Klabu ya Simba imeweka wazi kuwa haiko tayari kufanya usajili wa kukurupuka katika dirisha dogo la usajili, kuwa kila hatua inayochukuliwa inalenga kuimarisha kikosi kwa kuzingatia mahitaji halisi ya benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Steve Barker.
Akizungumza kuhusu mikakati ya klabu hiyo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally, amesema uongozi unafanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha usajili unaofanyika unaongeza ushindani na ubora ndani ya kikosi, badala ya kuongeza majina bila sababu za msingi.
Kwa kipindi cha hivi karibuni, Simba imekuwa ikihusishwa na majina mbalimbali ya wachezaji, akiwemo kiungo Clatous Chama, ambaye kumekuwa na tetesi za kurejea kwake Msimbazi. Hata hivyo, Ahmed ameeleza kuwa kwa sasa taarifa nyingi zinazosambaa mitandaoni ni tetesi za kawaida za kipindi cha usajili.
“Kinachoonekana mitandaoni ni sehemu ya kelele za dirisha dogo. Kuhusu Chama au mchezaji mwingine yeyote, ukweli utajulikana pale mambo yatakapokuwa yamekamilika,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa Simba inalenga kufanya maboresho madogo lakini yenye tija, ili kujiandaa vyema na ushindani mkubwa katika mashindano yanayokuja.
“Tunaangalia maboresho machache yatakayoongeza nguvu ya timu. Wale waliopo kwenye mpango wetu, mambo yakikaa sawa, tutawaweka wazi kwa wakati muafaka,” amesisitiza.
Ahmed ameongeza kuwa Simba haitafanya usajili kwa shinikizo la kufunguliwa kwa dirisha, bali itaangalia kama kikosi kilichopo kinamridhisha kocha.
Endapo kutabainika mapungufu, ndipo usajili wa mchezaji mwenye mchango wa moja kwa moja utafanyika, na si kwa lengo la kumpa muda mfupi kabla ya kumtoa kwa mkopo.