Home Habari za michezo ZA NDAAAANIII KABISA…..SIKU ZA MPANZU SIMBA ZAHESABIKA….TIMU ULAYA YAMFUNGIA KAZI…

ZA NDAAAANIII KABISA…..SIKU ZA MPANZU SIMBA ZAHESABIKA….TIMU ULAYA YAMFUNGIA KAZI…

Habari za Simba leo

WAKATI mashabiki na wapenzi wa Simba wakiendelea kujiuliza kilichowakuta katika pambano la Dabi ya Kariakoo kwa kulazwa mabao 2-0 na Yanga, kuna taarifa ya kushtua ambayo huenda wasingependa kuisikia kuhusu kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Ellie Mpanzu.

Mpanzu ambaye ameibuka kuwa kipenzi cha mashabiki wa klabu hiyo kwa siku za hivi karibuni, inadaiwa anahesabu siku klabuni hapo kutokana na kunyemelewa na klabu tatu tofauti za Ulaya zilizoonyesha nia ya kumbeba kwa kiwango alichokionyesha msimu huu uliomalizika kwa Simba kutoka kapa Bara.

Vyanzo mbalimbali vimeripoti nyota huyo kwa sasa anahitajika na Brest FC inayoshiriki Ligue 1 ya Ufaransa, KRC Genk ya Ubelgiji, sambamba na Malmo FF ya Sweden zilizoripotiwa kuvutiwa naye na zimeanza harakati za kuinasa saini yake.

Mpanzu aliyetambulishwa Simba, Septemba 30, 2024, akitokea AS Vita Club ya kwao DR Congo, aliichezea timu hiyo katika dirisha dogo la Januari 2025, baada ya kuchelewa kutokana na usajili kufungwa Agosti 15, tangu ulipofunguliwa Juni 15, 2024.

Katika miezi sita tu aliyoichezea timu hiyo, nyota huyo ameonyesha uwezo mkubwa na kuanza kuzivutia timu hizo za Ulaya zinazohitaji saini yake, ingawa inatambulika wazi kuwa Mpanzu ni miongoni mwa wachezaji wanaopambaniwa kubakizwa kikosini.

Taarifa zinasema kuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids anavutiwa na uwezo wa mchezaji huyo kwa ajili ya kubaki msimu ujao, ingawa hadi sasa hakuna uamuzi rasmi uliofanyika kuhusiana na watakaobakia au kuondoka.

“Licha ya mkataba alionao hata kocha mwenyewe bado hajajua hatima yake kama atabaki au ataondoka hivyo, bado ni mapema kuzungumzia hilo, ingawa nafikiria kuanzia Julai tutaanza kujua mustakabali wao kwa wote,” kilisema chanzo hicho.

Sababu kubwa zilizoelezwa klabu hizo za Ulaya kuvutiwa na mchezaji huyo, ni kutokana na kiwango kizuri alichokionyesha pia hasa katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwa sababu maskauti mbalimbali walikuwa wakimfuatilia.

Katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024-25, Mpanzu alifunga bao moja na kuasisti mawili na kuiwezesha Simba kufika hadi fainali ya CAF, ikiwa ni kwa mara ya kwanza baada ya miaka 32, tangu ilipocheza mwaka 1993.

Fainali ya msimu huu wa 2024-25, Simba ilikosa ubingwa mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa kufungwa jumla ya mabao 3-1, ikichapwa ugenini 2-0, Mei 17, 2025, kisha kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ikatoka sare ya bao 1-1, Mei 25, 2025.

Katika Ligi Kuu iliyofikia tamati Juni 25, 2025, Mpanzu alichangia mabao 10 ya Simba kati ya 69, yaliyofungwa na kikosi hicho kizima, baada ya kufunga manne na kuasisti sita, akiisaidia kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 78.

Simba ilimaliza nafasi ya pili baada ya kufungwa mabao 2-0 na Yanga katika mechi ya kuamua bingwa, ambapo kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani kilitwaa taji la nne mfululizo la Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 82.

SOMA NA HII  MABINGWA WATETEZI WA KOMBE LA SHIRIKISHO KUKUTANA NA AFRICAN LYON