Home Habari za michezo YANGA YAJIPANGA KIVITA DHIDI YA TRA UNITED

YANGA YAJIPANGA KIVITA DHIDI YA TRA UNITED

38
0

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kushuka dimbani kesho Januari 6, 2026 kuikabili TRA United katika mchezo wake wa pili wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea visiwani Zanzibar.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo pamoja na umuhimu wa pointi katika hatua ya makundi.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara wataikaribisha TRA United katika dimba la New Amaan Complex, ambapo timu zote mbili zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Uzoefu wa ligi moja umeifanya kila timu kufahamu vyema mbinu na uwezo wa mpinzani wake, jambo linaloongeza presha na mvuto wa pambano hilo.

Yanga wanaingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu chungu ya kupoteza alama tatu mbele ya TRA United kabla ya kuanza kwa msimu huu, wakati timu hiyo ikiitwa Tabora United.

Hali hiyo inawafanya Wananchi kuwa makini zaidi na kuutambua mchezo huo kama mtihani mgumu unaohitaji umakini wa hali ya juu.

Kwa upande wao, TRA United nao wanakumbuka uchungu wa kufungwa na Yanga katika dimba lao la nyumbani msimu uliopita. Hilo linawapa motisha ya ziada ya kutaka kulipa kisasi na kuonyesha mabadiliko waliyojiwekea kuelekea msimu huu.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Gocalves, amesema kikosi chake kimefanya maandalizi ya kutosha na kiko tayari kwa changamoto hiyo.

Amesisitiza  kuwa lengo lao ni kufanya vizuri katika kila mchezo bila kujali muda wa maandalizi wa mpinzani.

“Dhamira yetu kubwa ni kuwa tayari kila wakati. Haijalishi wenzetu wamepata muda mrefu wa kujiandaa kuliko sisi, ni lazima tuwe tayari kushinda. Ninaamini baada ya mchezo wa kesho tutatinga hatua ya nusu fainali,” amesema Pedro kwa kujiamini.

Hata hivyo, Yanga watakosa huduma ya wachezaji kadhaa akiwemo Clement Mzize ambaye anaendelea na mazoezi ya kurejea kwenye kiwango bora baada ya majeraha, pamoja na Mudathir aliye karibu kurejea uwanjani.

Aidha, Lassine Kouma na golikipa Khomein nao bado wapo kwenye majeraha, lakini kocha Pedro anaamini kikosi alichonacho kina uwezo wa kufanya vizuri na kuendeleza mwendo mzuri katika mashindano hayo.