Home Habari za michezo BAADA YA MAYELE KUBEBA CAF….TUZO BONGO NI AIDHA AHOUA AU PACOME…LISTI YOTE...

BAADA YA MAYELE KUBEBA CAF….TUZO BONGO NI AIDHA AHOUA AU PACOME…LISTI YOTE HII HAPA….

Habari za Michezo leo

WAKATI Ligi Kuu Bara msimu uliopita ilipofikia tamati kulikuwa na mjadala mkubwa juu ya nani ni mchezaji bora wa msimu (MVP). Wapo waliamini Pacome Zouzoua wa Yanga anastahili na wengine walimpigia chapuo nyota wa Simba, Jean Charles Ahoua kubeba tuzo hiyo ya msimu.

Bahati mbaya ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilichelewa kuandaa hafla ya tuzo za msimu huo, hata hivyo, siyo kwamba vita ndiyo imeisha. Mziki umeanza upya baada ya TFF kutangaza Desemba 5 ndipo itakapokuwa siku ya kutoa tuzo hizo za msimu uliopita.

Majina ya Pacome, Ahoua sambamba na ya Dickson Job, Maxi Nzengeli wa Yanga na kiungo mshambuliaji wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ yapo katika kapu moja la tuzo hiyo ya MVP.

Tuzo hizo zinazokuja kutolewa wakati msimu mpya wa 2025-2026 ukiwa unazidi kushika kasi, hafla itafanyika kwenye Ukumbi wa Super Dome Masaki, jijini Dar es Salaam, huku zikigawanywa katika makundi matano yanayosubiria kuvuta hisia za wadau.

Makundi hayo ni ya tuzo za Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho FA, Ligi Kuu ya Wanawake na ligi nyingine, pamoja na za Utawala.

Kwa msimu wa 2024-2025, kutakuwa na tuzo moja mpya ambayo ni ya Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza nje ya Tanzania kwa upande wa Wanawake, ambayo kwa msimu wa 2023-2024, ilitolewa kwenye tuzo za TFF, ingawa ilikuwa upande wa Wanaume pekee.

Nyota watano wa Simba, Yanga na Azam wameteuliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025.

Katika orodha iliyotolewa na (TFF), wachezaji hao ni Dickson Job, Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli wa Yanga, Jean Ahoua wa Simba na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam.

Kwa msimu uliopita Ahoua aliisaidia Simba kumaliza nafasi ya pili akifunga mabao 16 akiwa ndiye Mfungaji Bora na kuasisti 10, huku Pacome, Job na Maxi wakiiwezesha Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya nne mfululizo, wakati Fei Toto aliibeba Azam kumaliza ya tatu Bara.

Mmoja wao mwenye bahati kulingana na turufu itakavyomuangukia, atabeba tuzo hiyo ambayo msimu wa nyuma ilibebwa na Stephane Aziz Ki aliyekuwa Yanga ambaye kwa sasa anakipiga Wydad Casablanca ya Morocco. Aziz KI alikuwa amepokea kijiti kutoka kwa Fiston Mayele aliyekuwa Yanga pia akicheza kwa sasa Pyramids ambaye naye aliipokea kutoka kwa Yannick Bangala aliyekuwa MVP wa 2021-2022 akiwa Yanga pia japo kwa sasa yupo AS Vita.

Ikitokea Pacome, Maxi au Job kama mmoja ataibuka na kutwaa tuzo hiyo itakuwa na maana, kwa misimu minne mfululizo MVP anatokea Jangwani, kitu kinachosubiriwa kwa hamu kuona kama Ahoua na Fei Toto watalizuia hilo au watalibariki.

Kwa upande wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi ya Wanawake, nyota watano wameteuliwa kuwania kinyang’anyiro hicho, ambao ni Donisia Minja, Stumai Abdallah (JKT Queens), Jeannine Mukandayisenga (Yanga Princess), Jentrix Shikangwa (Simba Queens) na Esther Maseke (Bunda Queens).

Tuzo ya Refa Bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025 inawaniwa na Ahmed Arajiga (Manyara), Saad Mrope (Dodoma) na Abdallah Mwinyimkuu wa Singida.

Kocha Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, wanaowania ni Fadlu Davids aliyekuwa Simba, kisha kuondoka na kujiunga na Raja Casablanca ya Morocco, Rachid Taoussi aliyekuwa timu ya Azam na Ahmad Ally wa kikosi cha maafande wa JKT Tanzania.

Katika Kombe la Shirikisho la (FA), Tuzo ya Mchezaji Bora inawaniwa na Clement Mzize na Stephane Aziz KI wa Yanga ambaye kwa sasa anaichezea Wydad Casablanca ya Morocco na kiungo nyota wa Singida Black Stars raia wa Ghana, Emmanuel Keyekeh.

Kwa upande wa Tuzo za Kipa Bora wa Kombe la Shirikisho la FA, wanaowania ni Djigui Diarra aliyeipa Yanga ubingwa huo kwa msimu wa 2024-2025, Amas Obasogie aliyeifikisha fainali Singida Black Stars na Yakoub Suleiman aliyekuwa JKT Tanzania.

Tuzo ya Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho la FA, yupo mchezaji mmoja tu wa JKT Tanzania, Mohamed Bakari aliyefunga mabao matano.

Katika Tuzo za Ligi Kuu ya Wanawake wanaowania Kipa Bora ni Asha Mrisho (Mashujaa Queens), Naijath Abbas (JKT Queens) na Rita Akarekor wa Yanga Princess.

Tuzo ya Chipukizi Bora wa Wanawake wanaowania ni Elizabeth Chenge (JKT Queens), Elizabeth Joseph (Alliance Girls) na Esther Maseke wa Bunda Queens.

