Home Habari za michezo KUMWEMBE: MPANZU ANARINGA…..ASIPOJIANGALIA SIMBA WATAMCHOKA…..

KUMWEMBE: MPANZU ANARINGA…..ASIPOJIANGALIA SIMBA WATAMCHOKA…..

Habari za Simba leo

JANUARI mwaka huu, mambo yalionekana kuwa mazito Simba. Ni wakati ambao dirisha la usajili la Januari lilikuwa linasubiriwa ili Ellie Mpanzu aingie rasmi Msimbazi baada ya kuwa akifanya mazoezi na timu tangu aliposajiliwa.

Sajili nyingi zilionekana kufeli na hivyo Simba ilimhitaji Mpanzu naye akaitika na kuwafanyia walichotaka.

Ni kipindi hicho, watani zao walikuwa wanang’ara na mastaa wao kama kawaida, huku mashabiki wa Simba wakilaza matumaini yao kwa Mpanzu ambaye alikuja na wasifu mzuri klabuni.

Kwanza ni wasifu wa kuwa mmoja wa mastaa waliotamba DR Congo akiwa na AS Vita, lakini kabla ya kutua Msimbazi alikuwa amekwenda Ubelgiji kufanya majaribio na Genk.

Simba SCSiyo kitu kidogo sana kwa mchezaji kuhitajika kwa majaribio katika timu ya Ligi Kuu ya Ubelgiji kama Genk. Lazima awe ana kitu.

Simba ilimhitaji kama dereva anavyohitaji mafuta katika kituo cha mafuta. Na kweli. Hakuwaangusha. Akawa habari ya mjini. Simba walipata sehemu ya kusemea kupitia yeye. Walau wakawa na mtu wa kujitapa naye.

Wakasema Mpanzu alikuwa bora kuliko Pacome Zouzoua. Kwamba alikuwa bora kuliko Stephane Aziz Ki na Maxi Nzengeli. Ili mradi walimpata mtu wa kujivunia.

Mwishowe kabisa katika zile ‘hatuchezi’ ikaja kauli hauwezi kuwa bingwa bila ya kumkaba Mpanzu. Yanga ndio walikuwa wanasimangwa hivi wakati huo Mpanzu akiwa katika ubora wake. Hata hivyo, Yanga walichukua ubingwa mbele ya Mpanzu. Hakucheza wala nusu ya ubora wake. Katika mechi nzima alipiga shuti moja tu ambalo lilichezwa na Djigui Diarra.

Siyo mechi hiyo tu, mechi nyingi kubwa Mpanzu huwa anatoweka. Hata hivyo, mashabiki na viongozi wanampenda sana Mpanzu. Nadhani hapa ndipo kuna tatizo linaanzia. Kuna Wacongo wa aina mbili. Kuna Wakongo wanaojisikia na kuna wale wenye upole mwingi. Maxi Nzengeli ni Mkongo mwenye upole na adabu kubwa. Nyoshi El Saadat ni Mkongo mwenye majivuno.

Sijui nimweke Mpanzu katika kundi gani, lakini mtazamiko wake wa mwili siuelewi, hasa kwa sasa. Anaonekana kama vile hayupo uwanjani kimwili na kiakili. Anaonekana kama vile anapuuza mambo.

Kutokuwa katika kiwango ni jambo moja, lakini kuwa na lugha mbovu ya mwili ni jambo jingine. Mpanzu sio tu hayupo fomu, lakini anaonekana kama vile mwili wake na akili yake vipo mbali na wenzake.

Sijui kama ni mtu mwenye majivuno au hapana. Sijawahi kuwa naye karibu. Wakati mwingine tu wachezaji wanapitia masahibu yao. Lakini kwa kuanzia picha haikuanza vizuri kwake msimu huu baada ya kuchelewa kujiunga na kambi ya Simba pale Misri. Mashabiki walikuwa roho juu na inawezekana mwenyewe alikuwa anafurahia kwa sababu alikuwa amepima ni kwa kiasi gani ameishika timu.

Habari za Simba leoVyovyote ilivyo, Simba walikuwa wanamhitaji Mpanzu bora zaidi katika msimu huu mpya kwa sababu mbalimbali. Mashabiki na viongozi wanaamini wamemletea wenzake walio bora ili kufanya mambo yawe bora zaidi. Mpira wa kisasa unadhihirisha hivyo katika siku za karibuni. Kwenye ubora unaongeza ubora zaidi.

