Home Habari za michezo MPANZU ATANGAZA HATARI JUMAPILI

MPANZU ATANGAZA HATARI JUMAPILI

45
0

NYOTA wa Simba SC, Elie Mpanzu, ameonyesha kiwango kikubwa cha hamasa na ari ya kupambana kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumapili.

Kiungo huyo ameweka wazi kuwa yuko tayari kutoa kila alichonacho kwa ajili ya timu na mashabiki wake, akiahidi kiwango cha juu uwanjani.

Simba inatarajia kuikabili Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi muhimu kabla ya safari ya kwenda Tunisia kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance Sportive de Tunis utakaochezwa Januari 24.

Mchezo huo dhidi ya Mtibwa Sugar wanaocheza Jumapili unaonekana kuwa na umuhimu mkubwa katika kujenga morali ya kikosi.

Kupitia ujumbe aliouchapisha, Mpanzu amesema ana motisha ya hali ya juu na hawezi kusubiri siku ya Jumapili kufika ili kuingia uwanjani na kutekeleza kile alichokijiandaa kwa muda mrefu.

Amesisitiza kuwa huu ni wakati wa kurejesha tabasamu na furaha kwa Wanasimba waliokuwa na matarajio makubwa kwa timu yao.

Mpanzu ameongeza kuwa anatambua vyema shinikizo na matarajio ya mashabiki wa Simba, jambo linalompa nguvu ya ziada ya kujituma zaidi kila siku mazoezini. Kwa mujibu wake, dhamira ya kikosi ni kuhakikisha kinapata matokeo chanya na kuonyesha ushindani wa kweli.

Kiungo huyo amesisitiza kuwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ni muhimu si kwake binafsi tu, bali kwa timu nzima, kwani ni fursa ya kuonyesha umoja, mshikamano na kiu ya ushindi waliyonayo kama familia moja ya Simba SC.

Mpanzu amewahakikishia mashabiki kuwa yeye pamoja na wenzake wako tayari kupambana kwa nguvu zote uwanjani, wakilenga kutekeleza maelekezo ya benchi la ufundi na kupigania heshima ya klabu.

Amewaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu, akisisitiza kauli mbiu ya “Mabingwa Wekundu” kama ishara ya imani na matumaini ya ushindi mkubwa Jumapili.