Home Habari za michezo BAADA YA KUMALIZANA NA BALLA CONTE….MASHINE HIZI ZA KAZI KUFUATIA YANGA….

BAADA YA KUMALIZANA NA BALLA CONTE….MASHINE HIZI ZA KAZI KUFUATIA YANGA….

Habari za Yanga leo

VURUGU walizoanza nazo mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga katika kutangaza majembe mapya, zimeanza kushtua.

Hiyo ni baada ya kumtambulisha kiungo Moussa Balla Conte, raia wa Guinea ambaye pia watani wao wa jadi, Simba walikuwa wakimpigia hesabu kali.

Kabla ya Conte, Yanga ulimalizana na mshambuliaji Celestin Ecua kutoka Zoman ya Ivory Coast ambaye utambulisho wake bado haujafanyika lakini dili limekamilika.

Sasa unaambiwa baada ya hapo, kuna mashine nyingine tatu zipo kwenye hatua nzuri kukamilisha usajili ndani ya Yanga, kisha nazo zitambulishwe kabla ya Julai 26 mwaka huu kikosi hicho kucheza mechi moja ya kirafiki jijini Dar.

Inaelezwa kwamba, mazungumzo ya viongozi wa Yanga na mashine hizo tatu ambazo ni winga Edmund Godfrey John, beki wa kati Kevin Mondeko na kiungo mkabaji Mohamed Damaro, yapo kwenye asilimia kubwa kufikia makubaliano mazuri, hivyo kama hakutakuwa na mabadiliko, basi utambulisho wao utafanyika siku chache zijazo.

Mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya Yanga, amesema kuwa, kinachofanyika sasa ni kushusha majembe ambayo ni sehemu ya ripoti ya maboresho ya kikosi iliyoachwa na benchi la ufundi baada ya msimu wa 2024-2025 kumalizika, lakini pia ni mapendekezo ya kocha mpya.

“Utambulisho wa Conte ni sehemu ya kuonyesha uongozi wa Yanga hautaki maneno mengi, bali ni vitendo tu. Hivyo mashabiki wanatakiwa kutulia, kuna mashine nyingine zinakuja,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Kwa sasa kuna mazungumzo yanaendelea na yamefikia pazuri yakiwahusu wachezaji watatu, kuna Edmund John ambaye ni winga wa Singida Black Stars, pia kiungo mkabaji wa timu hiyo, Mohamed Damaro.

“Mwingine ni beki wa kati raia wa DR Congo, Kevin Mondeko aliyemaliza mkataba na USM Alger na tayari klabu yake imemuaga huku yeye pia akiwaaga viongozi na mashabiki wa timu hiyo.”

Damaro amekuwa akihusishwa na Yanga kwa muda mrefu ili kwenda kuongeza nguvu eneo hilo ambapo tayari Conte ametua, huku Khalid Aucho akitajwa kuondoka. Pia kuna Duke Abuya na Mudathir Yahya wanaocheza kikosi cha kwanza.

Kwa sasa nyota huyo yupo nchini kwao Guinea kwa ajili ya mapumziko, lakini ameonekana akifanya mazoezi ya nguvu akiwa amevaa jezi ya Yanga, jambo lililotafsiriwa ni kama shughuli imeisha tayari.

Ikumbukwe kuwa, kiungo huyo ni kati ya nyota watatu wa Singida Black Stars waliobadilisha uraia Januari mwaka huu na kuwa Watanzania sambamba na Emmanuel Keyekeh (Ghana) na Josaphat Arthur Bada (Ivory Coast), hivyo usajili wa Damaro ndani ya Yanga utatambulika kama mchezaji mzawa na sio wa kimataifa.

Kwa upande wa Mondeko raia wa DR Congo mwenye umri wa miaka 29, kabla ya kutua USM Alger akicheza kwa msimu mmoja tu, alikuwa TP Mazembe tangu mwaka 2016 aliyojiunga nayo akitokea RC Kinshasa.

Beki huyo mwenye uwezo pia wa kucheza kulia, msimu wa 2016-17 alishinda Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na TP Mazembe, pia msimu uliomalizika 2024-2025 alishinda Kombe la Algeria na kikosi cha USM Alger.

Msimu wa 2022-2023 ambao Yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, beki huyo alikutana na kikosi hicho Februari 19, 2023 akiwa TP Mazembe ambapo dakika tisini alizocheza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar, alishuhudia wakiondoka na kichapo cha mabao 3-1.

Mondeko anatajwa kwenda kuongeza nguvu kwenye beki wa kati kufuatia nahodha Bakari Mwamnyeto kuonekana kushindwa kutoa upinzani mkubwa kwa Ibrahim Bacca na Dickson Job wanaocheza zaidi kikosi cha kwanza.

Naye Edmund John anayecheza katika wingi zote kulia na kushoto ambapo alifanya vizuri akiwa na Geita Gold kabla ya msimu wa 2024-2025 kutua Singida Black Stars, ni sehemu ya kuboresha kikosi baada ya mawinga wazawa waliopo, Farid Mussa na Denis Nkane kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

SOMA NA HII  YANGA: MASHABIKI VIMBENI, BADO TUPO IMARA