAPEWA NDINGA MPYAA...GARI MOJA BIL 3...