KIKOSI cha Yanga usiku wa jana kilikuwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar kumalizana na Singida Black Stars katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho, ikiwa ni siku chache tu tangu itoke kubeba taji la Ligi Kuu lililochangiwa kwa kiasi kikubwa na watani wao, Simba.
Ndio, Yanga ilitwaa ubingwa huo wa Ligi kwa msimu wa nne mfululizo baada ya kuilaza Simba kwa mabao 2-0 katika mechi ya kiporo cha Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Jumatano kwenye Uwanja wa Mkapa baada ya kuahirishwa mara mbili Machi 8 na Juni 15.
Mabao ya Pacome Zouzoua la penalti na jingine la Clement Mzize yaliifanya Yanga kumaliza mbabe wa ligi kwa kukusanya jumla ya pointi 82 kupitia mechi 30, ikishinda 27, sare moja na kupoteza mbili, ikifunga mabao 83 na kufungwa 10.
Ubingwa huo wa Yanga katika Ligi Kuu umechangiwa na klabu 12 zilizokubali kufungwa nje ndani, ikiwamo Simba, huku klabu za JKT Tanzania, Azam na Tabora United ndio timu pekee zilizoichangia timu hiyo pointi chache.
Simba iliyomaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha klabu 16, ni moja ya timu 12 zilizoipa Yanga pointi sita kutokana na kufungwa nje ndani mbele ya wababe hao waliotwaa taji la 31 tangu kuanzishwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965.
Simba ilianza kugawa pointi Oktoba 19 mwaka jana ilipojifunga bao na kuipa Yanga ushindi wa pointi tatu na bao moja, kisha kurudia tena Jumatano iliyopita kwa kulala 2-0 na kukamilisha pointi sita na mabao matatu iliyoizawadia Yanga katika ubingwa wao.
Timu nyingine zilizogawa pointi sita na mabao yao kwenye mabano ni, Tanzania Prisons, Fountain Gate na Dodoma Jiji zilizoongoza kwa kugawa mabao mengi (9), Mashujaa (8), KMC, Pamba Jiji na Kengold (7), Kagera Sugar (6), Namungo (5), Singida BS (3) na Coastal Union (2).
Tabora United na Azam FC ndizo zilizokuwa timu zilizogawa pointi chache msimu huu kwa Yanga baada ya kupoteza mechi moja na kushinda moja, hata hivyo Nyuki wa Tabora wameipa Yanga mabao manne, japo wenyewe walivuna matatu. Timu hiyo ilianza kwa kushinda 3-1 kabla ya kukubali kichapo 3-0 ziliporudiana.
Azam imegawa mabao mawili na kuvuna mawili pia, baada ya kushinda 1-0 katika mechi ya kwanza na kulala 2-1 ziliporudiana, huku JKT Tanzania ikigawa pointi nne baada ya kulala 2-0 mechi ya awali na kutoka suluhu ziliporudiana.
Hii ina maana Azam na Tabora ndizo zilizovuna pointi tatu mbele ya Yanga, wakati JKT iliambulia moja ikiwa ni zaidi kuliko hata Simba na klabu nyingine 11 zilizopasuka nje ndani, huku Clement Mzize akiwa kinara wa kugawa dozi kwa timu pinzani kwa kufunga jumla ya mabao 14, akifuatiwa na Prince Dube aliyefunga 13.
Pacome Zouzoua anafuata kwa kuzitungua timu pinzani zilizokutana na Yanga kwa kufunga 12 akifuatiwa na Stephane Aziz KI aliyeuzwa Wydad AC akifunga mabao tisa, huku Clatous Chama na Maxi Nzengeli kila mmoja akifunga sita na beki Ibrahim Bacca akifuata akiwa na matano akiwa beki kinara kwa Yanga kufunga mabao mengi.
Bacca anashika nafasi ya pili sambamba na Erasto Nyoni (Namungo) kwa mabeki nyuma ya kinara Lusajo Mwaikenda wa Azam FC (6).