Kocha Bora wa Ligi ya Wanawake, wanaowania ni Edna Lema wa Yanga Princess, Esther Chabruma wa JKT Queens na Yusuf Basigi wa Simba Queens, huku Stumai Abdallah wa JKT Queens akiwa ndiye mfungaji bora wa Ligi ya Wanawake baada ya kufunga mabao 27.

Tuzo ya timu yenye nidhamu Bora zinazowania ni JKT Queens, Yanga Princess na Ceasiaa Queens, huku wanaoshindania refa bora kwa upande wa Ligi ya Wanawake ni Tatu Malogo wa Tanga, Florentina Zabron wa Dodoma na Amina Kyando wa Morogoro.

Mwamuzi Bora Msaidizi wa Ligi ya Wanawake wanaowania ni Glory Tesha, Sikudhani Mkurungwa na Zawadi Yusuph, huku Tuzo ya Mchezaji Bora wa vijana chini ya miaka 20 ni Ashrafu Kibeku wa Azam, Luqman Mbala (Kagera Sugar) na Popah Mwatomdoa wa KenGold.

Wachezaji Mbwana Samatta (Le Havre), Novatus Dismas (Goztepe) na Saimon Msuva (Al-Talaba SC), wanawania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kiume anayechezea nje ya Tanzania.

Wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike anayecheza nje ya nchi ni Opa Clement anayeichezea FC Juarez ya Mexico, Diana Lucas wa Trabzonspor ya Uturuki na Enekia Kasonga anayecheza Mazatlan FC ya Mexico.

Wanaoshindania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi ya Championship ni Andrew Simchimba wa Geita Gold ambaye kwa sasa anacheza Mtibwa Sugar kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, Mwani Willy Thobias wa Mbeya City na Raizin Hafidh wa Mtibwa Sugar.

Tuzo ya mchezaji Bora wa First League, wanaowania ni George Elwin Komba na Moses Peter Kitandu wote wa Rhino Rangers na Ramadhani Hashimu Kalanje anayeichezea Tanesco inayoshiriki Championship, ambayo kwa sasa inajulikana kwa jina la B19.

Tuzo za Utawala zitakazotangazwa ukumbini, ni ya Mchezaji Gwiji, Tuzo ya Heshima Soka la Wanawake, Tuzo ya Rais na Tuzo ya Heshima.

Wanaowania Tuzo ya Kipa Bora wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2024-2025, ni Djigui Diarra wa Yanga, Moussa Camara wa Simba aliyeongoza kwa (Clean Sheets) nyingi akiwa nazo 19, sambamba na Patrick Munthary wa kikosi cha maafande wa Mashujaa.

Kwa upande wa Tuzo ya kiungo Bora wa Ligi Kuu, wanaowania ni Feisal Salum wa Azam, Jean Charles Ahoua wa Simba na Pacome Zouzoua wa Yanga.

Tuzo ya beki Bora wanaowania ni Dickson Job wa Yanga, Israel Mwenda wa Azam na Antony Tra Bi wa kikosi cha Singida Black Stars.

Chipukizi Bora wa Ligi Kuu, wanaowania ni Anthony Mligo aliyekuwa Namungo ingawa msimu huu anaichezea Simba, Bakari Msimu wa Coastal Union na Benno Ngassa aliyeichezea Tanzania Prisons msimu uliopita, japo kwa sasa yupo Dodoma Jiji.

Meneja Bora wa Uwanja wa Ligi Kuu Bara, wanaowania ni Ashraf Omar wa Meja Jenerali Isamuhyo unaotumiwa na Klabu ya JKT Tanzania na Godwin Israel anayehudumia Kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati, unaotumiwa na kikosi cha Fountain Gate.

Kamishina Bora wanaowania ni Abousufian Silia wa Iringa, Zakayo Mjema wa Arusha na Zena Chande kutoka Jiji la Dar es Salaam.

Tuzo ya timu yenye nidhamu bora kwa Ligi Kuu, zinazowania ni Kagera Sugar inayoshiriki Championship msimu huu, KMC na Namungo.

Seti Bora ya waamuzi wanaowania ni ya mechi kati ya Azam na Yanga ambao ni Ahmed Arajiga (mwamuzi wa kati), Kassim Mpanga (mwamuzi msaidizi namba moja), Hamdan Said (mwamuzi msaidizi namba mbili) na mwamuzi wa akiba, Nassoro Mwinchui.

Tuzo nyingine ya seti bora ya waamuzi ni ya mechi ya Singida Black Stars na Yanga ambao ni Ally Mnyupe (mwamuzi wa kati), Makame Mdogo (mwamuzi msaidizi namba moja), Sunday Komba (mwamuzi msaidizi namba mbili) na mwamuzi wa akiba, Isihaka Mwalile.

Seti nyingine ya waamuzi bora ni ya Azam na Singida Black Stars ambao ni Thabit Maniamba (mwamuzi wa kati), Ayoub Fulgance (mwamuzi msaidizi namba moja), Black Tubuke (mwamuzi msaidizi namba mbili) na mwamuzi wa akiba, Omar Bofu.

Mwamuzi Bora msaidizi wanaowania ni Hamdani Said kutoka Mtwara, Kassim Mpanga (Dar es Salaam) na Janeth Balama kutokea Iringa.

Mfungaji Bora ni Charles Ahoua wa Simba aliyefunga mabao 16, huku Tuzo ya Bao Bora la msimu, Kikosi Bora cha msimu, Tuzo ya mchezo wa kiungwana (Fair Play), zote kwa pamoja zitatangazwa usiku huo ukumbini katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo.

SOMA NA HII  ZA NDANII KABISA...MECHI SIMBA NA YANGA...MAREFA HAWA WOTE WANAWAKE