Home Habari za michezo YANGA BORA INAKUJA HERSI AFICHUA MAZITO

YANGA BORA INAKUJA HERSI AFICHUA MAZITO

22
0

RAIS  wa Klabu ya Young Africans (Yanga), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vilabu Afrika (ACA) na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya FIFA, Eng. Hersi Said, leo anakutana na Rais wa Klabu ya Sevilla, José María del Nido Carrasco, katika kikao kinachotajwa kuwa cha kihistoria kwa mustakabali wa Yanga.

Mkutano huo unatajwa kuwa na ajenda nzito zinazolenga kuimarisha maendeleo ya Klabu ya Yanga kwa viwango vya kimataifa, huku ukitarajiwa kufungua milango ya ushirikiano mpana kati ya klabu hiyo ya Tanzania na vigogo wa soka barani Ulaya.

Vyanzo vya karibu vinaeleza kuwa mazungumzo hayo yatahusisha masuala ya kubadilishana uzoefu wa kiufundi, maendeleo ya vijana, pamoja na mifumo ya uendeshaji wa klabu kwa viwango vya kisasa vinavyotumika katika soka la kulipwa.

Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa uongozi wa Yanga wa kuhakikisha klabu hiyo inaendelea kupiga hatua kubwa kimataifa, sambamba na kuinua hadhi ya mpira wa miguu wa Tanzania kwa ujumla.

Mbali na kikao hicho, Eng. Hersi atapata fursa ya kutazama mchezo wa Ligi ya Hispania kati ya Sevilla na Levante, utakaopigwa katika dimba la Ramón Sánchez Pizjuán, akiwa pamoja na Rais wa Sevilla.

Tukio hilo linaendelea kuwapa matumaini mashabiki wa Yanga kwamba mwelekeo mpya wa uongozi wao unalenga kuifanya klabu hiyo kuwa mfano wa kuigwa Afrika na kuleta enzi mpya ya mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi