Home Habari za michezo OHHH…HUKO SIMBA MAMBO NI BADO KUMBE…VYUMA HIVI KUTUA KIMAFIA…

OHHH…HUKO SIMBA MAMBO NI BADO KUMBE…VYUMA HIVI KUTUA KIMAFIA…

Habari za Simba leo

KLABU ya Simba imeonekana safari hii haina masihara kwenye usajili baada ya kubainisha kuwa inatarajia kuwatangaza wachezaji wengine wapya watatu wa kigeni ambao watafunga masuala ya usajili kuelekea msimu ujao wa mashindano.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema wachezaji ambao itawatangaza si kama inamalizia zoezi la usajili, la hasha, bali imeshafanya hivyo na imeshapata vibali pamoja na Hati za Uhamisho wa Kimataifa, ITC.

“Hawa tuliowatangaza ambao kila mmoja anawafahamu hawajatosha bado kuna vyuma vitatu hatujavitambulisha, safari hii hatutaki mchezo,” alisema Ahmed.

Alisema wameshamaliza usajili wa wachezaji wote wa kigeni kwani mwisho wa usajili kwa nyota hao ilikuwa ni Agosti 15, mwaka huu.

“Tumemaliza usajili wa wachezaji wote wa kimataifa, tumepata vibali vyao pamoja na ITC zao na tayari dirisha la usajili la wachezaji wa nje ya nchi limeshafungwa tangu Agosti 15.

Hata wale ambao bado hatujawatangaza nao tumeshamaliza vibali na ITC zao ina maana ni wachezaji halali wa Simba tunasubiri wakati tu tulioupanga ili tuwatambulishe.

Kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wachezaji baada ya kufanya usajili huo, Ahmed alikiri na kusema kwa sasa wapo kwenye harakati za kuhakikisha baadhi ya wachezaji hasa wa kigeni wanaondoka na kuwapisha wengine wanaoingia.

“Ni kweli zipo dalili zote za baadhi ya wachezaji wa kimataifa tuliokuwa nao, kuachana nao, tunaangalia nani tutaachana nao kwa wema ili nafasi zichukuliwe na hawa tuliowaongeza na hicho ndicho kinasababisha tuchelewe kuwatangaza, kila kitu kikikamilika tutawatangazia,” alisema Ahmed.

Mchezaji anayefahamika na wanachama na mashabiki wa Simba ambaye bado hajatangazwa rasmi ni Neo Maema, aliyesajiliwa kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Kiungo mshambuliaji huyo yupo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Afrika Kusini kinachoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), inayoendelea hapa nchini, Kenya na Uganda.

Taarifa zinaeleza kuwa, Simba itamtangaza mchezaji huyo mara baada ya kumalizika kwa michuano ya CHAN.

Kuhusu tetesi za kumsajili straika Selemani Mwalimu wa Wydad Casablanca, Ahmed alisema bado halijafika mikononi mwake, lakini akikiri kuwa awali Kocha Mkuu, Fadlu Davids, alikuwa akimhitaji mchezaji huyo wa Kitanzania aliyekuwa akiichezea Fountain Gate.

“Sijapewa taarifa yake, inawezekana lipo, lakini halijafika kwenye meza yangu, ninachojua ni kwamba Kocha Mkuu, Fadlu Davids, aliulizia upatikanaji wake hasa baada ya kuonesha kiwango bora kwenye michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia lililomalizika hivi karibuni nchini Marekani, lakini wenyewe walikataa, kama limerudi tena litakuwapo, basi tutarudi tena kuwaambia,” alisema.

Imetajwa kuwa Simba iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa straika huyo

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo na vyanzo vingine vya nje ya nchi zinaeleza huenda Wekundu wa Msimbazi hao wakamtangaza wakati wowote kuanzia sasa.

Imeelezwa kuwa, Wydad Casablanca, imekubali kumtoa mchezaji huyo kwa mkopo wa mwaka mmoja na hii ni baada ya mazungumzo kati ya Rais wa heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji na Rais wa klabu hiyo ya Morocco, Hicham Ait Menna baada ya dili hilo kushindikana awali.

Taarifa zinaeleza Klabu ya Simba italipa asilimia 100 ya mshahara wake pamoja na ada ya mkopo ya Dola 30,000 za Kimarekani.

SOMA NA HII  BAADA YA KUPOST PICHA AKIWA NA RONALDO..OMMY DIMPOZI ALAMBA HILI SHAVU MAN UTD...AWA MTZ WAKWANZA ...