UONGOZI wa Yanga umeweka wazi mikakati yake ya kuimarisha kikosi kabla ya kibarua kigumu dhidi ya Al Ahly ya Misri, huku ukithibitisha kukamilisha usajili wa wachezaji wawili wa kigeni kwa ajili ya kuongeza nguvu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema hadi sasa klabu hiyo imeshawatambulisha wachezaji watatu, lakini bado kuna nyota wawili wa kigeni ambao wanatarajiwa kutua nchini hivi karibuni na kujiunga na kikosi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo mkubwa.
Kamwe ameeleza kuwa nyota hao wawili watakuwa tayari kabla ya Yanga kusafiri kwenda Misri, ambapo timu hiyo itavaana na Al Ahly Januari 23, 2026, katika mchezo wa hatua ya makundi unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Amefafanua kuwa kabla ya Januari 21, siku ambayo kikosi kitapanda ndege kuelekea Misri, klabu itawatambulisha rasmi wachezaji hao wawili ili wawe sehemu ya kikosi kitakachosaka matokeo chanya ugenini.
Akizungumzia ushiriki wa Yanga kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kamwe amesema lengo halikuwa kushinda kombe hilo bali lilikuwa ni kutumia mashindano hayo kama sehemu ya maandalizi, hatua ambayo imesaidia kufanikisha malengo ya kiufundi ya timu.
“Wachezaji wetu wote, wakiwemo waliokuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa, wamepata nafasi ya kucheza mechi za ushindani kwa ajili ya kuongeza utimamu na maandalizi kabla ya kukutana na Al Ahly,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa Yanga pia inatarajia kucheza mechi ya Ligi Kuu baada ya ratiba kupangwa vizuri, jambo litakalosaidia zaidi katika maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.