MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube, amejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zimbabwe kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zinazotarajiwa kufanyika nchini Morocco.
Dube amekuwa kwenye kiwango bora ndani ya Yanga katika michezo ya hivi karibuni, hali iliyoweka wazi ubora wake na kumfanya kuendelea kuaminiwa na benchi la ufundi la Zimbabwe.
Uwezo wake wa kufunga na kuandaa mabao, pamoja na mchango mkubwa katika ushambuliaji, umeonekana kuwa sababu kubwa ya kumrejesha kwenye majina ya wanaotegemewa na nchi yake.
Katika kikosi hicho, makipa walioitwa ni Washington Arubi wa Marumo Gallants, Elvis Chipezeze wa Magesi, pamoja na Martin Mapisa wa MWOS FC.
Safu ya kiungo imejumuisha nyota kadhaa wenye uzoefu na vijana chipukizi akiwemo Marvelous Nakamba wa Luton Town, Jonah Fabisch wa Erzgebirg Aue, Andrew Rinomhota wa Reading FC, Prosper Padera wa SJK Seinäjoki, Tawanda Chirewa wa Wolves na mshambuliaji mkongwe Knowledge Musona wa Scotland FC.
Upande wa ushambuliaji, mbali na Dube, wametajwa pia Bill Antonio wa KV Mechelen, Ishmael Wadi wa CAPS United, Tawanda Maswanhise wa Motherwell, Daniel Msendami wa Marumo Gallants, Washington Navaya wa TelOne, Macauley Bonne wa Maldon & Tiptree, Junior Zindoga wa TS Galaxy na Tadiwanashe Chakuchichi wa Scotland FC.
Kwa upande wa mabeki, majina kama Godknows Murwira, Emmanuel Jalai, Sean Fusire wa Sheffield Wednesday, pamoja na Teenage Hadebe wa FC Cincinnati yametajwa, sambamba na wengine akina Munashe Garananga, Gerald Takuwa, Isheanesu Mauchi, Brandon Galloway, Alec Mudimu na Divine Lunga.
Kwa ujumla, ujumuishwaji wa Dube kwenye kikosi hiki ni uthibitisho wa thamani yake na mwenendo mzuri aliouonyesha Yanga. Mashabiki wa Wananchi na wa Zimbabwe wanatarajia kumuona akitoa mchango mkubwa katika michuano ya AFCON 2025.