Home Habari za michezo ZA NDAAANIII KABISA….HII HAPA SABABU KUBWA YA PANTEV KUPIGWA CHINI SIMBA….

ZA NDAAANIII KABISA….HII HAPA SABABU KUBWA YA PANTEV KUPIGWA CHINI SIMBA….

Habari za Simba leo

Uamuzi wa Simba kuachana ghafla na Meneja wake Dimitar Pantev ambaye alikuwa mkuu wa benchi la ufundi, jana Jumanne, Desemba 2, 2025 unatajwa kuchangiwa na sababu tatu.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Simba imeanika kuwa imefikia makubaliano ya kuvunja mkataba wa Pantev na timu hiyo itakuwa chini ya usimamizi wa Selemani Matola kwa sasa wakati ikisaka Kocha Mkuu mpya.

“Uongozi wa klabu ya Simba umefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba na Meneja Mkuu Dimitar Pantev pamoja na Wasaidizi wake wawili.

“Kwa sasa kikosi kitabaki chini ya Kocha Selemani Matola wakati mchakato wa kutafuta Kocha mwingine undendelea,” imefafanua taarifa ya Simba.

Wakati taarifa hiyo ikitoka, chanzo kutoka ndani ya Simba kimefichua sababu tatu ambazo zimechangia kuifanya klabu hiyo kuachana na Pantev.

Sababu hizo ni upangaji usioridhisha wa kikosi na mbinu, kiwango kisichoridhisha cha timu na matokeo mabaya kwenye mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Inaripotiwa kwamba tangu uongozi wa Simba na hata wachezaji wengi wa timu hiyo hawakuwa wakifurahishwa na uamuzi wa Pantev kutotumia washambuliaji asilia wa kati katika mechi za timu hiyo jambo ambalo wanaamini linachangia timu kupata matokeo kwa tabu.

“Alifanya hivyo katika mchezo wa nyumbani dhidi ya Nsingizini ukaisha kwa sare ya bila kufungana. Baada ya hapo tukazungumza naye akatuahidi kubadilika lakini jambo la kushangaza akarudia, tena katika mechi muhimu ya kwanza dhidi ya Petro Luanda.

“Tulikuwa na uwezo wa kuimaliza ile mechi mapema lakini uamuzi wake ukatugharimu,” kimefichua chanzo ndani ya Simba.

Inadaiwa kwamba uamuzi huo umewagawa wachezaji ndani ya Simba hasa wale wa nafasi za ushambuliaji jambo ambalo uongozi umehofia lingeweza kukipasua zaidi kikosi chao na kukifanya kiwe na muendelezo wa kufanya vibaya.

Lakini pia bado Wanasimba wengi wanaonekana kutofurahishwa na ukosefu wa mabao ambao wachezaji mbalimbali wamekuwa wakionyesha katika mechi za ligi na zile za kimataifa wakiamini kwamba benchi la ufundi halitimizi vyema wajibu wake.

Sababu hizo mbili zinaonekana kuongezewa nguvu na ya tatu ambayo ni matokeo yasiyo mazuri ambayo Simba imepata katika mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Petro Luanda nyumbani na dhidi ya Stade Malien ugenini.

Simba ilianza kupoteza kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Petro Luanda na mchezo uliofuata juzi Jumapili ikafungwa mabao 2-1 na Stade Malien huko Bamako, Mali.

Matokeo hayo yameifanya Simba ishike mkia katika kundi D na inatakiwa kulazimika kufanya kazi ya ziada katika mechi nne zilizobakia ambazo inatakiwa kushinda ili iweze kutinga hatua ya robo fainali.

SOMA NA HII  KUHUSU NABI KUONGEZWA MKATABA YANGA..SENZO AFUNGUKA HAYA...ADAI WAPO VITANI KWANZA..