Home Habari za michezo HIZI HAPA REKODI 5 KALI ZA YANGA BAADA YA LIGI KUU KUSIMAMA…SIMBA...

HIZI HAPA REKODI 5 KALI ZA YANGA BAADA YA LIGI KUU KUSIMAMA…SIMBA MHHH……

24
0
Habari za Yanga leo

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kupisha Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazoanza kuanzia Desemba 21, mwaka huu huko Morocco, mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, wameweka rekodi ‘kali’ tano ikiwa imecheza mechi sita tu.

Yanga inaongoza kwa kufunga mabao mengi mpaka sasa, kushinda michezo mingi mfululizo, ndio timu pekee imepata penalti nyingi, imeshinda mechi nyingi nyumbani na kuruhusu mabao machache.

Kwa mujibu wa takwimu za michezo , Yanga imefunga mabao 12, yakiwa ni mabao mengi zaidi katika ligi, ikiwa sawa na JKT Tanzania ambayo ina idadi kama hiyo ya mabao.

Hata hivyo, Yanga imecheza mechi sita tu wakati ‘Maafande’ wa JKT Tanzania wameshuka dimbani katika michezo 10 mpaka sasa.

Yanga ina rekodi nyingine safi ya kushinda michezo mingi mfululizo ikiwa imefanya hivyo mara nne.

Baada ya kulazimishwa suluhu dhidi ya Mbeya City Septemba 30, mwaka huu, Yanga ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, halafu ikatoa kichapo cha mabao 4-1 kwa KMC baadaye ikawafunga Fountain Gate mabao 2-0 na kuidungua Coastal Union ya Tanga goli 1-0.

Katika rekodi hiyo iko sawa na Simba, ambayo nayo ilishinda michezo minne mfululizo ya mwanzo, kabla ya rekodi hiyo kuzimwa Desemba 7, mwaka huu, ilipotandikwa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC.

Yanga pia ina rekodi ya kuwa timu pekee iliyopata penati nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa, zote ikizitumia.

Imepata penalti mbili, kati ya nane zilizotolewa na waamuzi kwenye Ligi Kuu na zote ikiziweka kwenye kamba.

Ilipata penalti yake ya kwanza Novemba 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam ilipocheza dhidi ya wenyeji, KMC mfungaji akiwa ni straika raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), Andy Boyeli, vigogo hao wakishinda mabao 4-1.

Yanga ilipata penalti nyingine Desemba 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex ilipowakaribisha Fountain Gate, ikafungwa na Prince Dube, Yanga ikishinda mabao 2-0.

Kama vile haitoshi, Yanga ndiyo timu pekee iliyoshinda michezo mingi ya nyumbani msimu huu mpaka sasa, ikifanya hivyo mara nne, kwa kuichapa Pamba Jiji mabao 3-0, Mtibwa Sugar mabao 2-0, KMC mabao 4-1 na Fountain Gate, mabao 2-0.

Mabingwa hao watetezi ndiyo timu pekee iliyoruhusu mabao machache katika vyavy zake, ikiruhusu bao 1-0 tu, ilifanya hivyo Novemba 9, mwaka huu ilipocheza dhidi ya KMC na kushinda mabao 4-1.

Katika msimamo wa ligi, Yanga yenye pointi 16 iko kwenye nafasi ya pili ikilingana pointi na Pamba Jiji huku JKT Tanzania wakiongoza na pointi zao 17 kibindoni.