Yanga walikuwa bora na Aziz Ki wakamuongeza Pacome kutoka ASEC Mimosas. Wakaona haitoshi wakamuongeza Clatous Chama kabisa. Timu iliendelea kufanya mazuri zaidi. Simba wameongeza mastaa wengine kando ya Mpanzu, lakini ndio kwanza inaonekana kama vile nyota huyo anarudi nyuma badala ya kwenda mbele. Kifupi anawaangusha.

Nimeangalia kiwango chake cha msimu huu naona kimeendelea pale alipoishia katika msimu uliopita. Hajakuwa na maajabu mengi. Hana maamuzi mazuri uwanjani. Na katika kitu ambacho nimekuwa nikimlaumu Mpanzu tangu msimu ulioisha ni namna ambavyo amekuwa mbinafsi uwanjani. Sidhani kama anacheza sana kwa ajili ya timu.

Wakati mwingine juhudi zake binafsi zimekuwa zikiiisaidia Simba, lakini wakati mwingine anahitajika kurahisisha maisha kwa wengine kwa sababu ana kipaji kikubwa. Hili huwa halifanyi mara nyingi lakini kama akili yake ya kwanza ingekuwa kuwasaidia wenzake uwanjani basi wachezaji wengi wa Simba eneo la mbele wangekuwa wananufaika na Mpanzu.

Na kwa sasa wakati hatumwelewi vizuri Mpanzu ni vyema kumkumbusha kuna watu waliishika Simba vizuri zaidi yake. Kuna mmoja alikuwa Mganda mwingine alikuwa anatoka Msumbiji na mwingine anatoka Zambia. Waliishika Simba vyema kiasi walistahili kuringa katika siku za baadae.

Kuna huyu Mganda Emmanuel Okwi. Aliishika Simba vema kiasi kwamba mashabiki na viongozi walikuwa hawapumui juu yake. Waliishiwa pawa kwa mapenzi dhidi yake. Okwi kwa Simba alikuwa kama Diego Maradona na Argentina ya mwaka 1986 katika fainali za Kombe la Dunia pale Mexico. Alikuwa na mpango wake wa mtu mmoja. Mechi nyingi alikuwa anaamua yeye mwenyewe bila ya kuhusisha watu wengine.

Staili hii Waingereza huwa wanaita singlehandedly. Jeshi la mtu mmoja. Baadaye wakaja Mmakonde Jose Luis Miquissone na Mzambia Clatous Chama. Hawa pia waliishika Simba katika namna ya kushangaza na katika kitu kizuri zaidi ni waliishika Simba huku ikitamba robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mpanzu bado hajaishika Simba kiasi hicho. Ana bahati alikutana na baadhi ya wachezaji ambao hawakuwa hata na hadhi ya kuvaa jezi ya Simba. Akasimama na kuhesabiwa. Hata hivyo, hajawahi kuwa na utawala uliotukuka kama Okwi, Chama na Miquissone. Kwa hiyo anaweza kuweka maringo kando kidogo akaendelea kuwashika Simba.

Bahati mbaya mashabiki wetu wakati mwingine sio wanafiki. Wanaweza kukuhama dakika moja tu wakiona mambo hayaendi kama wanavyokutarajia. Hata nyakati fulani walimhama Chama. Kama mastaa wengine wakifanya vizuri basi unapikiwa msala ambao hauwezi kuubeba. Unaweza kujikuta unaishia kudaiwa unahujumu au unatumika.

Mpanzu apambane kuipeleka Simba inakostahili. Wamekuja kina Seleman Mwalimu, Morice Abraham, Jonathan Sowah na wengineo. Wanaweza kuwa wachezaji wazuri kuliko wale aliokuwa nao msimu uliopita. Ili atengeneze ufalme wake vizuri pale Simba inabidi aende juu ya hawa. Hivi ndivyo kina Okwi na Chama walitengeneza ufalme kwa miaka nenda rudi.

Ufalme wa miezi mitatu tu ambao aliutengeneza alipowasili unaweza kupotea kama akiendelea na kiwango hiki. Tusirudi kwa kina Okwi na Chama, amtazame tu hata Pacome ambaye wiki baada ya wiki ameendelea kuwa mchezaji yule yule tu, licha ya kwamba amezungukwa na mastaa wakubwa kando yake.

Vinginevyo wengine tutamchukulia kama Big G. Ukianza kuitafuna inakuwa tamu, lakini kadri ikiendelea kuwa mdomoni utamu unaondoka. Alianza vizuri haswa, lakini kadri tunavyosonga mbele anageuka kuwa mchezaji wa kawaida. Utamu wake unapotea.

Credit:- Edo Kumwembe/MwanaSpoti.

SOMA NA HII  CHEZA SLOTI YA BURSTING HOT 5 KASINO USHINDE KIRAHISI.