Home Habari za michezo AHMEDY ALLY AWATUPIA DONGO WATANI WA JADI

AHMEDY ALLY AWATUPIA DONGO WATANI WA JADI

42
0

MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba Ahmed Ally, ameibuka na kauli inayoonekana kuwachokoza watani wao wa jadi, Yanga, kufuatia taarifa zinazosambaa kuwa klabu hiyo ina mpango wa kumsajili kiungo mshambuliaji wa Wekundu wa Msimbazi, Morice Abraham.

Kauli ya Ahmed inakuja wakati ambao tetesi za usajili zimeanza kuchukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii, hususani zikihusisha wachezaji wa Simba kuhamia kwa wapinzani wao wakubwa, Yanga.

Hivi karibuni, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alijigamba hadharani kuwa klabu hiyo tayari imefanikiwa kuwanasa nyota wawili kutoka Simba, Morice Abraham na Elie Mpanzu kama sehemu ya wachezaji waliotajwa katika mipango hiyo.

Tamko hilo la Kamwe limezua mijadala mikubwa miongoni mwa mashabiki wa soka, huku wengi wakisubiri uthibitisho wa kweli juu ya hatma ya wachezaji hao na uhalisia wa madai hayo.

Kufuatia tetesi hizo, Ahmed Ally aliamua kuvunja ukimya kwa kuandika ujumbe mfupi lakini mzito kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, akisema: “Unaruhusiwa kutamani vitu vizuri ambavyo huna uwezo navyo.”

Ujumbe huo umetafsiriwa na wengi kama dongo lililoelekezwa moja kwa moja kwa Yanga, likionesha kuwa Simba haina mpango wa kumwachia mchezaji huyo muhimu kwa wapinzani wao wa karibu.

Kauli ya Ahmed pia inaashiria wazi kuwa Morice bado yupo chini ya mkataba halali na Simba  na kwamba atasalia ndani ya kikosi hicho kwa msimu mwingine licha ya presha na tetesi zinazoendelea nje ya uwanja.